Prime
Miaka 12 ya ACT, ikipitia nyakati ngumu na mafanikio
Dar es Salaam. Chama cha ACT–Wazalendo kimetimiza miaka 12 tangu kuanzishwa kwake Mei 5, 2014, safari iliyojaa mafanikio, changamoto na mabadiliko ya kisiasa na kiuongozi.
Ndani ya kipindi hicho, chama hicho kimejijenga kutoka harakati za vijana wachache hadi kuwa miongoni mwa vyama vinavyotajwa katika ushindani wa kisiasa nchini Tanzania.
Kilipoanzishwa, ACT–Wazalendo kilibeba dhima ya kuleta siasa mbadala zenye misingi ya uwajibikaji, usawa na uzalendo.
Waasisi wake, akiwamo Zitto Kabwe, Kitila Mkumbo na marehemu Anna Mghwira, walilenga kujenga chama cha kisasa kinachotegemea taasisi badala ya mtu mmoja.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chama hicho kilishiriki kwa mara ya kwanza Uchaguzi Mkuu wa Tanzania na kufanikiwa kupata kiti kimoja cha ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini, pamoja na kuongoza Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Hii ilikuwa hatua ya awali iliyoonesha uwezo wake wa kuanza kupata mizizi katika siasa za ushindani.
Ukuaji wake uliendelea kuonekana mwaka 2020, ambapo kilipata wabunge wanne kutoka Zanzibar, hususan Pemba na madiwani kadhaa Tanzania Bara.
Hata hivyo, chama kilipinga matokeo ya uchaguzi huo kikidai kuwepo kwa kasoro katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Hata hivyo, ilishuhudiwa na Watanzania mafanikio makubwa zaidi yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, chama hicho cha ACT–Wazalendo kiliongeza uwakilishi wake kwa kupata wabunge wanane, wawakilishi 10 na wabunge wa viti maalumu wanne katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Hatua hii imeonekana kama ishara ya kuimarika kwa ushawishi wake kisiasa na kukua kwa mtaji wa imani kutoka kwa wananchi kwa chama hicho.
Licha ya mafanikio hayo, safari ya chama hicho haijakosa misukosuko. Tangu mwaka 2015, kimepitia changamoto mbalimbali, ikiwemo kuondokewa na baadhi ya waasisi wake na kukumbana na migogoro ya ndani.
Pia, mabadiliko ya kisiasa nchini yamekuwa yakikiathiri kwa namna moja au nyingine.
Makamu Mwenyekiti wa chama Zanzibar, Ismail Jussa akizungumza na Mwananchi kuhusiana na maadhimisho hayo, amesema safari ya ACT–Wazalendo imekuwa ya “milima na mabonde,” lakini imefanikiwa kusimama imara.
Jussa amesema mwanzoni, chama hicho hakikuwa na uzito mkubwa katika ramani ya siasa Bara na Visiwani, lakini kwa sasa kinatajwa miongoni mwa vyama vikuu nchini.
Kwa mujibu wa Jussa, chama hicho kimefanikiwa kujenga ngome katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kigoma, Pwani, Ruvuma na Zanzibar.
Jussa anasema kwa hatua hiyo muhimu katika ukuaji wake ilitokea mwaka 2019 baada ya mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad, pamoja na wafuasi wake walihamia Chama cha ACT–Wazalendo.
Uamuzi huo uliambatana na kampeni maarufu ya “Shusha Tanga, Pandisha Tanga,” iliyosaidia kuongeza wanachama wengi kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Jussa, hatua hiyo iliashiria kuzaliwa upya kwa chama cha ACT – Wazalendo na kukipa nguvu mpya ya kisiasa.
“Tulipojiunga, tulikuta chama kina mbunge mmoja, lakini leo kina wabunge wanane, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 14 na madiwani kadhaa,” anasema Jussa, akisisitiza kuwa licha ya changamoto za uchaguzi, chama kimeendelea kukua.
Anabainisha kuwa moja ya sifa inayokitofautisha ACT–Wazalendo ni mfumo wake wa uongozi unaozingatia katiba, ikiwamo kuweka ukomo wa madaraka na kufanya mabadiliko ya uongozi kwa utaratibu.
Hali hiyo, anasema imekisaidia chama hicho kubaki imara na kuepuka migogoro mikubwa ya ndani.
Aidha, Jussa anasema chama hicho kimekuwa sehemu ya mijadala mikubwa ya kitaifa kupitia baraza lake kivuli la mawaziri, ambalo limekuwa likitoa hoja mbadala kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maisha ya wananchi.
Hata hivyo, changamoto hazijakosekana. Hata hivyo anasema kifo cha Maalim Seif mwaka 2021 kilikuwa pigo kubwa, hasa kwa upande wa Zanzibar ambako alikuwa na ushawishi mkubwa kisiasa.
“Watu wengi walihofia kuwa chama kingetikisika, lakini kimeendelea kusimama na kubakia imara mpaka sasa na kinazidi kuvuna wanachama kila kukicha,” anasema Jussa.
Changamoto nyingine ni kuondoka kwa baadhi ya viongozi wake waliokuwa na ushawishi mkubwa kuelekea vyama vingine, pamoja na madai ya kasoro katika michakato ya uchaguzi kuanzia mwaka 2019 hadi 2025.
Jussa anadai hali hiyo imekuwa ikidhoofisha matarajio ya chama kupata uwakilishi mkubwa zaidi licha ya uwekezaji mkubwa wa rasilimali katika kampeni.
Katika kuadhimisha miaka 12, ACT–Wazalendo kimepanga kufanya shughuli zake mkoani Lindi, zikiwamo za mkutano mkuu wa jimbo na mkutano wa hadhara kama sehemu ya kuendelea kujijenga na kuimarisha uhusiano na wananchi.
Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa mustakabali wa chama hicho unategemea namna kitakavyoweza kuendeleza misingi yake ya siasa za kistaarabu na kujenga imani ya wananchi.
Mchambuzi wa siasa, Kiama Mwaimu anasema dalili zinaonesha kuwa chama kinaendelea kuimarika, hasa kutokana na ongezeko la uwakilishi wake bungeni.
Anasisitiza kuwa ili kuendelea kukua, ACT–Wazalendo kinapaswa kudumisha mshikamano wa ndani na kuendeleza siasa za ustaarabu ambazo zimekuwa alama yake.
Kwa upande wake, mchambuzi Rainery Songea anashauri chama hicho kiendelee kusimamia misimamo yake bila kuyumba, akieleza kuwa uthabiti wa kisiasa ndio msingi wa kujenga imani kwa wananchi.
Kwa ujumla, miaka 12 ya ACT–Wazalendo inaonesha safari ya chama kinachokua hatua kwa hatua, kikikabiliana na changamoto huku kikijenga msingi wa ushindani wa kisiasa.
Hatua inayofuata itategemea uwezo wake wa kuimarisha taasisi zake, kudumisha misingi yake na kuendelea kuwavutia Watanzania wanaotafuta mbadala wa kisiasa.