Safari ya Abdul Nondo kutoka ‘kutekwa’ hadi kushinda kesi

Muktasari:
Jumatatu Novemba 5, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemwachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya kushindwa kumtia hatiani
Juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa ilimuachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka mawili yaliyosababisha afikishwe mahakamani hapo.
Hadi anafutiwa mashtaka Nondo alikuwa ametimiza siku 224 tangu aliposimamishwa masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Machi 26 kutokana na kukabiliwa na tuhuma mahakamani.
Nondo alifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Machi 21, akikabiliwa na makosa mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo kwamba “nipo hatarini” na kuzisambaza mtandaoni.
Kupotea na kufikishwa mahakamani
Usiku wa Machi 6, 2018 taarifa za kupotea kwa Nondo zilisambaa kila kona huku ndugu na viongozi wa TSNP wakijaribu kupaza sauti kwa vyombo vya habari ili kusaidia kupatikana kwake.
Jambo hilo lilizua hofu miongoni mwa ndugu na baadhi ya wanafunzi, wengi wao wakihofu huenda ametekwa kwa jinsi alivyojipambanua katika kukemea maovu bila woga.
Kwa mujibu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi UDSM, Jeremiah Jilili, taarifa za kupotea kwa Nondo zilienea baada ya kuonekana amejitoa kwenye makundi ya mitandao ya kijamii ikiwamo WhatsApp.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema Nondo alipatikana Machi 7, katika mazingira ya kutatanisha wilayani Mufindi jambo lililofanya afikishwe Polisi kutoa maelezo alifikaje eneo hilo.
Machi 8, Kamanda Bwire aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamefungua jalada la uchunguzi ili kubaini iwapo Nondo alitekwa au alitoa taarifa za uongo ili kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani. Wakati hayo yakiendelea viongozi wanne wa mtandao huo wa wanafunzi, walihojiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Waliohojiwa ni mwangalizi wa haki za binadamu, Alphonce Lusako; katibu wa mtandao huo, Malekela Brigthon; ofisa habari, Hellen Sisya na mkurugenzi wa idara ya sheria, Paul Kisabo.
Wakili wa wanafunzi hao, Reginald Martine alisema waliitwa kuhojiwa ili kutoa ushahidi kuhusu kutekwa kwa Nondo.
Machi 13, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kwa kushirikiana na Polisi mkoani Iringa, walifanya uchunguzi na kubaini mwanafunzi huyo hakutekwa, bali alijiteka ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kuzua tafrani kwa jamii.
Machi 21, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Iringa, John Mpitanjia alizuia dhamana ya mwanafunzi huyo kwa sababu za usalama akieleza kuwa maisha yake bado yapo hatarini huku akiomba muda wa kusoma vifungu hadi Machi 26.
Makosa yaliyompeleka mahakamani
Siku hiyo Nondo alisomewa mashtaka mawili na wakili wa Serikali, Abeid Mwandalamo. La kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7 akiwa Ubungo na kusambaza kwenye mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.
“Shtaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto Mafinga,” alidai Mwandalamo. Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo huku Wakili Mwandalamo akidai ushahidi haujakamilika, hivyo kuomba mtuhumiwa asipewe dhamana wakati upelelezi ukiendelea.
“Kulingana na umri wake, Serikali bado inamtegemea na akiachiwa kwa dhamana usalama wake utakuwa mdogo kwa sababu waliomteka hawajapatikana. Kwa sababu hizo mbili naomba asipewe dhamana,” alidai.
Kutokana na hali hiyo, wakili wa Nondo alimshtaki mkuu wa polisi nchini na wenzake wawili kwa kunyimwa dhamana mwanafunzi huyo licha ya kufikishwa mahakamani mara 15.
Kesi hiyo ilikuwa dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) akitaka mambo matatu; mteja wake apewe dhamana, waonane naye na aachiwe huru.
Machi 26, mwanafuzni huyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili walioweka bondi ya Sh5 milioni na kuwa na mali isiyohamishika huku akitakiwa kuripoti mahakamani hapo Aprili 4.
Soma Zaidi:
Asimamishwa, achunguzwa uraia
Baada ya kuachiwa kwa dhamana mwanafunzi huyo alikutana na barua ya kusimamishwa masomo kutoka kwa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye.
“Ni kweli na tumefanya hivyo kwa mujibu wa utaratibu, mwanafunzi anapokuwa amepandishwa kizimbani na kuwa na kesi ya kujibu husimamishwa masomo na anapomaliza kesi yake anarejea kuendelea,” anasema.
Aprili 4, siku aliyopaswa kuripoti mahakamani mwanafunzi huyo alihojiwa kwa saa mbili na Idara ya Uhamiaji na kuamriwa kujaza fomu kuhusu taarifa za uraia wake na kutakiwa kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wake.
Soma Zaidi:
Mei 10, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Iringa, ilipokea vielelezo vya kimtandao vilivyoletwa na upande wa mashtaka dhidi ya mwanafunzi huyo baada ya kupitia sheria mbalimbali za mitandao ya kijamii.
Mei 15, mwanafunzi huyo kupitia wakli wake, Jebra Kambole waliwasilisha barua katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa kwa ajili ya kumkataa hakimu wa mkoa, Iringa John Mpitanjia kutokana na kumtilia mashaka.
Mei 16, Hakimu huyo aligoma kujitoa kusikiliza kesi hiyo huku akieleza kuwa maelezo ya mshitakiwa yanayomtaka ajitoe hayana ushahidi wa kutosha. Baada ya muda kupita na kimya kingi kutawala kwa zaidi ya miezi miwili taarifa za kukamatwa kwa Nondo zikasambaa.
Nondo alikamatwa tena na polisi Julai 26, mwaka huu saa tatu usiku maeneo ya UDSM kwa kile kilichodaiwa ni kuonekana katika maeneo la chuo kinyume na sheria. Hata hivyo, aliachiwa kwa dhamana Julai 27, saa tisa alasiri baada ya kukaa mahabusu kwa saa 19.
Kwa mujibu wa Wakili Kambole, licha ya kukamatwa kwake polisi walishindwa kuonyesha uthibitisho wa kumzuia Nondo kufika eneo la chuo hicho.
Agosti 27, Mahakama ya Iringa ilimkuta mwanafunzi huyo na kesi ya kujibu huku ikipanga kuanza kusikiliza mashahidi wa utetezi Septemba 18 na 19.
Ashukuru, kurudi chuoni
Akizungumza baada ya kuachiwa huru na mahakama, Nondo alisema amefurahishwa na namna mahakama ilivyosimama kidete kutenda haki kuwashukuru mawakili wake, mtandao wa watetezi wa haki za binadamu na Watanzania wote waliokuwa nyuma yake tangu kesi yake ianze kusikilizwa.
Alisema kesi hiyo imemuongezea ujasiri na kuahidi kuendelea kutetea kwa nguvu zake zote haki za wanafunzi zitakapoonekana zinacheleweshwa, zinazuiwa au kunyang’anywa.
Soma Zaidi:
Nondo akizungumza na Mwananchi kuhusu kurejea chuoni, alisema alisimamishwa kwa mujibu wa sheria za wanafunzi chuoni, “Sasa kesi imeisha hivyo nitarudi chuo kama barua ilivyojieleza ingawa ni dhahiri sasa yapaswa kuanza kuangalia sheria tulizo nazo vyuoni mwetu kama zipo sawa. Unapomsimamisha mtu ina maana kwa tafsiri tayari umemuhukumu ni mkosaji wakati chombo chenye mamlaka ya kufanya hivyo ni mahakama, hivyo kuna haja ya kuanza kuangalia ‘fairness’ ya hizi sheria zetu ili zisiathiri wengine huko mbele”
Soma Zaidi: