Lowassa agoma kujibu swali la Richmond

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akihutubia wananchi wa kijiji cha Mvumi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini hapo katika Jimbo la Mtera wilayani Chamwino, mkoani Dodoma jana. Pamoja naye ni Mgombea Ubunge Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.  Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Lowassa, ambaye amekuwa akitoa hotuba fupi zisizozidi dakika 20 kwenye mikutano yake, jana aliamua kutohutubia na badala yake aliruhusu wananchi wamuulize maswali alipokuwa kijiji cha Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Dodoma. Mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa jana aliruhusu maswali kwenye mkutano wake wa kampeni, lakini akakataa kujibu swali lililomtaka aelezee kilichotokea kwenye sakata la Richmond, akisema swali hilo “halina maana”.

Lowassa, ambaye amekuwa akitoa hotuba fupi zisizozidi dakika 20 kwenye mikutano yake, jana aliamua kutohutubia na badala yake aliruhusu wananchi wamuulize maswali alipokuwa kijiji cha Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Waziri huyo mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, amekuwa hazungumzii sakata hilo na inapotokea kulizungumzia amekuwa akieleza kuwa alijiuzulu kisiasa kuilinda Serikali ya CCM na kwamba ushiriki wake ulitokana na maagizo kutoka juu.

Jana, baada ya kutoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali, Michael Makanyi alitaka kufahamu kama Lowassa, ambaye anagombea urais kwa tiketi ya Chadema, anahusika katika sakata hilo linalohusu kuipa Richmond Development Company ya Marekani zabuni ya kufua umeme wa dharura wakati nchi ilipokumbwa na tatizo kubwa la ukosefu wa nishati hiyo mwaka 2006.

“Ulipokuwa Waziri Mkuu ulijenga hospitali ngapi. Wewe unatuhumiwa katika Richmond na tatu Wamasai wamekuwa na tabia ya kufanya vurugu na kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima. Sasa kama umeshindwa kuwatuliza Wamasai huko kwenu, utaweza kumaliza vipi migogoro ya ardhi?” aliuliza Makanyi kwenye mkutano huo uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mvumi kwenye Jimbo la Mtera ambalo ni ngome ya CCM.

Akijibu maswali hayo, Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka miwili kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata hilo, alisema: “Maswali yako mawili ya mwisho hayana maana (swali la Richmond na Wamasai), ila la kwanza najibu.

“Ilani ya CCM ilikuwa ikizungumzia afya na elimu, lakini tulianza na elimu. Tulijenga shule katika kila kata.”

Mbunge huyo wa Monduli alitakiwa kuzungumzia sakata hilo muda mfupi baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu Richmond, akirejea kwenye ripoti aliyoishika ya Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe kuchunguza suala hilo.

Lissu aliwaeleza wananchi hao kuwa ripoti hiyo haikumtaja Lowassa kuhusika na sakata la Richmond.

“Ndiyo maana hawampeleki mahakamani licha ya kuwa (Lowassa) alijiuzulu miaka minane iliyopita,” alisema Lissu.

Lissu alisema waliohusika katika sakata la Richmond na kutajwa kwenye ripoti ya Dk Mwakyembe walikuwa ni aliyekuwa waziri na naibu waziri wa Wizara ya Nishati na Madini na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo.

Pia alimpongeza Lowassa kwa mtindo wake wa kuruhusu wananchi kumuuliza maswali, huku akiwaeleza wananchi kuwa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli hawezi kutoa nafasi kama hiyo.

Katika mkutano huo, Lowassa, ambaye alipanda jukwaani saa 6:15 mchana, alizungumzia kwa ufupi Ilani ya Uchaguzi ya Chadema na Ukawa na kisha akatoa nafasi ya maswali matatu kutoka kwa wananchi katika mkutano huo uliohudhuliwa na mamia ya watu, wakiwamo vijana wasiozidi 10 waliokuwa wakipinga kila jambo lililokuwa linazungumzwa mkutanoni hapo.

Wakati akiwa Waziri Mkuu, mwaka 2007, Lowassa aliwahi kuruhusu swali katika mkutano uliofanyika Ukerewe, mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Aron Wambura wa Shule ya Sekondari ya Pius Msekwa, alimuuliza wamekuwa wakiwaambia kuwa mshika mawili moja humponyoka na kuwa vijana ni taifa la kesho, hivyo wasome ili kulitumikia Taifa.

“Vipi wao (viongozi) wamekuwa wakirundikiana vyeo zaidi ya kimoja kama kumteua Dk Alex James Msekela kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati pia ni mbunge?”

Swali hilo Lowassa hakulijibu.

Katika mkutano wa jana, mkazi mwingine wa kijiji hicho, Daniel Makabali alimuuliza Lowassa alikisaidiaje kijiji cha Mvumi kutatua tatizo la maji na barabara wakati akiwa Waziri Mkuu, akihoji: “Leo hii unataka kutusaidia, utawezaje wakati kipindi hicho ulishindwa?”

“Wananchi wa Mvumi mna mambo mengi sana,” alisema Lowassa huku akicheka.

“Nilikuja hapa nikiwa waziri na pia nimewahi kuja kumtembelea (Waziri Mkuu wa zamani, John) Malecela. Nimewahi kuja mara kadhaa katika hopitali kubwa iliyopo hapa. Nimejitahidi kwa uwezo wangu wote kushughulikia matatizo ya hapa na wananchi wote wa Tanzania. Nawashukuru kwa mapokezi yenu nawashukuru kwa maswali yenu,” alisema Lowassa.

Baada ya kujibu maswali hayo, Lowassa aliwataka wananchi hao kupanda treni ya mabadiliko kwa maelezo kuwa akiwa rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, elimu itakuwa bure na bora.

Lowassa pia alifanya mikutano ya kampeni Bahi, Chilonwa na Dodoma Mjini.

Awali Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alimshukia Jaji Joseph Warioba ambaye hivi karibuni aliwaponda makada wa CCM waliohamia upinzani kuwa wamepungukiwa.

“Ninawashangaa watu wanaosema kuwa tunaohama CCM, tumepungukiwa. Mtu kama Warioba ambaye ameshakuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusema maneno haya inaonyesha ndani ya CCM kuna matatizo makubwa sana,” alisema Sumaye.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM ikipata asilimia 20 ya kura katika baadhi ya mikoa, itakuwa na bahati kubwa kwa kuwa sasa wananchi wameamua kubadilika.

“Tunaotetea wanyonge, tunaambiwa tumechanganyikiwa. Nilikwenda shule kwa ajili ya kulitumikia Taifa langu na wananchi masikini. Ni upuuzi kuamini kuwa upinzani ukichukua madaraka nchi haitatawalika. CCM wasitishe watu wajiandae kuachia madaraka,” alisema Sumaye.

Alisema ndani ya CCM vigogo wanalindana kwa kuambiana “kula rushwa taratibu”, kwamba hakuna anayeweza kumkamata mwenzake kwa maelezo kuwa mtandao wa rushwa umeshakuwa mkubwa.

“Jaribuni kuichagua Ukawa muone, hakika hamtarudi tena CCM na mtajuta kwa kutowachagua wapinzani kwa muda mrefu. Dk Magufuli hawezi kupambana na rushwa ndani ya CCM maana rushwa ndani ya chama kile ni kama mtandao wa simu,” alisema Sumaye.

Aliyekuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga alisema ameacha mafao ya uwaziri unaoisha Novemba mwaka huu kutokana na “hali kuchafuka” ndani ya CCM na ndio maana akajiunga Chadema.