Prime
Malisa: Safari ya demokrasia ya kweli bado ni ndefu
Mchungaji, Godfrey Malisa akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwanachi.
Muktasari:
- Asema vyama vya siasa na taasisi za kijamii zinatakiwa kujipanga na kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu na thamani ya demokrasia ili waamke na kudai haki zao za kidemokrasia.
Moshi. Mchungaji Godfrey Malisa amesema Tanzania bado ina safari ndefu kuifikia demokrasia ya kweli kutokana na kuwepo kwa makundi mawili ya watu wanaoitaka na wasioitaka, hali ambayo amesema ni tatizo kubwa linalolikabili Taifa.
Kutokana na sintofahamu hiyo, amesema mazingira ya kisiasa yaliyopo sasa yakiendelea kubaki kama yalivyo, mgombea urais wa CCM ndiye atakayeendelea kushinda na vyama vingine vitaendelea kuwa na nafasi ndogo ya kufanya mabadiliko makubwa kisiasa.
Malisa amebainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo amezungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii kuhusu mustakabali wa taifa.
Alifanya mahojiano hayo Mei 29, 2026, zikiwa zimepita siku tisa tangu Mahakama imwachie huru, baada ya kukaa gerezani kwa zaidi ya miezi sita kutokana na kesi ya uhaini iliyokuwa ikimkabili.
Dk Malisa amesema Watanzania wanapaswa kuamka na kuendelea kuipigania demokrasia yao kwa njia ya amani na utulivu, badala ya kufanya fujo au kuchoma mali.
“Tanzania bado tuna safari ndefu sana. Tunatakiwa kuendelea kuipambania demokrasia ya Tanzania. Bado tuna safari ndefu kwa sababu kuna wanaotaka demokrasia na kuna wasioitaka demokrasia,” amesema Malisa.
Amesema, “Bahati mbaya wale wasioitaka demokrasia wana uwezo mkubwa wa kuizima na kuigeuza kwa manufaa yao wenyewe, kwa hiyo bado kuna tatizo kubwa katika kuifikia demokrasia ya kweli.”
Malisa amesema ili kufanikisha hilo, ni muhimu kuwaamsha Watanzania ambao bado wapo usingizini kuipambania demokrasia yao.
“Hatua muhimu kuliko zote ni kuwaamsha Watanzania, hawa raia wa kawaida kabisa ambao wapo kwenye usingizi mzito, kwa sababu hawajali sana. Mtanzania anachojali leo ni atakula nini, atalala wapi, kibarua gani atapata kinachoweza kumpa pesa.
“Ukizungumzia demokrasia anakwambia, ‘Mimi nitakula demokrasia?’ Huyu mtu hajui kabisa kwamba yupo vile alivyo kwa sababu hakuna demokrasia,” amesema Mchungaji Malisa katika mahojiano hayo.
Nini mifanyike
Akishauri nini kifanyike, Dk Malisa amesema vyama vya siasa na taasisi za kijamii vina nafasi kubwa ya kujipanga na kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu na thamani ya demokrasia, ili waamke na kudai haki zao za kidemokrasia.
“Sio kwa kufanya fujo, kuchoma vitu au nini. Kwangu mimi, huko sio kudai demokrasia, bali ni kuleta vurugu nchini, jambo ambalo silikubali. Lakini unaweza kuwafundisha watu wakaamka na kujua hali ilivyo, kwa sababu Watanzania wengi hawajui haki zao kabisa.
Hawajui hata kwamba Katiba inawaruhusu kutoa maoni yao bila kuhojiwa na chombo chochote. Hawajui, wanaogopa hata kusema wasije wakafuatiliwa,” amesema Mchungaji Malisa.
Amesema: “Wale wanaozima demokrasia wamefanikiwa sana kuwatia watu hofu na kuwafanya waogope. Tukidai demokrasia kwa amani na utulivu, kwa kufuata Katiba ya nchi, tutafanikiwa kabisa.”
Hata hivyo, DkMalisa amesema vyama vingi vya siasa bado havijajipata, hali ambayo amesema inaonekana wazi kwa sababu wananchi wengi hujiunga navyo wakitarajia kukuta misimamo thabiti ya kupambania masuala ya kijamii na maendeleo ya wananchi, lakini wanachokikuta ni tofauti kabisa.
“Vyama vingi vya siasa hapa nchini havijajipata bado. Nasema hivyo kwa sababu unakuta mtu anajiunga na chama fulani akitegemea atakuta kuna misimamo ya kupambania masuala ya kijamii, lakini anakuta kitu tofauti kabisa. Mara nyingi vinasubiri uchaguzi na baada ya hapo hakuna kinachoendelea. Vyama vya namna hiyo haviwezi kufika mbali,” amesema Malisa.
Amesema: “Mfumo wa siasa katika nchi hii unamlazimisha mtu ili awe kiongozi lazima awe amejiunga na chama fulani. Sasa vyama vingeweza kuwa jukwaa zuri la kupambania mapungufu yaliyopo, lakini cha kushangaza haviko hivyo.
“Hata nilipoenda CCM, ambako nipo mpaka sasa, niliona kwamba lile ni jukwaa zuri zaidi la kupambana ndani ya CCM yenyewe na nje ya CCM. Hata CCM inahitaji kurekebishwa, na hili nimelisema sana. Inahitaji msaada kama vilivyo vyama vingine. Ina dola, lakini hakuna uhuru,” amesema Mchungaji Malisa.
Amesema haja yake si kuwa ndani ya chama fulani bali kuona nchi inakuwa huru, na kwamba hadi sasa hali hiyo haijafikia.
CCM itaendelea kushinda
Mchungaji Malisa amesema mazingira ya kisiasa yaliyopo hivi sasa yakibaki kama yalivyo, mgombea urais wa CCM ndiye atakayeendelea kushinda, huku akidai kuwa vyama vingine vina nafasi ndogo ya kufanya mabadiliko makubwa kisiasa.
“Mazingira tuliyonayo kama yataendelea hivi siku zote, mgombea urais wa CCM ndiye atakayeshinda. Vyama vingine visahau. Sivioni kama vina nia thabiti ya kutaka urais katika nchi hii, labda kwa mbali sana Chadema.
“Nasema hivyo kwa sababu CCM ina nguvu ya fedha, rasilimali na imejikita kila kona ya nchi hii, na ndiyo imeunda Serikali, hivyo inakuwa ngumu,” amesema Mchungaji Malisa.
Ameongeza kuwa: “Inawezekana kuiondoa CCM madarakani, lakini ni shughuli kubwa. Inakuwa ngumu zaidi kwa sababu hata hivi vyama vingine sivioni vina mwelekeo wowote. Wanachosubiri ni uchaguzi ufike waonekane, majina yao yatangazwe kuwa waligombea urais. Kipindi hiki walipewa hata magari ya kuzunguka, lakini ukifuatilia baada ya Oktoba, vyama hivyo vinafanya nini?”
Mchungaji Malisa ni nani?
Mchungaji Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alipogombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia chama cha TLP. Mwaka 2015 aligombea urais kupitia Chama cha Kijamii (CCK) na baadaye akagombea uspika.
Mwaka 2018 aligombea ubunge wa Kinondoni kupitia TLP, na mwaka 2020 aligombea ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Baada ya uchaguzi huo alijiunga na CCM hadi mwaka 2025 alipotimuliwa. Hata hivyo, ameendelea kusisitiza kuwa yeye bado ni kada wa CCM.
Mwaka 2022, Malisa alijitosa kuchukua fomu na kuwa miongoni mwa makada tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Hata hivyo, Februari 10, 2025, Mchungaji Malisa, ambaye ni mwanazuoni mwenye shahada ya uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kupinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Uamuzi wa kumfukuza ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, akitekeleza uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro uliomuondolea sifa za kuendelea kuwa mwanachama.