Miaka 66 ya uhuru DRC ndoto ya Lumumba bado haijatimia
Ilikuwa Alhamisi, Juni 30, 1960, wakati viongozi wa Ubelgiji na Congo walipokusanyika katika Ikulu ya Taifa (Palais de la Nation) jijini Kinshasa, iliyokuwa ikijulikana wakati huo kama Leopoldville, kushuhudia sherehe za kumalizika kwa zaidi ya miongo saba ya utawala wa kikoloni.
Katika hafla hiyo, Mfalme Baudouin I wa Ubelgiji alitangaza rasmi uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku maelfu ya wananchi wakifurika mitaani kusherehekea uhuru waliokuwa wakiusubiri kwa muda mrefu, ingawa ulitolewa kwa kusitasita na utawala wa kikoloni wa Ubelgiji.
Mtafiti wa historia ya DRC katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Akramm Tumsifu amenukuliwa na Al Jazeera akisema uhuru huo haukuwa sehemu ya mpango wa haraka wa Ubelgiji.
“Kwa kiasi kikubwa, Wabelgiji walitarajia DRC ipate uhuru katika miaka ya 1980. Walitaka kuendelea kunufaika na rasilimali za taifa hili,” anasema.
Kwa mujibu wa Tumsifu, hotuba ya Mfalme Baudouin I ilionyesha mtazamo wa kibaba uliolenga kuhalalisha nafasi ya Ubelgiji nchini Congo hata baada ya ukoloni.
Katika hotuba yake, mfalme huyo alisema kwa miaka 80 Ubelgiji ilikuwa imetuma watu wake bora nchini Congo ili kukomesha biashara ya utumwa na kuunganisha makabila yaliyokuwa mahasimu, yakielekea kuunda taifa kubwa zaidi huru barani Afrika.
Hata hivyo, mwanahistoria wa Congo anayeishi Goma, Dany Kayeye anasema hotuba hiyo iliakisi dharau dhidi ya wananchi wa Congo walioteseka chini ya utawala wa kikoloni.
Anasema rais wa kwanza wa DRC huru, Joseph Kasavubu, alichagua kutoa hotuba ya kidiplomasia na yenye msimamo wa wastani kwa sababu alitegemea uungwaji mkono wa Wabelgiji kuiongoza nchi hiyo. “Lakini wakati sauti za Wakongo ziliponyamazishwa na matumaini yao kupuuzwa, ilihitajika kiongozi mwenye ujasiri wa kusimama mbele ya Wazungu waliokuwa wakionekana kama miungu,” alisema Kayeye.
Lumumba avunja utaratibu
Waziri Mkuu wa kwanza wa DRC, Patrice Emery Lumumba, alikuwa mmoja wa vinara wa harakati za kudai uhuru na mwanzilishi wa chama cha Movement National Congolais (MNC).
Alijitokeza kama mmoja wa wakosoaji wakubwa wa utawala wa kikoloni wa Ubelgiji, akisisitiza uhuru kamili na kukomeshwa kwa unyonyaji wa kikoloni pamoja na ubaguzi wa rangi.
Kwa mujibu wa Kayeye, Lumumba hakuwa amepangwa kutoa hotuba katika sherehe hizo.
“Huenda kutokana na misimamo yake mikali na ukosoaji wake wa wazi, hakupangiwa kuhutubia. Lakini kinyume cha matarajio ya wengi, alisimama na kutoa hotuba ambayo imeendelea kukumbukwa hadi leo,” anasema.
Katika hotuba hiyo, Lumumba alikumbusha mateso yaliyowapata Wakongo chini ya ukoloni, yakiwamo vipigo, ubaguzi wa rangi na ukandamizaji, akisisitiza kuwa uhuru haukutolewa kama zawadi bali ulipatikana kupitia mapambano. “Tulivumilia dhuluma na vipigo mchana na usiku kwa sababu tu tulikuwa weusi,” alisema.
Aliongeza kuwa Wakongo waliteseka, walitengwa kwa sababu ya mitazamo yao ya kisiasa na dini, huku wengine wakijikuta kama wageni ndani ya nchi yao wenyewe.
Kauli hizo ziliwakasirisha viongozi wa Ubelgiji na kuashiria mwanzo wa uhusiano wenye misuguano kati ya mataifa hayo baada ya uhuru, anasema Tumsifu.
Ahadi ya uhuru haijatimia
Miaka 66 tangu DRC ijipatie uhuru, wananchi wengi wanaamini ndoto ya taifa huru na lenye ustawi bado haijafikiwa.
Mwanaharakati wa haki za watoto kutoka Bunia, David Kalume (26), anasema maadhimisho ya uhuru yanapaswa kuwa muda wa kutafakari hali halisi ya nchi.
“Uhuru unapaswa kumaanisha taifa lililoendelea, linalojitegemea na linalojiendesha kwa uwezo wake. Hilo bado halijafikiwa DRC. Vita vinaendelea mashariki mwa nchi na hata sehemu ya ardhi yetu hatuwezi kuidhibiti,” anasema.
Kwa mujibu wake, kama DRC ingekuwa huru kwa maana halisi, isingekuwa bado inakabiliwa na migogoro ya silaha, umaskini, ukosefu wa usalama wa kijamii na kiuchumi pamoja na ubaguzi.
“Mahali penye uhuru kuna maendeleo na usalama. Lakini jamii zimegawanyika, nasi tunaoishi mashariki mwa nchi tunahisi tumeachwa na Serikali ya Kinshasa,” anasema.
Katika hotuba yake ya mwaka 1960, Lumumba alihitimisha kwa ujumbe wa matumaini akisema:
“Tutaonyesha dunia kile ambacho Waafrika wanaweza kukifanya wanapofanya kazi katika mazingira ya uhuru.”
Kalume anaamini maono hayo bado hayajageuka kuwa uhalisia.
“Tuna viongozi wanaotanguliza masilahi yao binafsi kuliko wananchi. Bado hatujafikia kiwango cha kutimiza ndoto ambazo Lumumba alikuwa nazo kwa taifa hili.”
Wategemezi wa misaada
Mkazi wa Bunia na baba wa watoto saba, Noé Kabiona, aliyezaliwa mwaka 1963, naye anaona maana ya uhuru bado haijaonekana. “Kwa kila namna bado hatujawa huru. Hata katika elimu, wasomi wetu wanafanikiwa zaidi nje ya nchi kwa sababu hapa hawapati fursa. Inasikitisha kuona wanaamini wana maisha bora ugenini kuliko nyumbani,” anasema.
Maoni yake yanakuja wakati mashariki mwa DRC ikiendelea kukumbwa na migogoro ya muda mrefu iliyosababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na kutegemea misaada ya kibinadamu.
Kabiona anaamini taifa hilo bado lina nafasi ya kurejea kwenye mstari sahihi. “Nchi hii inatupa maumivu kutokana na matatizo mengi, kuanzia migogoro ya kibinadamu hadi mivutano ya kisiasa inayochochea ukosefu wa usalama. Tukitambua thamani yetu, bado tunaweza kubadili hali hii.”
Anasema utegemezi mkubwa wa misaada ya kimataifa unaibua maswali kuhusu maana halisi ya uhuru.
“Siku zote tunaomba misaada kutoka nje. Hatujawahi kusikia DRC ikifadhili mradi nchini Marekani. Mara zote tunasikia Marekani, Canada na mataifa mengine yakitusaidia kifedha. Tuna kila kitu, lakini bado tunaendelea kuomba msaada,” anasema.
Changamoto za uongozi
Mwanaharakati wa demokrasia na utawala bora kutoka vuguvugu la Filimbi, Muyisa Christophe, anaamini changamoto nyingi zilizoikumba DRC baada ya uhuru zilitokana na ukosefu wa viongozi wenye maandalizi ya kutosha.
“Mwaka 1960, Congo haikuwa na wasomi wa kutosha wala wanasiasa waliokuwa wameandaliwa kuongoza nchi,” anasema.
Anasema hali hiyo ilichangiwa na sera za kikoloni zilizowazuia Wacongo wengi kupata elimu ya juu, jambo lililoiacha nchi ikiwa na uhaba wa watendaji na viongozi wenye taaluma wakati wa uhuru.
“Kwangu, miaka hii 66 imekuwa kipindi cha mpito kilichojaa ukosefu wa maandalizi, uamuzi wa dharura, ukosefu wa usalama, matatizo ya uchumi, maasi na harakati za kujitenga. Tunapaswa kutathmini tulikotoka, kujifunza kutokana na makosa yetu na kupanga vipaumbele kabla ya kusonga mbele,” anasema.