Nondo autaka tena uenyekiti ngome ya vijana ACT-Wazalendo

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo

Muktasari:

 Uchaguzi wa ngome ya vijana wa ACT-Wazalendo umepangwa kufanyika Februari 29, 2024.

Dar es Salaam. Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, Abdul Nondo ametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Nondo amebainisha hilo kupitia taarifa aliyoitoa leo Februari 5, 2024, huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Februari 29, 2024.

“Mimi mwenyekiti wenu rasmi natangaza nia ya kugombea tena awamu ya pili ili kumalizia tulipoishia,” amesema Nondo.

Hata hivyo, amehimiza vijana ndani ya chama hicho kujitokeza kugombea nafasi zilizopo, hususani uenyekiti wa Ngome na Makamu Mwenyekiti Taifa ili wajumbe wawe na machaguo mengi zaidi.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Nondo amesema anaazimia kuendelea kusemea changamoto za vijana nchini.

Nondo aliyedumu kwenye kiti hicho kwa miaka minne amesema katika awamu ya pili wataimarisha ngome ya vijana na chama ngazi za chini sababu tatizo la rasilimali fedha tayari wamelipatia ufumbuzi.

“Tutashuka chini kufanya ziara na kuhimiza vijana kugombea chaguzi za Serikali ya mitaa na uchaguzi mkuu ili kuwapigania vijana kupitishwa kwa wingi katika kura za maoni ndani ya chama kuanzia serikali ya mitaa hadi udiwani na ubunge ili malengo yetu ya kuongeza ushiriki wa vijana katika vyombo vya maamuzi yafikiwe,’’ amesema.

ACT-Wazalendo pia watafanya uchaguzi wa ngome ya wazee Machi 1, 2024, vilevile uchaguzi wa ngome ya wanawake Machi 2, 2024.

Uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho, wakiwamo mwenyekiti na makamu wake utafanyika Machi 5, 2024.

Chama hicho kimepanga kufanya mkutano wa hadhara kutangaza viongozi wapya waliochaguliwa Machi 6, 2024.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi, mchambuzi wa siasa, Ali Makame amesema chaguzi ni jambo la kawaida katika vyama vya siasa, hivyo kinachopaswa kufanyika ni kufuata katiba na kanuni walizojiwekea.

Amesema chaguzi zikiwa huru na za haki kutakua na uongozi imara, hivyo kukiwa na uongozi imara kutakua na chama imara.

“Kinyume cha misingi hiyo, hakutakuwa na maendeleo yatakayopatikana,” amesema.