Prime
Kauli ya Wenje ishu ya Msigwa kurudi Chadema
Mwanasiasa Ezekia Wenje akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi leo Jumatatu Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Msigwa aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema, alishindwa kwenye uchaguzi wa Kanda uliopita na miezi kadhaa baadaye alihamia CCM, mwaka 2025 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025.
Dar es Salaam. Mwanasiasa Ezekia Wenje amesema mbunge wa zamani wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa alimpa taarifa binafsi za uamuzi wake wa kurejea katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), siku chache kabla ya kuweka hadharani uamuzi huo.
Wenje amebainisha hayo katika mahojiano maalumu aliyofanya na Mwananchi jana Mei 24, 2026, ikiwa ni siku moja baada ya Msigwa kutangaza kurejea kwenye chama hicho alichokiongoza akiwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa na mjumbe wa kamati kuu.
Msigwa, aliyejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), Juni 30, 2024, alitangaza kurejea Chadema Mei 23, 2026 akisema ni baada ya kutafakari kwa kina kuhusu hali ya haki na utu wa binadamu hapa nchini.
Katika taarifa yake aliyoitoa Jumamosi iliyopita kupitia mitandao ya kijamii, Mchungaji Msigwa amesema amefikia uamuzi huo baada ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, dhuluma na ukosefu wa utu yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Katika ujumbe wake, mwanasiasa huyo amewaomba radhi wanachama wa Chadema pamoja na Watanzania wote ambao waliwahi kuumizwa au kukatishwa tamaa na msimamo wake wa awali alipokuwa nje ya chama hicho.
Msigwa aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema, alishindwa kwenye uchaguzi wa Kanda na miezi kadhaa baadaye alihamia CCM mwaka 2025.
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, alishiriki kwenye kampeni za mgombea mwenza wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, baadaye akaenda kwenye kampeni za mgombea urais, Samia Suluhu Hassan kabla ya Mei 23, 2026 kutangaza kurejea Chadema.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam, Wenje aliyaangazia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii, ikiwamo suala la Msigwa kurejea Chadema akisema Msigwa alimtafuta kwa simu siku chache zilizopita kupitia WhatsApp.
Wenje amesema katika mazungumzo yao, Msigwa alimtaka asishtuke atakaposikia uamuzi wake huo kwenye vyombo vya habari.
“Alinipigia simu juzi (Mei 22) nikawa bize, sikupokea. Baadaye nikamtafuta nikamuuliza kuna nini nimeona umenipigia sana, akasema nataka nikuage ili usije ukashtuka,” amesema Wenje na kuongeza:
“Nikamuuliza unaaga unaenda wapi, akasema narudi Chadema, akanieleza sababu zake ambazo lazima niziheshimu, siwezi kuziweka hadharani.”
Kwa mujibu wa Wenje, Msigwa alimweleza kuwa ameamua kurejea Chadema baada ya kutafakari kwa kina huku sababu zake akisema ni binafsi na zinapaswa kuheshimiwa.
“Nilimwambia kama umeamua hivyo na unaona inakufaa basi sawa, siasa bado ni pana,” amesema Wenje.
Akizungumzia sababu za wanasiasa kuhama na kisha kurejea, Wenje amesema katika maisha na siasa, watu hupitia nyakati tofauti na kufanya uamuzi kulingana na mazingira wanayokutana nayo.
“Maisha ni majira na wakati, ukikaa na watu mbalimbali unajifunza kwamba kuna space (nafasi) lazima uiheshimu,” amesema.
Hata hivyo, amesema kurejea kwa mwanasiasa katika chama alichowahi kukihama mara nyingi uamuzi huo huambatana na changamoto ya kurejesha imani kwa wanachama.
“Ukiondoka ukarudi, watu hawawezi kukuamini asilimia 100 kama awali,” amesema Wenje akitolea mfano uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo baadhi ya wanasiasa waliokuwa wamehama kutoka CCM kwenda Chadema baadaye walirejea tena CCM baada ya uchaguzi, lakini walikumbana na mashaka kutoka kwa wanachama wa zamani.
“Wakati huo ndipo likaibuka neno la kukatwa mkia, Rais Magufuli (hayati John Magufuli) kwenye sherehe za CCM Singida aliwaambia wale walioondoka kwenda Chadema kisha wakarudi kwamba wamekatwa mkia,” amesema.
Mbunge huyo wa zamani wa Nyamagana (Chadema) amesema licha ya hali hiyo, amemtakia kila la heri katika hatua yake mpya ya kisiasa.