Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Mzigo mwingine kwa wasafiri Mbagala



Hapa nchini bado kuna umbali mrefu kati ya walala hai na walala hoi. Yaani Mkurugenzi anayefuatwa nyumbani na VX la kazini, na yule anayegombea daladala ili akapambanie maisha ya familia yake.

Mbaya zaidi, hawa masikini wanaishi bila ya uhakika wa maamuzi ya wakubwa wao. Wale wenye hali nzuri ndio wanaofanya maamuzi ya wote bila hata kuwashirikisha.

Maamuzi mengine yanafanana na hadithi ya watoto waliokuwa wakifurahia mchezo wa kurusha mawe bwawani. Wao hawakujali kuwa bwawani humo ni makazi ya vyura na viumbe wengine.

kwa mujibu wa hadithi hiyo, chura mzee aliibuka na kuwaonya kwamba “mchezo wenu ni mauti yetu”. Lakini badala ya kusitisha au kupunguza mirusho, watoto hao waliongeza kasi huku wakisherehekea.

Haujapita muda tangu nikunong’oneze yaliyotokea Buza. Wananchi wa maeneo hayo waliamka kama kawaida, wakaenda kwenye kituo cha basi ili kila mmoja akalijenge Taifa kwa namna yake. Lakini pale kituoni walipigwa na taharuki baada ya kukuta askari wametanda badala ya madaladala.

Walifukuzwa na kupewa maelezo kuwa kuanzia siku hiyo kituo chao kimehamishiwa katika kituo kipya cha Mama Kibonge.

Kwa umbali uliopo kati ya Buza Kanisani hadi Kwa Mama Kibonge, iliwapasa kulipia bajaji au boda mpaka hapo ili kupata daladala za kuwafikisha katikati ya mji. Na kwa hali ya maisha ilivyokuwa ngumu, wengi wao walirudi majumbani kujipanga upya.

Wafanyakazi walishindwa kwenda makazini, watoto wakakosa kwenda shuleni kama vile wagonjwa walivyoshindwa kuwahi hospitali.

Wapo waliomudu kulipa nauli mbili kwa safari moja, lakini pia wapo walioshindwa kabisa. Waliamua kupaza sauti hadi wakubwa zaidi walipoliingilia kati sakata hilo. Haki ikaonekana kusiginwa kwa wanyonge, na hatimaye wakarudishiwa baadhi ya haki zao kimyakimya.

Ndiyo maana nasema kuna umbali mrefu kati ya mla ndizi na mtupa maganda. Baadhi ya watu wanaamua pasi na kujali athari za maamuzi yao kwa umma.

Hivi karibuni tukaona yanayoendelea mpaka hivi sasa kule Mbagala. Vichwa vya habari vilikuwa na mkanganyiko kwa walio nje kudhani ni neema inayobashiriwa, wakati walio ndani wakikiona cha moto.

Ni pale Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilipozitaka daladala zinazotoa huduma barabara ya Kilwa kusitisha huduma ifikapo Julai Mosi, 2026 ili kupisha mradi wa mabasi yaendayo kasi (BRT).

Mamlaka zilisema kuwa kuanzia tarehe 1 Julai mwaka huu, huduma za daladala katika njia ya Mbagala – Kariakoo – Posta – Kivukoni zingeondolewa rasmi katika njia hizo, na zingepangiwa njia mbadala za kufanya kazi. Imeelezwa kuwa hatua hii inalenga kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri, na kuongeza ufanisi wa huduma na kuboresha usafiri wa umma jijini Dar es Salaam.

Kwa maneno yao, viongozi wa LATRA wanasema daladala zinasababisha mwingiliano wa huduma na kuathiri ufanisi wa huduma hizo, ambazo Serikali imewekeza kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa umma kwa wananchi.

Lakini wananchi wanatishwa na ukweli kwamba abiria wanaotoka vitongoji vya pembezoni, kushuka katika Kituo cha Mbagala Rangi Tatu, na kuunganisha safari zao kwa kutumia mabasi ya mwendokasi.

Kwa mtu anayeishi Mikocheni, hatua hii inaonekana kama itakayokidhi mahitaji makubwa ya wasafiri wa Mbagala, lakini kwa wakazi wa maeneo hayo wamezua malalamiko makubwa zaidi ya usafiri.

Changamoto kuu zinazowakabili wananchi ni pamoja na mfumuko wa nauli. Baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa mabasi ya mwendokasi yanawatoza nauli kubwa kulinganishwa na daladala.

Lakini pia Mbagala ni kubwa sana. Kuna vitongoji vingi vilivyo kando ya Rangi Tatu, hivyo wakazi wake watalazimika kulipia bajaji na bodaboda kabla ya kuifikia mwendokasi.

Jambo hili linategemewa kumtwisha mzigo mzito mkazi mwenye kipato cha chini, hasa ukizingatia kuwa analazimika pia kuwasafirisha watoto kwenda shuleni. Wadau wa usafiri wanalalamika kuwa uamuzi huo wa Latra haukuzingatia maoni yao, na unaweza kuchochea upandaji holela wa nauli.

Wanasema kuwa laiti mamlaka ingewasikiliza, wangeondokana na changamoto kama zinazowakumba abiria wenzao wanaosota kutwa nzima vituoni kusubiri mabasi ya mwendokasi. Aidha, mageuzi yoyote ya mfumo wa usafiri yanapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya kutosha, elimu kwa umma na ushirikishwaji wa wadau wote.

Wananchi wanapopewa nafasi ya kueleza changamoto zao kabla ya maamuzi kutekelezwa, huwa rahisi kupata suluhisho linalonufaisha kila upande. Serikali inaweza kufanikisha malengo ya kuboresha usafiri bila kuongeza mzigo kwa wananchi kwa kuhakikisha kuna njia mbadala zinazofanya kazi, nauli zinabaki ndani ya uwezo wa wengi na idadi ya mabasi inakidhi mahitaji halisi.

Vinginevyo, nia njema ya kuboresha huduma inaweza kutafsiriwa kama adhabu kwa watu wanaotegemea usafiri wa umma kila siku kutafuta riziki zao. Mwisho wa yote, maendeleo ya kweli hupimwa kwa namna yanavyorahisisha maisha ya mwananchi wa kawaida, si kwa ukubwa wa miradi pekee. Hivyo, busara, usikivu na tathmini endelevu ni msingi muhimu wa mafanikio ya mabadiliko hayo.