Kiti cha dhahabu kwenye makaa ya moto
Nimefuatilia kwa muda mrefu wito wako unaowataka viongozi wa vyama na Serikali wawe wabunifu na wanaokwenda na wakati.
Nakuunga mkono, kwani wakati wa bla-bla ulikwisha kupita, sasa tupo kwenye zama za sayansi na teknolojia. Uongozi wa propaganda za pande zinazokinzana utatuzuia kufikia malengo yetu, na pengine utatusambaratisha. Sorry, nimeanza na moto mkali maana sote tunavurugwa na hali inavyoendelea kwenye chama kinachounda Serikali yetu.
Leo ningependa turudishe kumbukumbu nyuma, maana bila kuichimbua mizizi ya fitina, hawa mafahali wanaokinzana juu yetu watatuvunja vichwa. Kwanza waelewe kuwa siasa ni kama dini.
Ni kada inayoongozwa na wito anaopewa mja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Pamoja na kuwapo kwa vyuo vya siasa na vya dini, shughuli hizi haziwezi kufanywa na wanataaluma wasio na wito.
Katika historia ya kisiasa na kiimani, vyeti na shahada hutajwa mwishoni. Hapo kale hatukutajiwa PhD za mitume wateule wa Mwenyezi Mungu, wala za wanasiasa hata wale waliotingisha dunia kwa matendo yao yaliyotukuka. Pia ikumbukwe jinsi kada hizi mbili zilivyolazimika kwenda pamoja pale mwanzoni. Mataifa na Falme zilikuwa zikiongozwa na wateule wa Mungu katika enzi zile.
Kwenye msafara wa mamba kenge hujipenyeza. Kutokana na imani ya wananchi juu ya viongozi wao, watu wabaya walitengeneza fursa haramu na kupandikiza udanganyifu katika tasnia hizo.
Tunasoma kwenye vitabu jinsi manabii wa ukweli walivyopata shida na wanasiasa waongo, na manabii waongo walivyopata wakati mgumu kwa wanasiasa wa kweli. Hata sasa kwenye siasa zetu tunaona mitikisiko ya kidunia inayotokana na tasnia hizo mbili.
Kwa sababu shughuli hizo mbili zinashika roho za watu kwa ukaribu sana, mataifa ya kale yaliandika simulizi za mifano ili kuwahami raia dhidi ya watu wasio waaminifu kwao. Warusi ambao ni mababa wa siasa zetu za Ujamaa na Kujitegemea walitunga hadithi nyingi za watoto na za watu wazima ili kuwahami na wanasiasa uchwara. Naomba nikupe kipande kifupi cha simulizi mojawapo.
Simulizi inaanzia kwa msafiri aliyeharibikiwa na gari yake msituni. Alihangaika kuifufua bila mafanikio, ndipo akaamua kutafuta msaada mahali penye dalili ya kuishi watu. Kwa mbali aliona moshi hewani, dalili ya uhai. Aliufuata moshi huo uliofuka umbali wa kilomita kadhaa katikati ya msitu.
Ule moshi ulitokea katika mgahawa wa wenyeji uliokuwa ukikesha kuuza supu. Msafiri wetu aliufikia, akakaribishwa na kuletewa karatasi ya bei za vyakula (menu). Menu ilisomeka: “Supu ya (a) kichwa cha mwindaji Sh 1,000; (b) kichwa cha mzururaji Sh2,000; kichwa cha mwanasiasa Sh20,000.”
Akajua kuwa ameingia choo cha mazombi! Kwa kujihami ili asionekane mgeni akajifanya kulalamika: “Mi nilitaka kichwa cha mwanasiasa lakini bei imenishinda...” Mhudumu akamjibu kwa ukali: “We kichwa cha mwanasiasa unakichukulia poa? Inanigharimu siku nzima kukisafisha na siku nzima tena kukiivisha!”
Msimulizi wa hadithi hii alitaka kuonesha uchafu wa baadhi ya wanasiasa. Tunakubaliana kwamba wapo wanasiasa waliotukuka, lakini tukubaliane kwamba wapo wa uchwara wanaojivika sura za wenzao. Ni mara ngapi tumeshuhudia mwanasiasa anavyoweza kufa mara mbili. Anaweza kufa kisiasa kwenye chama kimoja, akazaliwa upya kwenye chama hasimu.
Katika siku za nyuma mwanasiasa mmoja aliondoka kwenye chama tawala kwa kelbu za kutisha. Akaweka nadhiri ya kumuoa mama yake mzazi iwapo angebadilisha uamuzi na kulamba matapishi yake. Aliporudia chama tawala na kuulizwa utayari wake wa kutimiza ahadi yake akajibu “mama yangu alikwisha kufariki!”
Jeuri ya aina hii hufanywa na wale wanaochukulia siasa kama mchezo. Anaweza kucheza rafu kuinusuru timu yake kwa lengo la kuipandisha thamani yake. Lakini kwa vile hana jipya, atawakusanya wadhaifu kama yeye na kuanzisha rafu dhidi ya viongozi thabiti ndani ya chama chake. Linapojengeka kundi la wanasiasa wa aina hii, lazima chama kiende mrama. Utamaduni wa watu wasio wabunifu unaeleweka.
Lakini upande wa pili unanifikirisha zaidi. Wahanga wa vikundi vya wanafiki ndani ya vyama ni viongozi waadilifu. Unapoona watu wenye majukumu makubwa na nyeti kama makatibu wakuu wa vyama wanakikimbia kiti, ujue kuna bomu huko uvunguni.
Siyo rahisi kwa chama kikubwa kama CCM kumuamini mtendaji asiyejielewa katika nafasi nyeti kama hiyo, lakini maamuzi ya kujiuzulu na sababu wanazotoa zinathibitisha kuwa kiti hicho ni sawa na kaa la moto.
Orodha ya makatibu wakuu waliojiuzulu ama kutiwa msukosuko ni ndefu. Kumbukumbu kwa uchache zinaonesha makatibu wakuu wawili tu (Pius Msekwa na Rashid Kawawa 1977-1990) ndio walioondoka kwa amani katika majukumu yao. Kuanzia 1990 mpaka leo hakuna aliyetoka salama. Tena basi wengine wakikitumikia chama kwa muda mfupi kuliko ilivyotarajiwa.
Hata ukitazama kwa macho ya mbali, unauona wazi “ukaburu” ndani ya chama. Yaelekea kuna “wanachama” na “wenyechama” wanaosiginana ndani ya mtungi mmoja. Kama sababu ni kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii, mchafuaji huyo ni nani hasa? Tuna uhakika gani iwapo amemaliza shughuli yake au la? Nini matokeo ya moto wanaowashiana ndani ya mtungi waliomo?