NIKWAMBIE MAMA: Mama, mambo halali kwao haramu kwetu

Leo naogopa hata kunong’ona mama yangu, usije kuniona nimegeuka kuwa mhuni. Lakini, potelea mbali hata kama taulo litanidondoka wakati nikimrukia mtoto asiingie kwenye chungu cha moto, alimradi nitakuwa nimefanikiwa kuokoa maisha yake.

Neno langu la leo lisipoeleweka vizuri litakuwa kama utetezi wa mambo yasiyofaa kwenye jamii, lakini nitajaribu kunyoosha mistari kabla hujaamua kunifukuza.

Tumekuwa tukiushangilia uhuru wetu kwa miaka zaidi ya 60 sasa.

Tunafanya kazi na kusherehekea mafanikio yetu wenyewe, tunazitukuza rasilimali zetu tulizozawadiwa na Mwenyezi Mungu na kujivunia jinsi tunavyoweza kuzigeuza kuwa chanzo cha mapato ya Taifa letu.

Lakini, inasikitisha kuona miongoni mwetu bado tunao wenzetu waliolewa sumu ya ukoloni, ambao wanatuficha yale ya uvunguni mwetu kwa nia ya kufaidi peke yao.

Hakuna asiyejua kwamba ili nchi tajiri ziendelee kung’ara, uwepo wa nchi masikini ni wa lazima.

Pamoja na kuwa matajiri wapo juu sana kwenye maendeleo kwa kuongoza ulimwengu wa teknolojia tangu mapinduzi ya viwanda, lakini hawana jinsi ya kwenda bila sisi kutokana na ukweli kwamba Afrika ndiye mama wa mafanikio yao.

Afrika ni malighafi, lakini pia ni soko la bidhaa zao. Pia, utajiri hauwezi kuonekana pasipokuwa na umasikini.

Kama nilivyopata kusema nyakati zilizopita, wewe ukiwa kiongozi wa juu wa mikoa 31 yenye Watanzania zaidi ya milioni 68, huwezi kufahamu kila kitu bila kufahamishwa na wawakilishi wako walio kila kona ya nchi.

Timu yako ya viongozi ina jukumu la kukuletea taarifa kutoka ngazi ya chini kabisa kwa ajili ya upembuzi na uamuzi.

Haishangazi, maana hapa uswazi tunaweza kushindwa kujua msiba wa jirani kwa sababu hatupo kwenye “grupu” lao la “wasapu”.

Sasa kwa vile hapa ndipo malighafi ya dawa inapopatikana, wale wananchi pamoja na viongozi wenye mtindio wa kikoloni wameamua kuchepuka kwenye njia za panya na wanaupiga mwingi kimyakimya.

Wameamua kufanya dili na mataifa makubwa kutumia ardhi yetu na kuzalisha mazao ambayo ni marufuku kwa watu wengine kuyalima.

Moja wa mazao haya ni bangi inayolimwa kwenye mashamba makubwa sehemu tofauti hapa nchini.

Kilimo cha bangi kimekuwa fursa ya chini chini kwa wahusika hao ambapo inalimwa na kuvunwa hapa nchini.

 Fungu la kwanza lenye ubora linasafirishwa kwenda nje ya nchi kama malighafi kwenye viwanda vya dawa za binadamu.

Lakini fungu jingine lisilo na ubora husambazwa mitaani kwa Watanzania.

Lengo la kufanya hivyo ni kupata faida, lakini mbaya zaidi ni kuwaingiza Watanzania kwenye uraibu.

Mchezo mchafu wa aina hii ulikuwa ukifanywa na mataifa haya makubwa kwenye nchi kadhaa masikini hapa duniani.

Mimea ya Opium na Kokeini ililimwa kwenye mashamba makubwa kule Amerika ya Kusini.

Mazao yake ya daraja za juu yalipelekwa ughaibuni kama malighafi ya dawa.

Mazao yake ya daraja za juu yalipelekwa ughaibuni kama malighafi ya dawa.

Lakini, daraja za chini pamoja na mabaki yake zilimwagwa uraiani kama njugu.

Wakatumia wafanyakazi wa mashambani mpaka wanafunzi wa shule za msingi.

Kilio kikubwa kilizikuta Colombia, Peru, Mexico, Panama na majirani zao kufuatia majanga waliyoachiwa na biashara hiyo.

Asilimia kubwa ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa lolote ilikumbwa na uraibu wa dawa za kulevya.

Na kwa sababu uraibu unatafuna afya ya akili, vijana hao wakakosa akili ya kuzalisha mali. Badala yake uhalifu na mauaji vikawa ndio maisha ya wananchi wa maneo hayo.

Hapa nchini hatari ya kilimo cha bangi imeshakuwa wazi. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata mamia ya kilo za bangi iliyosindikwa (wenyewe wanaita skanka).

Skanka ni mseto wa bangi na kiwango fulani cha kemikali, kisha hutiwa kwenye biskuti, keki na kadhalika kuzuia kutambulika kirahisi.

Imeelezwa mchanganyiko huo (skanka) hubeba asilimia 45 ya sumu ukilinganisha na asilimia 3 kabla haijachanganywa.

Kwa mtindo huu, wanafunzi na watoto huwa kwenye hatari kubwa zaidi.

Wao hupenda lawalawa na sharubati mpya ili kuonja ladha tofauti.

Ina maana baada ya muda mfupi tutakuwa na Taifa lisilo na afya ya akili, litakaloshindwa kufikiria kufanya kazi halali tofauti na uhalifu.

Mraibu wa dawa hizi anaweza kupora simu yenye thamani ya Sh1 milioni, akaenda kubadilishana na kete ya dawa za kulevya ya Sh2,000.

Sasa ndio nakupa mawazo yangu niliyokuwa naogopa hata kuyanong’ona.

Kabla ya wachimba madini wadogo kutambuliwa rasmi, shughuli zao zilikuwa haramu. Hii iliwavutia wahuni hata ikagharimu maisha ya watu wengi sana.

Ishu za kizani hazina staha, hivyo dhuluma na mauaji ilikuwa siyo habari.

Lakini baada ya kurasimishwa, wachimbaji hao wamekuwa wakichangia pato kubwa la Taifa na sasa wanaonekana watu wa maana sana mbele za jamii na Serikali.

Tafadhali mama usinihisi vibaya, naomba turasimishe kilimo cha mmea ule ili kiongeze tija na ajira kwa vijana.

Shughuli hiyo ikiwa halali, itaondolewa kwenye mikono michafu na kuwa chini ya usimamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Hivyo, pamoja na kuzaa faida, makinikia yake hayatasambaa mtaani na kuwazevenza wanetu.

Hali itakuwa sawa na mageuzi yaliyofanyika kwa wachimbaji wadogo, maana nao walikuwa wakichinjana kwa ajili ya makinikia ya dhahabu.