Prime
Mchungaji Msigwa ‘alivyowachambua’ Mbowe, Lissu
Muktasari:
- Mbowe aliongoza Chadema kwa miongo miwili na nafasi yake kuchukuliwa na Lissu aliyeshinda katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amewachambua Freeman Mbowe na Tundu Lissu ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akisema ukuaji na mafanikio ya chama hicho hayawezi kutenganishwa na mchango wa Mbowe.
Mbowe alikiongoza chama hicho kwa miongo miwili na nafasi yake kuchukuliwa na Lissu aliyeshinda uenyekiti dhidi ya Mbowe katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025, jijini Dar es Salaam.
Wawili hao wamekuwa na tofauti tangu mwaka 2024 katika uchaguzi wa Kanda ya Nyasa ambao Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ alishinda nafasi ya uenyekiti dhidi ya Msigwa huku Msigwa akidai zilikuwa ni njama za Mbowe kumwondoa katika nafasi hiyo.
Juni 30, 2024, Mchungaji Msigwa aliamua kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) ambako alitumia majukwaa ya chama hicho kumshambulia Mbowe na Chadema akidai amekuwa akikiendesha chama hicho kihuni.
Jambo hilo lilimsukuma Mbowe kutangaza nia ya kumpeleka Msigwa mahakamani akitaka kulipwa fidia ya Sh5 bilioni kwa madai ya kudhalilishwa. Msigwa naye alitangaza nia ya kwenda mahakamani akidai fidia ya Sh10 bilioni.
Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Mchungaji Msigwa, zikiwa zimepita wiki mbili tangu alipotangaza kurejea Chadema, Mei 23, 2026, baada ya kukaa CCM kwa takribani miaka miwili.
Akizungumza katika mahojiano hayo, Msigwa amesema licha ya tofauti za kisiasa zilizopo baina yao, anaamini Mbowe alifanya kazi kubwa ya kutafuta na kukuza viongozi waliochangia kukijenga chama hicho.
“Mbowe amefanya kazi kubwa, ikiwamo kukuza wanasiasa na kukieneza chama nchini. Ana mchango mkubwa ndani ya Chadema, na mimi mwenyewe ni miongoni mwa watu aliowashawishi kujiunga na chama hiki nikiwa Iringa,” amesema.
Msigwa amesema wakati Mbowe alipomkaribia alikuwa kada wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), walikutana kwa mara ya kwanza katika ofisi ya Mbowe iliyokuwa jengo la Bilicanas, Posta jijini Dar es Salaam ambapo alimshawishi kujiunga na Chadema.
“Mbowe alikuwa na uwezo mkubwa wa kutafuta watu wenye vipaji kutoka maeneo mbalimbali. Hata hivyo, mafanikio hayo hayaondoi ukweli kwamba alikuwa na upungufu wake kama binadamu. Pamoja na hayo, mchango wake katika ukuaji wa Chadema hauwezi kubezwa,” amesema.
Amesema Mbowe ni zao la zama zilizopita, lakini kila kizazi kina nafasi na wakati wake. Kwa mtazamo wake, mazuri kutoka kizazi kilichopita yanapaswa kuendelezwa huku makosa yakiachwa.
“Mbowe ni wa kizazi tofauti kabisa na kizazi cha sasa. Vizazi vingi vimepita kati ya wakati wake na kizazi cha sasa. Binafsi naamini alifanya kazi yake vizuri na ametoa mchango mkubwa ndani ya Chadema. Hilo haliwezi kupuuzwa, japokuwa kila kizazi kina zama zake,” amesema.
Hoja za Lissu hazijajibiwa
Katika mahojiano hayo, Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa amesema tofauti ya Mbowe na Lissu ni kwamba kila nyakati na kizazi chake.
“Sisi kwa jumla ni matokeo ya kizazi kilichopita, lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa kizazi hicho. Kila zama huwa na mahitaji na muktadha wake; yapo mazuri tunayoyarithi kutoka kwa waliotutangulia, na yapo mabaya tunayopaswa kuyaacha,” amesema.
Amesema kizazi cha sasa kinachomzunguka Lissu kinapaswa kujijenga upya na kuendana na wakati, akibainisha Mbowe anatoka katika kizazi cha Baby Boomers, huku vizazi vingine vingi vikifuatia baada yake, ikiwamo Generation X hadi kufika Generation Alpha.
“Nadhani Mbowe amefanya kazi yake vizuri na ametoa mchango mkubwa ndani ya Chadema, jambo ambalo binafsi siwezi kulibeza. Hata hivyo, kila zama huwa na mahitaji na changamoto zake,” amesema.
Kuhusu kumtembelea Lissu gerezani ambako anakabiliwa na kesi ya uhaini, Mchungaji Msigwa amesema bado hajapata nafasi hiyo licha ya kwamba amekuwa akitamani kufanya hivyo.
“Sijafanikiwa kwenda kumuona, lakini naamini anapitia wakati mgumu. Kwa uwezo wake wa kiakili na mchango wake kwa Taifa, nadhani angeweza kusaidia zaidi akiwa huru,” amesema Msigwa.
Amedai hoja nyingi ambazo Lissu ameziibua ikiwamo ya Katiba, Tume Huru ya Uchaguzi na mgawanyo wa madaraka, hazijajibiwa kikamilifu na Serikali.
“Hakuna aliyewahi kutoa majibu ya kina kuhusu madai yake kwamba Katiba iliyopo inampa Rais madaraka makubwa mno. Pia, amekuwa akihoji mfumo wa uchaguzi na uwiano wa nguvu kati ya viongozi waliochaguliwa na walioteuliwa,” amesema.
Kwa mtazamo wake, kumweka Lissu gerezani ni kupoteza mchango ambao angeweza kuutoa kwa Taifa, hususan katika masuala ya sheria na mikataba ya rasilimali.
“Kumweka Lissu gerezani ni kupoteza rasilimali muhimu ya Taifa badala ya kutumia maarifa yake kwa manufaa ya nchi,” amesema.
Tofauti ya CCM, Chadema
Akizungumzia tofauti za kiutendaji kati ya CCM na Chadema, Msigwa amesema CCM ina mfumo wenye nidhamu ya kufuata uamuzi wa pamoja, tofauti na Chadema ambayo huweka mazingira ya kuruhusu vipaji na uwezo wa mtu binafsi kujitokeza.
“Hali ya kuruhusu vipaji vipya kujitokeza inaweza kuonekana kama ukosefu wa nidhamu, lakini ndani yake kuna mfumo wa kuheshimiana na kupeana nafasi. Hata hivyo, wakati mwingine hali hiyo inaweza kupitiliza na kufanya vipaji vingine kushindwa kujitokeza,” amesema.
Amesema CCM ni chama chenye umri mkubwa zaidi ikilinganishwa na Chadema kwani imepitia mchakato mrefu wa kujijenga na kukua katika mifumo yake ya kiutawala tangu wakati wa mfumo wa chama kimoja.
Kuhusu kurejea kwake Chadema, Msigwa amesema chama hicho kimefikia hatua ambayo hakimtegemei mtu mmoja. Hata mtu yeyote akiondoka, chama hakiwezi kuyumba kwa kuwa tayari kimejijengea imani kwa wananchi.
“Kurudi kwangu Chadema hakumaanishi kwamba nina majibu yote sahihi au nina uwezo mkubwa kuliko waliopo. Ninachofanya ni kuungana na wenzangu mahali nilikokulia kisiasa, katika mazingira ambayo watu walipitia changamoto nyingi lakini waliendelea kusimama imara kulinda imani yao,” amesema.
Amesema Chadema imepitia kipindi kigumu, ikiwamo kufungiwa shughuli zake, lakini viongozi na wanachama mbalimbali waliendelea kusimama kidete. Miongoni mwao ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, John Heche, Katibu Mkuu, John Mnyika na wajumbe wa kamati kuu.
Kuhusu ubunge 2030
Alipoulizwa kama ana mpango wa kuwania ubunge wa Iringa Mjini mwaka 2030, Mchungaji Msigwa amesema kwa sasa kipaumbele chake ni kuijenga Chadema kwa kushirikiana na wenzake na kutumia nafasi aliyonayo kuhamasisha mabadiliko.
“Tunapaswa kuimarisha chama, kuhakikisha Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na mabaraza mengine yanakuwa imara. Mambo mengine ya baadaye yatategemea matakwa ya wananchi,” amesema.
Amesema kugombea ubunge si kipaumbele chake kwa sasa, bali anataka kuongozwa na misingi ya utu, ukweli na mapenzi kwa Taifa.
“Mapenzi kwa Taifa langu yanapaswa kuwa juu ya cheo. Thamani yangu haitegemei kuwa na cheo au kutokuwa nacho. Sikufahamika katika siasa za Tanzania kwa sababu ya uteuzi, bali kwa sababu nilikuwa na jambo la kuwaambia wananchi wa Iringa, wakaniamini na kunichagua kuwa mbunge mara mbili,” amesema.
Msigwa amesema nafasi za uongozi si jambo analolipa uzito mkubwa, akibainisha kuwa tangu mwaka 2020 hajawahi kushika nafasi yoyote ya uongozi. Amesema wanaodhani anarudi Chadema kwa ajili ya cheo huenda hawafahamu historia yake kisiasa.
Wajibu wa Serikali
Katika maelezo yake, Mchungaji Msigwa amesema wajibu wa Serikali na chama tawala ni kulinda usalama wa Taifa.
Ameonya kutoheshimu mifumo na taasisi za nchi kunaweza kuwa tishio kwa usalama wa Taifa.
“Chama tawala kinaposhindwa kushinda uchaguzi bila kutegemea dola, badala ya kulinda usalama wa Taifa kinakuwa tishio kwa usalama huo. Taasisi kama Jeshi la Polisi, Mahakama, vyombo vya habari na Bunge zikichezewa, msingi wa Taifa unayumba,” amesema.
Mchungaji Msigwa ametoa wito kwa Watanzania kurejea katika misingi ya utawala bora kwamba, kila taasisi itekeleze wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
“Vyombo vya ulinzi vifanye kazi ya ulinzi, wanasheria walinde sheria, wanahabari wahabarishe umma. Dola haipaswi kuziba midomo ya watu au kuogopa kukosolewa. Mbinu hizo hazijawahi kuleta matokeo chanya,” amesema.
Amesema hata waliowahi kushindwa katika nyakati tofauti hawakuwa wajinga, bali mara nyingi mifumo ya nchi ilishindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Wito wangu ni kurejea kwenye misingi. Tuelewe majukumu ya Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Polisi, Bunge na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Tukifanya hivyo, tutaendelea kuishi kwa amani na utulivu,” amesema.