Mkutano mkuu CUF kuamua Siwale au Gombo urais Tanzania
Muktasari:
- Profesa Lipumba amewataja wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Mkunyutila Siwale na Samandito Gombo.
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimewateua makada wawili wa chama hicho watakaopigiwa kura kwenye mkutano mkuu ili kumpata mpeperusha bendera wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza majina ya watiania waliojitokeza katika chama hicho, leo Ijumaa, Agosti 8, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi kuu ya chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba amewataja wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Mkunyutila Siwale na Samandito Gombo.
Kwa upande wa Zanzibar, amesema kamati ya uongozi ya chama hicho imewapitisha Habib Mohammed, Masoud Hamad na Mohamed Khatib kugombea urais wa Zanzibar mbele ya mkutano mkuu.
Mtiania wa urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Masoud Hamad Msaoud akiwasili makao makuu ya chama hicho, yaliopo Buguruni Jijini Dar es Salaam.
Amesema wagombea wawili wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watatu wa urais wa Zanzibar, watapigiwa kura katika mkutano mkuu utakaoketi kesho Agosti 9, 2025 jijini Dar es Salaam ili kupata mgombea urais wa chama hicho kwa pande zote mbili za Muungano.
Mkutano mkuu utakaofanyika kesho Agosti 9, 2025, unatarajiwa pia kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho na kupitisha majina ya watiania wa nafasi ya ubunge.
Akizungumia uamuzi wake wa kutogombea urais kwenye uchaguzi ujao, Profesa Lipumba ambaye amegombea urais mara tano tangu kuanzishwa kwa chama hicho, amesema wagombea waliojitokeza wana sifa na atakayeteuliwa na mkutano mkuu atakuwa mtu sahihi.
“Nawaomba wafuasi wangu wajue tunawaletea mgombea bora zaidi, na mimi nitazunguka kumnadi, kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki, wajiandae kushangilia ushindi wa CUF,” amesema Profesa Lipumba.
Mtiania wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya CUF, Rose Kahoji akishuka kwenye gari baada ya kuwasili makao makuu ya chama hicho, yaliopo Buguruni Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia majina hayo yaliyopitishwa na kamati ya uongozi, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wagombea wa mwaka huu ni watu wenye ushawishi na uwezo mkubwa.
“Tuna imani kubwa sana mwaka huu kwani wagombea wetu ni wenye uwezo mkubwa sana, Watanzania wasubiri ushindi,” amesema.
Uteuzi huo unaandika historia ya uchaguzi wa kwanza kwa historia ya CUF kusimamisha mgombea wa urais tofauti na Profesa Lipumba.
Kinachosubiriwa sasa ni wajumbe wa mkutano mkuu kuamua ni Siwale au Gombo ili kuwapeleka kwa Watanzania waamue kupitia sanduku la kura Oktoba 29, 2025.