Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbunge asimulia kilichomliza kwenye uchaguzi

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Dkt. Neema Majule

Dodoma. Ingawa jina lake halikuwamo kwenye orodha ya awali ya wagombea wa Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Neema Majule anasimulia jinsi mabadiliko ya dakika za mwisho yalivyompa ushindi uliomtoa machozi hadharani.

Katika simulizi yake, Dk Majule anasema machozi yaliyomtoka hayakutokana na huzuni wala majonzi, bali mshangao wa kupata jambo ambalo hakulitarajia katika maisha yake ya kisiasa.

Julai 30, 2025, mwanasiasa huyo, alitangazwa mshindi wa Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM tukio liliambatana na kilio mbele ya wajumbe, viongozi na makada wa chama hicho.

Katika mahojiano yake maalumu na Mwananchi, Dk Majule anasema hajui hata machozi yake yalikotokea, hata naye anashangaa na kujiuliza ilikuwaje akalia kwa sauti.

"Ni kweli nililia kwa sauti, nilimwaga machozi ambayo sijui yalitoka wapi na wakati mwingine nikikaa natafakari lakini huenda Mungu alipanga iwe hivyo kwa siku husika," anasema Dk Majule.


Ilivyokuwa

Julai 29, 2025 majira ya jioni, aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Siasa, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, alitangaza majina ya wagombea Ubunge Viti Maalum na siku iliyofuata, Julai 30, 2025, ikawa ni siku iliyopangwa na chama hicho kwa ajili ya uchaguzi.

Haikushangaza jina la Dk Majule kutoonekana kwenye orodha ya wateule, kwa sababu taratibu za chama hicho hutumia vigezo vyake kwa vikao halali kwa ajili ya kuteua wenye sifa na mara nyingi hakuna nafasi ya kupinga uamuzi huo.

Hata hivyo, usiku wa manane zikibaki saa chache kabla ya muda wa uchaguzi, taarifa zilianza kusambaa kuwa jila la Majule litakuwa miongoni mwa watakaopigiwa kura.

Hata yeye anasema hakuamini na mpaka sasa anasema hajui nini kilitokea, bali anasema ni kwa Neema ya Mungu alipigiwa simu na anayesema kiongozi mkubwa akimwambia ameteuliwa na muda mfupi alipokea barua ya uteuzi kupitia mtandao wa simu.

"Ifahamike kwenye mipango na taratibu za chama chetu, kutoteuliwa siyo kitu kigeni, mtu unajua kwamba hata kama una sifa lakini wenzako wanakuwa na sifa kukuzidi japo kidogo, nilijua hivyo tu," anasema.


Machozi hadharani

Julai 30, 2025 uchaguzi ulipofanyika, anasema alitangazwa mshindi katikati ya kuvunjika moyo na kupoteza matumaini.

Si peke yake, wajumbe, wasimamizi na makada walikuwa kwenye mshangao walipoona jina lililorudishwa dakika za lala salama ndiye anaongoza kwa kupata asilimia 95 ya kura zilizopigwa na wajumbe, badala ya kushangilia anasema aliangua kilio hadharani ambacho anasema kilitokana na furaha iliyopitiliza.

Anasema siri ya ushindi wake ni uvumilivu na kujituma, akisisitiza mara nyingi waliovumilia ndiyo waliofanikiwa.


Safari yake kisiasa

Dk Majule anasema alikuwa mwanasiasa wa muda mrefu licha ya kuwa alikuwa kwenye nafasi za chini, lakini alifahamika vizuri ndani ya Chama cha Mapinduzi kutokana na ushiriki na mchango wake wa kukijenga chama.

Hata hivyo, mwaka 2015 anasema aliamua rasmi kujitosa katika kinyang’anyilo cha kugombea Ubunge wa Viti Maalum kwa Mkoa wa Dodoma na kutokana na ushawishi wake, aliamini angekuwa miongoni mwa washindi wawili ambao wangeteuliwa kuwa wabunge.

Anasema bahati haikuwa upande wake kwa sababu hakushinda na haikumkatisha tamaa. Katika simulizi yake anasema hali ilikuwa hivyo pia katika uchaguzi wa 2020.

“Lakini baada ya kuona wanawake wamenielewa, nikaamua kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa UWT katika uchaguzi wa 2017, nilishinda kwa kishindo kikubwa nikaingia tena kuomba nafasi ya ubunge 2020, kwa kweli siwezi kusema mengi lakini matokeo hayakuwa upande wangu pia.

"Lakini siku ya furaha yangu, usiku ule nikiwa nimejiandaa asubuhi nikawachague wenzangu, ghafla ikaingia simu, niliposoma ujumbe, huwezi amini niliondoka nyumbani mimi na kijana wangu mdogo, tuliingia kanisani nikalala madhabahuni hadi alfajili, nilimwambia Mungu, nimekuja kwako naomba uniongoze kwa chochote uwezacho,” anasema na kuongeza.

“Nilikwenda ukumbini nikitokea kanisani, lakini bado nilikuwa siamini, mara kadhaa nilikuwa naangalia simu yangu ili barua niliyotumiwa isijefutika, muda wote nilisema moyoni hii ndiyo CCM ambayo inaweza kuchuja na kufahamu kwa mawanda mapana,” anasema mbunge huyo.


Nini kilifanya ashinde

Anataja siri ya upendo wake kwa wanawake wa Dodoma, unatokana na mabadiriko aliyoyafanya ndani ya Jumuiya kutoka waombaji na sasa kuwa watoaji.

Mbunge huyo, anasema katika kipindi chake tangu alipochukua nafasi ya uongozi aliamua kufanya alichoita siasa na uchumi na akawezesha ununuzi wa gari, viwanja na sasa UWT Mkoa wa Dodoma wanamiliki shule ya watoto ambayo inafanya vizuri.

Anasema ndoto zake ni kuona anaacha alama katika kipindi chake na anachosisitiza ni kuwa, mafanikio yasiwalenge wanawake wa CCM, bali uchumi unapaswa kwenda kwa wote bila kubagua mapenzi ya mtu katika chama furani na wasiowanasiasa ili mradi wanawake wasimame.

"Hata juzi kati mliona nilikuwa na watu wa CRDB Foundation ambapo waliwakopesha wanawake Sh1.39 bilioni watakazorejesha bila riba, lakini dhamana nimeweka mali zangu, nataka mwanamke wa Dodoma aanze kukimbia siyo kutembelea kwenye uchumi.

Anaeleza kuwa, kuingia kwake Bungeni hakuna malengo ya kutafuta fedha, kwani alipofikia panamtosha kupata fedha, isipokuwa amekwenda kupambania Dodoma na kuweka kumbukumbu za nyayo zake ndani ya chombo hicho cha kutunga Sheria.


Kauli za wapinzani kupika viongozi

"Zile kauli zao ni za kisiasa, tanuri la kupika viongozi lipo CCM, huku tunavyo vyuo vya kuandaa viongozi wanaoanzia ngazi ya matawi hadi Taifa, huko kwingine wanajidanganya," anasema Dk Majule.

Kwa mtazamo wake, Watanzania wengi asili yao ni CCM, kama siyo wao basi Wazazi wao watakuwa ni mashabiki ama wanachama wa chama hicho kilichoko madarakani akibainisha kuwa ndiyo maana wengi wao huhama lakini baadae wanarudi tena.


Nje ya ubunge

Neema anasema mbali na ubunge, kwake biashara ndiyo kila kitu, ndiyo maana ameendelea kusimama imara wakati wote bila kuyumba kwa sababu mbali na miradi mingine, amefanikisha ndoto yake ya kumiliki shule.

"Hii Rhema ipo kwa ajili ya kusaidia watoto wa Dodoma na nje ya mkoa huu ili wapate Elimu kwa gharama nafuu, lakini wapo na wasio na uwezo tunawasomesha hasa wa mazingira magumu ili mradi wasikise fursa za kielimu mambo yanayonitofautisha na wengine," anasema.


Mgawanyo wa majukumu

Mbunge huyo anaeleza kitu anachosema kinawafanya Wanawake wengi kukosea ni pale wanaposhindwa kupangilia majukumu yao na hasa kwenye suala la muda.

Kwake anatambua ni mwanamke, mke wa Mtu, ni mama mchungaji, mwanasiasa na mfanyabiashara lakini mambo yote yanakwenda vizuri kwa sababu ya kutenga muda kwa kila eneo analotakiwa kulihudumia na kwa maelekezo yake hakuna kinachoshindikana.