Lema afichua sababu vijana kushindwa kuoa, kuwapeleka watoto kwa bibi zao

Muktasari:

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema wapinzani wataendelea kuhimiza maendeleo kwa wananchi siyo kwa sababu ya kuutaka ubunge, ila wanasukumwa na mapenzi mema kwa nchi, kwa faida ya vizazi vijavyo.

Kiteto. Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema wapinzani wataendelea kuhimiza maendeleo kwa wananchi siyo kwa sababu ya kuutaka ubunge, ila wanasukumwa na mapenzi mema kwa nchi, kwa faida ya vizazi vijavyo.

Lema ameyasema hayo jana Jumtano Juni 7, 2023 mbele ya mamia ya wananchi mjini Kibaya kwenye mkutano wa Chadema.

"Nilitaka kuuawa nikakwepa, nilienda jela mara nyingi, nimeharibiwa biashara zangu, nimekimbia na watoto nikakamatwa na kutakiwa kurudishwa hapa nchini," amesema Lema.

"Unakimbia na watoto hujui unakoenda mke wako anakuuliza tunakwenda wapi unamwambia twende mpaka Nairobi tutamkuta Mungu anatusubiri. Kukimbia nchi ni kubaya sana usiombe. Tumerudi tunaendelea kuwaambia Watanzania na kuwahimiza siyo kwa sababu tunataka ubunge ila ni mapenzi mema kwa vizazi vya nchi hii.

"Siku hizi mtoto anakuwa hata kuoa hawezi, anaenda kumpa binti mimba akizaliwa mtoto anapelekwa kwa bibi yake, hakuna bibi nchi hii ambaye halei mjukuu, vijana hawawezi kuishi na wake zao kwa sababu ya umaskini," amesema Lema na kuongeza;

“Nchi nzima vijana wamekuwa bodaboda, vijana watakufa baada ya miaka 20 kwa sababu ya kukimbiza upepo, vifua, nyonga, na figo vitaathirika tu katika mazingira hayo; kwangu biashara ya pikipiki siyo biashara nzuri kwa usafiri wa umma,” amesema.

Lema ameilaumu Serikali kwa kukosa mipango mizuri ya kuajiri watu na kwamba imeshindwa kuweka mikakati ya kila kijana akitoka shule afanye kazi yenye staha na badala yake bodaboda ndiyo imekuwa kimbilio.

Kwa upande wake aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kibaya mjini, Ramadhani Mwamba amesema tatizo kubwa hapa nchini haswa Kiteto ni mipango mibovu ya afya na kukiwa hakuna uhakika wa tiba.

"Leo hii mtu ukiugua ghafla hesabu ni kifo hicho kama huna pesa nchi hii unakufa, hapa Tanzania kuna kila kitu madini, mbuga za wanyama misitu lakini kwanini hatuendelei? Ni kwa sababu ya ubinafsi wa watawala wetu ambao wao watoto wanasoma nje na kutibiwa nje," amesema Mwamba.

Mkutano wa Lema Kiteto ni mwendelezo wa mikutana anayofanya ya kisiasa nchini kuzungumza na wananchi kuhusu mustakabali wa maisha ya watu na umuhimu ya kufanya maamuzi sahihi na ya busara.