Nyerere alivyomvuta Dk Salim kwenye siasa-1

Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere akiwa na mwanadiplomasia Dk Salim Salim. Picha na Maktaba

Dk Salim Ahmed Salim aliyezaliwa Ijumaa ya Januari 23, 1942 amekuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia wa Tanzania, aliyefanya kazi katika nyanja ya kidiplomasia ya kimataifa tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960.

Ni mwanadiplomasia nguli aliyehudumu katika nyadhifa mbalimbali duniani na alikuwa Waziri Mkuu wa tano wa Tanzania (1984-1985) na Katibu Mkuu wa nane wa OAU (1989-2001). Mwezi huu, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua makavazi ya kidijitali Dk Salim. Je, Dk Salim ni nani hasa?

Dk Salim alizaliwa katika Hospitali ya Mwembeladu, mjini Unguja. Wakati huo huduma za hospitali zilikuwa hazitoshi Pemba, nyumbani kwa wazazi wake, hivyo mama yake alilazimika kusafiri kwenda Unguja na kurejea nyumbani baada ya kujifungua.

Baba yake Dk Salim alitoka Pemba, ambako alifanya kazi kama karani katika Jumuiya ya Wakulima wa Karafuu, lakini mama yake alitokea Unguja.

Katika mahojiano aliyofanyiwa Februari 5, 2015, Dk Salim alithibitisha kwamba muda mwingi wa utoto wake aliishi Pemba, ingawa kwa vipindi tofauti alikuwa akisafiri kwenda Unguja.

Wazazi wake walipoteza watoto wao wawili wa kwanza, pacha kabla ya Salim kuzaliwa, hivyo ndiye mtoto mkubwa wa kiume katika familia ya ndugu 18. Mama yake Salim alifariki akiwa na miaka mitano, hivyo sehemu kubwa ya utoto wake alilelewa na mama wa kambo.

Dk Salim alisoma darasa la kwanza hadi la nane kisiwani Pemba kuanzia mwaka 1948 hadi 1956 katika Skuli ya Msingi Uweleni pamoja na skuli za Darajani na Mashimoni za Unguja.

Katika miaka hiyo alishiriki sana katika mchezo wa kuigiza na midahalo na pia skauti. Kushiriki katika harakati za skauti kulimsaidia kupata stadi nyingi za maisha.

Huko walifundishwa kuogelea, kupika, kutunza na kuwasaidia wengine, stadi za mawasiliano na muhimu zaidi heshima kwa wazee.

Kuanzia mwaka 1957 hadi 1960 Salim alipata elimu ya sekondari Unguja kuanzia kidato cha nne hadi 12. Kwanza katika shule ya sekondari ya wavulana ya Serikali (sasa Benbella High School) na kisha Shule ya Sekondari King George VI (sasa Shule ya Sekondari Lumumba).

Kuandikishwa kwa elimu ya sekondari siku hizo halikuwa jambo rahisi. Mtihani wa kujiunga na elimu ya sekondari ulikuwa na ushindani mkubwa na ni wanafunzi wachache tu waliodahiliwa.

Katika mwaka huo Dk Salim alifanya mitihani, ni yeye tu na mwanafunzi mwingine, Khamis Muhidin Vuai, kutoka wilaya yake, Mkoani, ndio waliofanikiwa kupata nafasi ya kujiunga.

Wakati wa miaka yake ya shule ya awali, Salim anakiri kwamba kulikuwa na watu kadhaa waliomlea nje ya darasa, miongoni mwao ni Francis X Salvi aliyekuwa akifanya kazi na baba yake.

Ingawa baba yake hakupata elimu ya juu, alijitoa sana watoto wake wapate elimu bora kwa kadiri alivyoweza. Salvi binafsi aliwafundisha masomo ya ziada Salim na nduguze.

Salim alimaliza shule ya sekondari mwaka 1960. Wakati huo alikuwa amejihusisha na mambo ya kisiasa shuleni pamoja na baadhi ya wanafunzi wenzake. Hadi wakati wa mitihani yake ya mwishoshuleni, tayari alikuwa ameamua kujiunga na mapambano ya kudai uhuru.

Baadaye, wakati akiwa balozi wa Tanzania nchini India, Salim akatumia fursa hiyo kujiendeleza kielimu. Kuanzia mwaka 1965 hadi 1968, alijiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika Chuo cha St Stephen's katika Chuo Kikuu cha Delhi, ambako alisoma historia na fasihi ya Kiingereza.

Akiwa New York, Salim aliendelea na masomo kwa kujiunga na shahada ya uzamili katika masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Columbia, New York.

Aliendelea na programu hiyo ya masomo alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.


Zanzibar na Tanganyika: Mapambano ya kupata uhuru

Nia ya Salim katika mapambano ya uhuru ilichochewa na Mwalimu Julius Nyerere wakati Salim akiwa na umri wa miaka 17. Alikuwa makamu mwenyekiti mwanzilishi wa Jumuiya ya Wanafunzi Wote Zanzibar na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichoanzishwa Desemba, 1955.

Nafasi zake katika jumuiya hizo zilimpa Salim nafasi ya fursa ya kuhudhuria mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1959 Mnazi Mmoja, Zanzibar.

Nyerere alizuru Zanzibar kutangaza PAFMECA (Umoja wa Ushirikiano wa Kupigania Uhuru wa Nchi za Afrika ya Mashariki na Kati).

PAFMECA ilianzishwa mkoani Mwanza Septemba 1958 kutokana na mkutano kati ya Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wa kitaifa kutoka Kenya, Malawi, Uganda, Zanzibar na Zimbabwe. Vyama vya ZNP na ASP viliwakilishwa katika mkutano huo.

Dhamira ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kuwahamasisha Wazanzibari kuungana kupigania uhuru, usawa na utu wa kila binadamu.

Dk Salim alivutiwa na maono ya Mwalimu Nyerere na alikiri hivyo alipohojiwa na Profesa Haroub Othman. Alisema: "Nilivutiwa na uelewa wa Mwalimu kuhusu hali ya kisiasa ya Zanzibar ... Ujumbe wake ulibaki kuwa kanuni elekezi katika maisha yangu."

Uanaharakati wake wa kupigania uhuru uliongezeka baada ya kumaliza shule, mojawapo ya malengo yake makubwa yalikuwa kufanya kazi kwa ajili ya umoja wa watu wa Zanzibar.

Hakufurahishwa na mgawanyiko wa kikanda uliosababisha mvutano kati ya Unguja na Pemba na migawanyiko ya kikabila na ubaguzi wa rangi iliyotawala Zanzibar.

Kwa mfano, kabla ya kuunganishwa na kuunda Afro-Shirazi Party (ASP) mwaka 1957 African Association (iliyoanzisha tawi lake la Zanzibar mwaka 1934) na Shirazi Association (iliyoanzishwa mwaka 1930) vilikuwa ni vyama tofauti.

Mgawanyiko huu ulijidhihirisha katika vurugu zilizofuatana na uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar. Uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1957, chaguzi zilizofuata, Januari 1961, Juni 1961 na Julai 1963, zilikuwa na migogoro mikali.

Baada ya kumaliza darasa la 12, Salim alijihusisha na uandishi wa habari. Nia yake ilikuwa kutumia maandishi yake kusaidia kuinua mwamko wa utaifa na kuwaunganisha wananchi katika mapambano dhidi ya ukoloni.

Mapambano dhidi ya utawala wa Waingereza yalikuwa yamefikia kilele chake. Alikuwa mhariri wa gazeti la ZNP na baadaye, gazeti la Umma party. Baadaye akawa mhariri wa gazeti 'Sauti ya Vyama Tisa', ambalo lilichapishwa na muungano wa vyama vya upinzani. Mbali na majukumu hayo, Salim pia alikuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Wanahabari Wote Zanzibar.

Mwaka 1961, akiwa na umri wa miaka 19, Salim alikuwa mmoja wa vijana watatu waliopata fursa ya kwenda Cuba. Wengine ni Ali Mahfoudh, ambaye baadaye alikuja kuwa kanali na mkuu wa operesheni na mafunzo katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Mohammed Ali Foum, ambaye alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia katika ngazi ya ubalozi katika Serikali ya Tanzania.

Viongozi wa ZNP, Abdulrahman Mohamed Babu na Ali Sultan Issa ambao walikuwa sehemu ya mtandao mpana wa kimataifa wa wanamapinduzi, walimteua Salim na wenzake kwenda Cuba, ambapo ZNP ilifungua ofisi ya Zanzibar huko Havana. Pia walifungua ofisi nyingine moja huko mjini Cairo, Misri.

Salim na wenzake walipaswa kufanya mapambano ya Zanzibar yajulikane duniani kote, hususan katika maeneo ya Caribbean na nchi za Amerika ya Kati na Kusini.

Huko Salim alishuhudia matokeo ya Mapinduzi ya Cuba katika kuondoa tawala kandamizi na kuanzishwa kwa jamii ambapo watu weusi na weupe walikuwa na haki na fursa sawa.

Nini kiliendelea baada ya hapo? Tukutane toleo lijalo.