Maazimio 15 Kamati Kuu Chadema haya hapa, yakumbushia fedha za ruzuku
Muktasari:
- Miongoni mwa maazimio hayo ni kupinga zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi.
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeazimia mambo 15 likiwemo la kuitisha Baraza Kuu la chama hicho na kuendelea na operesheni ya Katiba Mpya katika visiwa Pemba na Unguja.
Mengine ni kuwashukuru Watanzania wanaokiunga mkono chama hicho kupitia mikutano ya hadhara, kupinga zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi.
Mbali na hayo Kamati Kuu imeitaka Serikali kushusha gharama za mafuta, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikilipe chama hicho malimbikizo ya fedha za ruzuku.
Akitangaza maazimio hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema Kamati Kuu iliyoketi kuanzia Juni 28 hadi 30 imeazima kuhitisha Baraza Kuu la chama hicho litakalofanyika Septemba 15 mwaka huu ambayo ni siku ya kimataifa ya demokrasia, na kutoa uamuzi mkubwa.
"Ni siku ya kufanya uamuzi mkubwa kuhusu haki, uhuru, demokrasia na mabadiliko nchini ili kutekeleza kazi na kuhimiza majukumu ya chama kwa mujibu wa ibara 7.7 ya Katiba ya Chadema," amesema Mnyika.
Mnyika amesema Kamati Kuu imeazimia kuendeleza operesheni Katiba Mpya, Free Tundu Lissu katika visiwa vya Unguja na Pemba, huku kikiwaalika Watanzania wote kuendelea kushiriki shughuli za kisiasa kwa kujiunga na kukichangia na chama hicho.
Aidha, Mnyika amesema kamati kuu ilijadili kauli ya Katambi na kujiridhisha zuio hilo linakiuka ibara ya 18, 20, 26 ( 1) na 29 ( 1)-( 2)& ( 5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya mtu kujieleza, kujumuika, kutii na kufuata Katiba ya nchi.
"Kamati kuu inasisitiza si Katambi wala Waziri Mkuu mwenye mamlaka yoyote ya kikatiba na kisheria ya kumwamuru Mkuu wa Jeshi la Polisi kuzuia mikutano," amesema Mnyika.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti Katambi alinukuliwa akisema hajavunja sheria wala Katiba bali hayuko tayari kuona Taifa linaangamia kwa kuacha kundi la watu wachache wenye masilahi binafsi ambalo linakiuka haki za wananchi wengi.
"Pia, Kamati Kuu inataka Serikali kushusha bei ya mafuta ili kuleta unafuu kwa Watanzania," amesema Mnyika.
Malalamiko dhidi ya viongozi
Pia, John Mnyika, amesema viongozi wa chama wenye malalamiko dhidi ya viongozi wenzao wanapaswa kufuata taratibu za chama kwa kuwasilisha malalamiko rasmi yenye ushahidi na kuyawasilisha katika vikao vya chama, badala ya kuyapeleka kwenye vyombo vya habari na mitandaoni.
Mnyika amesema hatua zilizochukuliwa dhidi ya baadhi ya wanachama na viongozi zilizingatia Katiba, kanuni na maadili ya Chadema.
Aliongeza kuwa mwanachama yeyote ambaye hajaridhika na maamuzi hayo ana haki ya kukata rufaa kupitia utaratibu uliowekwa na chama.
Ameeleza kuwa kabla ya matukio hayo, uongozi wa chama ulikuwa umepokea taarifa za kuwapo kwa watu waliokuwa wakiwashawishi baadhi ya viongozi kufanya mikutano na waandishi wa habari kwa kupewa fedha ili kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wa chama.
Kwa mujibu wa Mnyika, mazingira hayo yalionyesha kuwa kulikuwa na mpango wa kuchafua chama na viongozi wake, jambo lililofanya hatua zilizochukuliwa kuwa za haraka kutokana na kile alichokiita viashiria vya usaliti na matumizi ya rushwa.
Mnyika amesema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kusimamishwa kwa baadhi ya wanachama waliokuwa wakihoji matumizi ya fedha za michango ya chama na kutaka Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, aondolewe madarakani.
Amesema fedha za Tonetone zipo salama na kila zinapokusanywa kwanza hupelekwa benki, ili kudhibiti matumizi yake kwa mujibu wa taratibu.