Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Othman ‘anavyompoteza Maalim Seif Sharif Hamad’



Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo Zanzibar yamefungua ukurasa mpya wa kisiasa visiwani humo, huku pande hizo zikikubaliana kujadili hoja saba zilizowasilishwa na kuangalia namna ya kuzitafutia ufumbuzi kwa njia ya maridhiano.

Tamko la makubaliano hayo lilisomwa na kutiwa saini Julai 9, 2026 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, huku Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa serikali na dini wakishuhudia.

Hatua hiyo inatazamwa na baadhi ya wachambuzi wa siasa kuwa inaweza kuirejesha Zanzibar kwenye misingi ya maridhiano na huenda ikafungua njia ya kurejea kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ambayo tangu uchaguzi mkuu uliopita imekuwa katika hali ya sintofahamu.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, CCM iliibuka mshindi, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, ACT-Wazalendo kilitakiwa kuwasilisha jina la mwakilishi wake kwa Rais wa Zanzibar kwa ajili ya nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na kupata asilimia 23 ya kura.

Hata hivyo, chama hicho kilikataa kufanya hivyo kikieleza kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi na kudai kulikuwa na mambo yaliyohitaji kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha haki inapatikana.

Ili kufikia muafaka, CCM na ACT-Wazalendo vilianza mazungumzo Novemba 9, 2025 hadi Julai 9, 2026, ambapo walikubaliana kujadili hoja zilizokuwa zikilalamikiwa na kutafuta namna ya kuzitatua.

Si mara ya kwanza Zanzibar kufikia makubaliano ya kisiasa kati ya CCM na upinzani. Mara kadhaa kumekuwa na mazungumzo yaliyolenga kurejesha utulivu wa kisiasa, ambapo mengi yalihusisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye kiongozi wa ACT-Wazalendo, Hayati, Maalim Seif Sharif Hamad.

Muafaka wa kwanza ulifikiwa mwaka 2001 kati ya Rais wa wakati huo, Amani Abeid Karume na Maalim Seif baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, huku Umoja wa Mataifa ukisimamia mazungumzo hayo.

Mwaka 2010, viongozi hao walifikia makubaliano mengine yaliyosababisha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar na kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mazungumzo yalifanyika mwaka 2016 kati ya Rais mstaafu, Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif, lakini baada ya uchaguzi wa marudio CUF haikushiriki, hivyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa haikuundwa.

Mwaka 2020, mazungumzo mengine yalifanyika kati ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Maalim Seif ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo. Mazungumzo ya sasa yamehusisha Rais Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman.

Pamoja na historia hiyo, baadhi ya viongozi wa ACT-Wazalendo wanaona tofauti kati ya mtazamo wa sasa chini ya Othman na ule wa wakati wa Maalim Seif.

Wanasema safari hii lengo kubwa si kugawana nafasi za uongozi, bali kuweka misingi ya utawala bora na kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza baada ya uchaguzi.

Mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji (Babu Duni), alisema ana matumaini makubwa kuwa makubaliano ya sasa yatafuata mwelekeo tofauti kwa kuwa yamewekwa wazi kupitia tamko lililosainiwa.

Anasema katika kipindi cha nyuma Maalim Seif alikuwa akikabiliwa na lawama kwamba walikuwa wakikubaliana na viongozi lakini hakukuwa na nyaraka zilizoonyesha wazi yaliyokubaliwa.

“Safari hii kila mmoja ameona mambo wanayokubaliana, hivyo hakutakuwa tena na hoja ya kuuliza karatasi ziko wapi,” anasema Duni.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT-Wazalendo, Mansour Yussuf Himid, anasema chama hicho kinaamini kiko katika mikono salama chini ya Othman Masoud, akieleza kuwa ameonyesha ukomavu katika kusimamia mazungumzo hayo.

Anasema Maalim Seif alikuwa kiongozi muhimu katika harakati za mageuzi na demokrasia kwa zaidi ya miongo minne, lakini anaamini Othman ameendelea kusimamia misingi hiyo kwa mazingira ya sasa.

Kamati iliyokuwa ikimshauri Othman katika mchakato wa mazungumzo iliundwa na watu tisa, ikiongozwa na yeye mwenyewe. Wajumbe wengine walikuwa Juma Duni Haji, Omar Said Shaaban, Ismail Jussa, Nassor Ahmed Mazrui, Fatma Fereji, Omar Fakih, Salim Biman na Yussuf Himid.

Hata hivyo, utekelezaji wa makubaliano hayo ndio utakaobaini iwapo safari hii Zanzibar itaingia katika hatua mpya ya kisiasa au itarejea katika changamoto zilizowahi kujitokeza baada ya chaguzi zilizopita.