Mbowe, Lissu kuongoza ziara ya Chadema Kanda ya Kusini

Muktasari:

  • Mbowe, Lissu na Mnyika kushambulia Kanda ya Kusini ikiwa ni mwezi mmoja tangu Chama cha ACT Wazalendo kilipofanya ziara lkatika mikoa hiyo.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kufanya ziara ya siku sita katika mikoa miwili ya Kanda ya Kusini.

Ziara hiyo itakayoanza Aprili 15 hadi 20 mwaka huu itaongozwa na viongozi wa kuu wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, Makamu wake, Tundu Lissu na Katibu Mkuu John Mnyika.

Januari mwaka huu Rais Samia aliruhusu mikutano ya hadhara iiliyokuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani.

Chama hicho kinafanya ziara katika mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu Chama cha ACT Wazalendo kilipofanya ziara huko.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 12,2023 Katibu wa Kanda ya Kusini, General Kaduma amesema ziara hiyo ni muendelezo wa mikutano ambayo ilishafanyika kwenye Kanda nyingine tangu Rais Samia Suluhu Hassan aliporuhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.

Amesema pamoja na ziara hiyo kuwa muendelezo wa uzinduzi wa mikutano kwenye Kanda lakini pia ina umuhimu wake kwa kuwa tangu Mwenyekiti atoke mahabusu Machi 2022 ajafanya ziara mikoa hiyo.

 “Toka mwenyekiti atoke mahabusu hajafika Kusini, lakini ikumbukwe wakati anakamatwa Mwanza alikuwa ametokea Kusini hivyo anakuja kukamilisha kazi aliyokuwa ameianza”amesema Kaduma.

Amebainisha kuwa pamoja na mambo mengine ziara hiyo inalenga kuhamasisha wanachama kujiandikisha kwenye mfumo wa kidigitali na kushiriki chaguzi zinazoendelea ndani ya chama.

“Kama Kanda ya Kusini tuna programu yetu ambayo itakuja kutamgazwa kabla ya kuzinduliwa, tunajua Kusini ni wakulia wa ufuta, korosho, mihogo na mazao mengine lazima kama chama tuhakikishe tunakuwa na mkakati wa kuwasaidia wakulima,”amesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kanda hiyo, ziara hiyo itakakuwa na timu mbili ikianzia majimbo ya Kilwa Kusini ikiongozwa na Mbowe wakati Lissu na Mnyika wa wakiwa Kilwa Kaskazini, Mchinga na Lindi mjini.

Majimbo mengine ni Nachingwea, Mtama, Liwale, Tandahimba, Mtwara Vijijini, Mtwara mjini, Newala Mjini na Masasi Mjini.