Kilichoharibu kura laki nne hadharani

Muktasari:

Baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuuu kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wiki iliyopita ilielezwa kuwa kura 402, 248 zimekataliwa kwa sababu mbalimbali.

Dar/Mikoani. Kutokujua kusoma, uelewa mdogo na ukosefu wa elimu ya mpiga kura, ni mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kura katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.

Baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuuu kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wiki iliyopita ilielezwa kuwa kura 402, 248 zimekataliwa kwa sababu mbalimbali.

Kutokana na tangazo hilo, Mwananchi imelazimika kutafuta sababu za kukataliwa kwa kura hizo na kwanini tatizo hilo limekuwapo kila uchaguzi unapofanyika.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NEC, Clarence Nanyaro alisema kwa ujumla tatizo hilo linatokana na elimu ya uraia na ya mpiga kura kutofika kwa wananchi kwa usahihi.

Alisema baadhi ya wananchi hawajui nafasi yao katika jamii na wanapokwenda kupiga kura hawatambui wanakwenda pale kama nani na wanafanya nini.

Pia alisema sababu ya pili ni baadhi ya wapiga kura kuwa na chuki na wagombea fulani, hivyo anapompigia kura mtu anayemtaka pia anamtoboa yule mwingine asiyemtaka na kuharibu kura bila kujijua.

 

Ushuhuda vituoni

Msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Kinondoni, Valence Urassa alisema eneo lake kura nyingi ziliharibika kutokana na wapiga kura kuweka alama ya vema kwa mgombea zaidi ya mmoja huku wengine wakiweka tiki zilizovuka nje ya kiboksi.

“Ukiweka tiki ikapitiliza, maana yake kura inaleta mgogoro, tunashindwa kutambua nani aliyepigiwa kura hiyo, mawakala wanavutana kuhusu kura za aina hii, mwisho tunaziweka kando kama kura zilizokataliwa,” alisema Urassa.

Sababu nyingine, alisema ni mpiga kura kutoweka alama yoyote kwa mgombea anayemtaka, kuchanganya kura kwenye boksi, kwa mfano mtu kuweka kura ya urais kwenye kisanduku cha udiwani na ya udiwani kwa mbunge, au ya ubunge kwa rais.

Msimamizi mkuu wa kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Kibonde-Maji, Mbagala, Stanslaus Massawe alisema katika semina walizopewa, kura inayoharibika ni ile ambayo mpiga kura ameweka alama ya vema kwa wagombea wawili, kutokuweka alama yoyote au kuweka tiki iliyovuka kisanduku cha mgombea.

Massawe alisema sababu kubwa ya kuharibika kwa kura hizo ni wananchi wengi kutokuwa na chaguo maalumu la mgombea wanayemtaka.

 

Mtazamo wa wasomi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa, Profesa Kitila Mkumbo alisema mwaka huu kura zilizoharibika siyo nyingi ukilinganisha na chaguzi zilizopita kwa sababu kuna majimbo ambayo hakukuwa na kura zilizoharibika.

“Ninadhani tatizo bado ni elimu kwa mpiga kura, NEC na vyama vya siasa bado havijawekeza vya kutosha kwa wapiga kura ambao ndio walengwa wakuu wa uchaguzi,” alisema Profesa Mkumbo.

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi na asasi zilizopewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura hazikufanya kazi zake vizuri.

“Watanzania hawana uelewa sawa juu ya kupiga kura ukizingatia kuwa na hasira juu ya mgombea wa chama fulani.

“Uwepo wa polisi na usalama, imechangia wapiga kura kukosa uhuru, hivyo kupiga kura kwa hofu na haraka jambo lililosababisha kuharibika kura hizo,” alisema Mbunda.

 

Elimu mjini

Mkazi wa Kijitonyama, Stephania Saad alisema watu waishio mijini wamepata elimu ya kutosha ya kupiga kura ukilinganisha na vijijini kwa sababu ya kuwa na urahisi wa upatikanaji wa taarifa muhimu.

Livingstone Mallya, mkazi wa Mabibo alisema kukatika kwa umeme kumechangia elimu ya mpiga kura kutowafikia walengwa wote kwa sababu elimu hiyo ilikuwa inatolewa zaidi kwa njia ya redio na televisheni.

 

Kilichotokea Arusha

Asilimia zaidi ya 60 ya wanawake wa jamii ya wafugaji wilayani Monduli na Longido mkoa wa Arusha, hawajui kusoma na kuandika na hilo limechangia kuharibika kwa kura zao nyingi.

Mratibu mradi wa Fahamu, Ongea Sikilizwa, Martha Katau alisema walibaini hali hiyo katika makongamano waliyofanya kabla ya uchaguzi katika wilaya za Monduli na Longido kwamba tatizo la elimu ni kubwa katika jamii ya pembezoni, hivyo ni muhimu jamii hiyo kujulishwa haki zao. Mwanasheria wa kujitegemea mkoani Arusha, Simon Lepilal alisema ni muhimu elimu kupewa kipaumbele katika jamii za pembezoni ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na fursa sawa ya kuchagua viongozi.

 

Magu

Hoja hiyo inaungwa mkono na msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Magu, Ntiniki Paul kuwa kura nyingi ziliharibika kutokana na watu wengi kutokujua kuandika huku wakikataa kupewa msaada. Alisema elimu ya mpiga kura pia ilikuwa ndogo katika eneo hilo huku baadhi ya watu wakitumia jazba wakati wa kupiga kura kwa kumchora mgombea mwingine kwa sababu tu hampendi.

 

Kwingineko

Hali hiyo ilitokeza pia katika majimbo ya Kondoa Mjini, Serengeti Mtwara, Rufiji, Kibiti na Tandahimba.

 

Imeandaliwa na Florence Wisso, Haika Kimaro, Azory Gwanda, Mary Sanyiwa, Mussa Juma, Anthony Mayunga, Shakila Nyerere, Jesse Mikofu, Borrice Bwire, Emma Kalalu na Ephraim Bahemu.