Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Malisa asimulia mafunzo, machungu ya siku 183 alizokaa gerezani

Muktasari:

  • Mchungaji Godfrey Malisa ameyasema hayo Mei 29, 2026 wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi siku tisa baada ya kuachiwa huru kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, likiwamo la uhaini.



Moshi. Zikiwa zimepita siku tisa tangu alipoachiwa huru, Mchungaji Godfrey Malisa amesema kipindi cha siku 183 alizokaa gerezani kilikuwa chuo cha mafunzo, huku akishauri kufanyika kwa marekebisho katika mfumo wa utoaji msamaha kwa wafungwa ili uwaguse wengi zaidi.

Malisa amesema akiwa huko alikutana na wafungwa waliokaa magerezani kwa muda mrefu, baadhi yao kwa miaka 15 hadi 18, huku wengine wakiwa ni watu wenye ulemavu ambao huendelea kuwa na matumaini tasa kila misamaha inapokuwa ikitangazwa.

Hata hivyo, amesema mara nyingi misamaha hiyo haiwagusi wafungwa hao, jambo ambalo huwasababishia maumivu makubwa na kukata tamaa.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 29, 2026 katika mahojiano maalumu na Mwananchi, siku tisa baada ya kuachiwa huru kufuatia kukabiliwa na mashtaka mbalimbali, likiwamo la uhaini, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Katika simulizi yake, Dk Maliaa ameeleza kwamba katika siku alizokuwa gerezani, amejifunza mambo mengi na alipitia nyakati ngumu katika kipindi ikiwemo kutokuwa huru kwenye sikukuu zote kama krismasi, mwaka mpya na pasaka.

“Mimi sikuwa gerezani, nilikuwa chuo cha mafunzo. Tunahitaji kurekebisha sheria za nchi hii ili watu wanaopelekwa magerezani wapelekwe kwa makosa waliyoyafanya. Lakini sheria za sasa unaweza kufanya unachotaka kufanya na ukaishia gerezani na kupewa adhabu ambayo hukustahili hata kidogo.

“Kwa hiyo, wafungwa wengi waliopo magerezani wapo pale kwa sababu tu ya udhaifu wa sheria zilizopo,” amesema Mchungaji Malisa.

Amesema watu wengi magerezani ni wa kawaida, amekaa nao miezi sita, wengi waliopo huko ni kwa sababu ya udhaifu wa sheria ambazo zinatakiwa zirekebishwe.

Amesema amewaona wafungwa walivyokuwa na matumaini makubwa wakati misamaha ikitolewa, lakini unakuta hiyo haiwagusi wanabaki na maumivu makubwa.

“Ni vizuri kurekebisha mfumo wa utoaji misamaha ili iwaguse wafungwa wengi. Hili jambo ndilo linalowaumiza wafungwa wengi. Kwa mfano unakuta kuna gereza lenye watu 600 lakini wanaopewa msamaha ni wawili.

“Unakuta kuna wafungwa wamekaa kule miaka 15 au 18, wengine ni walemavu, wote wapo kule na wana sifa kabisa za kupewa msamaha, hawa watu wangestahili msamaha. Utaratibu wa kutoa msamaha uangaliwe upya,” amesema Mchungaji Malisa. 


Alichokikosa akiwa gerezani 

Mchungaji Malisa amesema lengo la gereza lolote duniani ni kumnyima mtu uhuru hadi pale mamlaka husika zinapotoa uamuzi wa namna ya kuingia na kutoka kwa wafungwa na kwamba hali hiyo ilimuumiza.

“Lengo lolote la gereza duniani ni kukunyima uhuru mpaka wenyewe waamue unaingiaje na unatokaje. Nikiwa kule gerezani ‘nilimisi’ sana uhuru na ndio kilichoniumiza sana.

“Sikukuu ya Krismasi ilinikuta jela, mwisho wa mwaka mpya ukanikuta jela, pasaka yote ilinikuka jela, inauma sana hii, it's very painful (inaumiza sana), halafu ukizingatia hakuna kosa nililofanya,” amesema Mchungaji Malisa. 


Kesi ya uhaini

Mchungaji Malisa alikamtwa Novemba 19, 2025, akikabiliwa na tuhuma za uhaini  na kufunguliwa kesi namba 00028333 ya mwaka 2025 mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Kulingana na hati ya mashitaka, alidaiwa kuwa Novemba 16, 2025, huko eneo la Miembeni katika Wilaya ya Moshi, akiwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, alitenda kosa la uhaini.

Inadaiwa alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kushiriki katika kusanyiko lisilo halali kwa lengo la kumtisha mtendaji wa Serikali ya Tanzania na alidhihirisha nia hiyo kwa kitendo chake cha kutamka na kuchapisha maneno haya:

“Samia Suluhu Hassan…kabla ya kufika Desemba 9, uwe umekwishajiuzulu…Kama utang’ang’ania madaraka itakapofika Desemba 9 kutakuwa na maandamano ambayo hayajawahi kutoka katika bara la Afrika.”

Mchungaji Malisa alidaiwa kunukuliwa akisema: “Lengo la maandamano ni kumuondoa Samia Suluhu Hassan madarakani na maandamano hayo yatakuwa ni maandamano ya mwendelezo mpaka utakapotoka madarakani.”

Katika kesi hiyo nyingine, namba 000028411 ya mwaka 2025, Malisa alituhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mitandao yake ya YouTube, akidai Rais Samia Suluhu Hassan anatakiwa kijiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.

Hata hivyo, Mei 19, mwaka huu, mahakama hiyo ilimuachia huru kwa kumfutia mashitaka hayo.


Watanzania wamtia moyo

Mchungaji Malisa amesema akiwa gerezani, familia yake, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wakimtembelea na kumpa moyo.

“Nawashukuru watu wote walioniombea kipindi nipo gerezani, ndani na nje ya nchi, Watanzania wengi walikuwa wanaomba na kujihusisha na namna moja au nyingine ili niweze kuachiliwa huru, niwashukuru wote waliohusika, Mungu awabariki sana,” amesema. 

Malisa anayejiita kada wa CCM, amesema: “Nawashukuru Watanzania, wamenipa sapoti kubwa sana, mimi bado nipo kwa neema ya Mungu na hilo naliacha mikononi mwa Mungu.”


Akomalia ni mwanaCCM

Akisisitiza kuhusu kufutiwa uanachama ndani ya CCM, Mchungaji Malisa amesema bado yeye ni mwanachama halali wa chama hicho na uthibitisho anao.

“Ule ulikuwa uamuzi feki kwa sababu hakuna kosa lolote nililolitenda, bado mimi ni mwanachama wa CCM na nina kadi yangu halali na nimelipa ada za chama mpaka mwaka 2027. Mtu akitaka nimthibitishie namthibitishia,” amesema Mchungaji Malisa. 

Ameongeza kuwa: “Sijafutiwa uanachama na kila kikao kilichoketi hakikuwa na uhalali wala mamlaka, kilikwenda kinyume kabisa na taratibu.”

Februari 10, 2025, Dk Malisa alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kupinga uamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.

Uamuzi wa kumfukuza uanachama ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, akiegemea uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro uliomwondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.

“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza uamuzi halali uliofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, uliofanyika Januari 19, 2025,” alieleza Mollel.

Katibu huyo alisema Mchungaji Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kwa kuwa kudai mkutano mkuu uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja katiba, jambo ambalo si la kweli.


Maisha nje ya siasa

Dk Malisa amesema safari yake ndefu ya maisha iliyomfanya aishi nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 20, ilianzia Marekani akiwa mwanafunzi na baadaye kuendelea na huduma ya kiroho na taaluma ya ufundishaji katika vyuo mbalimbali.

Amesema akiwa Marekani, alisoma na baadaye kuwa mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wakati huo akihudumu pia kama mhadhiri katika taasisi za elimu ya juu, akiwa amejikita katika kufundisha na kuwajenga wanafunzi kielimu na kiimani.

Amesema badaye alipanua uzoefu wake kwa kusafiri na kuishi katika nchi tofauti ikiwemo Japan na nyingine, hatua iliyompa mtazamo mpana wa maisha na huduma.

Akieleza uamuzi wake wa kurejea nyumbani, amesema aliuchukua baada ya kuchoka kuishi ng’ambo, na watu walimshangaa aliporudi nchini.

“Nilichoka kwa sababu nimesafri nchi nyingi sana, nilifika mahali nikachoka, ni kama kulikuwa hakuna msukumo wa roho wa Mungu ndani yangu kwamba nirudi Tanzania, watu walishangaa nilipoamua kurudi nyumbani lakini hatimaye nilirudi,” amesema. 

“Nilifundisha kwa miaka 10 huko Marekani na nilipokuja Tanzania nilifundisha chuo cha kanisa kule Mwika kwa miaka mitano na taaluma yangu ni kufundisha na nimekuwa mhadhiri katika vyuo mbalimbali hapa Tanzania, mfano Mzumbe, Udom, Eckernforde kule Tanga baada ya kurudi nchini 2010.”


Itaendelea kesho…