Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Plea Bargaining mfupa mgumu kwa Haki Jinai

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai  Tanzania kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Julai 15, 2023

Mambo mawili niliyothibitisha baada ya kusikiliza uwasilishaji wa Ripoti ya Tume ya Haki Jinai ni haya yafuatayo; mosi, Tanzania dola mseto wa Jamhuri (Republic) na Ufalme (Monarchy).

Pili, Tume ya Haki Jinai, imekwepa wajibu mkubwa ambao ilikasimishwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Matokeo yake, wamekabidhi ripoti yenye matundu. Wamerejesha mpira tena kwa Rais.

Dhahiri, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohammed Othman na timu yake yote, wamekwepa kurukiwa damu ya sakata la makubaliano ya punguzo la adhabu ya jinai, yaani plea bargaining.

Pamoja na suala la plea bargain, maeneo mengi ambayo Tume imebainisha kasoro zake, imeacha hewani bila mapendekezo ya namna bora ya utatuzi. Mwisho kabisa, mpira umerejeshwa kwa Rais Samia.

Katika hotuba yake fupi, baada ya kusikiliza uwasilishwaji wa ripoti, Rais Samia alisema kuwa tume iling'ata maneno kwenye eneo la plea bargain. Zaidi, akaibakiza tume hiyohiyo kazini kwa lengo la kuipa matokeo ya haraka ripoti hiyo.

Jamhuri na Ufalme

Jina la nchi ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba, sehemu ya utangulizi, Msingi wa Katiba, ni tamko la “wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” kuwa wanaunda taifa la uhuru, haki, udugu na amani.

Ibara ya kwanza ya Katiba, inatamka: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.” Kwa mantiki hiyo, nyaraka ya mwafaka wa nchi (Katiba), inaitambulisha dola ya Tanzania kuwa Jamhuri. Hili halibishaniwi!

Tafsiri; Jamhuri ni dola ambayo mamlaka ya juu kabisa yapo kwa wananchi. Huchagua viongozi na wawakilishi, kuendesha nchi kulingana na mwafaka wao wa kikatiba.

Ile tafsiri kuwa mamlaka ya juu kwenye nchi yapo kwa wananchi, hujengewa uzio kwamba dola ikishaitwa Jamhuri, maana yake wananchi wote wanakuwa sawa. Hakuna raia wa kipeo cha pili, mwingine wa kawaida au pungufu.

Ripoti ya Tume ya Haki Jinai, ukiielewa na kuitafsiri bila kumung'unya maneno, itakuonesha kuwa Tanzania ni Jamhuri kikatiba, ila sheria zilizotungwa na Bunge, vilevile matendo ya viongozi, vinasaliti Jamhuri.

Mathalani, nchi ni Jamhuri, ila wananchi wanakamatwa hovyo. Mamlaka za ukamataji ni nyingi na kuna mahabusu hazijulikani zilipo. Hivyo, ndugu wanaweza kumtafuta mtu wao, wakamkosa, kumbe ameshikiliwa mahabusu isiyojulikana.

Matumizi makubwa ya nguvu ni jambo ambalo limezungumzwa na Tume. Kwamba polisi na mamlaka nyingine za ukamataji, hutumia nguvu nyingi. Hili linafahamika. Na limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu.

Ukamataji. Tume imeeleza kuwa malalamiko makubwa ni watu kukamatwa na kukaa zaidi ya wiki mbili pasipo kufikishwa mahakamani, wakati sheria imetoa mwongozo wa ukomo wa saa 24, mtuhumiwa aliye mahabusu awe amefikishwa mahakamani.

Kwa mantiki hiyo, polisi au mamlaka nyingine za ukamataji, hivi sasa (japo inafahamika), zinaweza kumkamata mtuhumiwa na kumweka mahabusu hadi saa 168. Tume imeeleza hivyo.

Bila swali, huo sio msingi wa dola ambayo imejipambanua kuwa Jamhuri. Mila na desturi za Jamhuri hutafsiriwa ndani ya utawala wa sheria, na sio ubabe au utashi binafsi wa viongozi au vyombo vya dola.

Watuhumiwa wanakamatwa bila uwepo wa mashitaka. Wanawekwa mahabusu kwanza, kisha polisi wanahangaika kuandaa mashitaka. Upelelezi haujakamilika, kesi inapelekwa mahakamani. Mtuhumiwa anasota mahabusu miaka, upelelezi haujakamilika.

Huo sio utamaduni wa Jamhuri. Utawala wa watu, hauwezi kuruhusu raia aonewe. Hivi sasa polisi wanaweza kumkamata mtu kwa sababu binafsi, wakamtupa mahabusu bila msingi wowote, ndio maana kunakuwa na kesi nyingi za kubambikia.

Mwanzoni kabisa mwa uongozi wa Rais Samia, alieleza kubaini kuwa kesi za kubambikia ni nyingi. Ni kwa sababu ya mianya iliyopo. Kama polisi wanakamata, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka inapeleka watu mahakamani pasipo mashitaka.

Mahakama inaambiwa kuwa upelelezi haujakamilika. Kisha, mwananchi anasota rumande. Hali hiyo inatengeneza mwanya mkubwa wa kesi za kubambikia. Mila na desturi za Jamhuri zimesimikwa kwenye ulinzi mkubwa wa haki za raia.

Dola ya Ufalme, ndiyo ambayo mamlaka yote ya nchi huwekezwa kwa mtu mmoja. Kila kitu kinaamuliwa na mtu mmoja. Wengine jukumu lao kumshauri tu. Akisema mtu afungwe jela, kinachofuata ni utekelezaji.

Mfalme anakuwa mtawala, mkuu wa Mahakama na Bunge. Bahati nzuri dunia kwa sehemu kubwa, imeshahama kwenye dola za aina hiyo. UK (United Kingdom), ni dola ya kifalme lakini sio kamili. Mamlaka za Ufalme zimemeng'enywa na Bunge pamoja na Mahakama.

Mfalme Charles III ni Mkuu wa Dola ya UK, ila ni nembo tu ya nchi (figurehead). UK ina Bunge (wawakilishi wa wananchi) na Serikali ya Mfumo wa Bunge (Parliamentary Government), halafu ina Mahakama.

Mataifa mengi yanayobaki na dola ya Ufalme, yanachukua muundo wa UK. Hispania, Uholanzi, Ubelgiji, Denmark, Norway, Canada na Australia, kutaja kwa uchache, mfumo wake ni Ufalme wa Kikatiba, yaani Constitutional Monarchy. Kwamba nchi ni ya kifalme, ila inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba.

Nchi chache ndio ambazo zimebaki na mamlaka kamili ya Ufalme (Absolute Monarchy). Mathalan, Eswatini, zamani Swaziland, Mfalme Mswati III ndiye kila kitu. Uamuzi wake una unafunika mihimili yote ya dola. Amri yake ina nguvu kuliko Katiba.

Mfano mdogo, mwaka 2010, aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Eswatini, wakati huo ikiitwa Swaziland, Ndumiso Mamba, alituhumiwa kukutwa kitandani na aliyekuwa mke wa Mfalme Mswati III, Nathando Dube. Baada ya hapo, aliwekwa kizuizini. Alianza kuonekana mwaka 2020. Yaani miaka 10 baada ya tuhuma.

Hayo hayatofautiani na yaliyoelezwa na Tume ya Haki Jinai. Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wanaweza kuamrisha mtu kuwekwa mahabusu saa 48 bila maelezo yoyote. Wanaamua tu.

Mantiki ni kuwa kilichoelezwa kwenye ripoti ya Tume ya Haki Jinai, jinsi ambavyo Watanzania wanaweza kuwekwa mahabusu kiholela na kwa muda mrefu, pasipo mashitaka, dhahiri Tanzania kuna mahali sio tu inakwenda kinyume na misingi ya dola ya Jamhuri, bali inapitiliza Ufalme wa Kikatiba na kufanana na ufalme kamili.

Rais Samia amethibitisha kuwa anahitaji mabadiliko katika mifumo ya haki jinai Tanzania, ndiyo maana amezuia Tume ya Jaji Othman kuvunjika ili isaidie kutafsiri maoni yake na kurahisisha utekelezaji.

Plea Bargain

Januari 31, 2023, Rais Samia, alipokuwa anaikabidhi rasmi Tume ya Haki Jinai majukumu, alielekeza maeneo ya mkazo. Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alisema kuna kazi maalumu lazima ifanyike.

Kuhusu Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, Rais Samia aligusa moja kwa moja suala la fedha zilizopatikana kupitia plea bargain. Akaagiza Tume ya Haki Jinai, iingie ndani na ieleze kuhusu yanayosemwa.

“Nakumbuka hapo nyuma kidogo, kuna ngoma kubwa kidogo ilikuwa inachezwa. Mpaka kukusanya fedha za wale wa plea bargaining. Fedha nyingine zinaonekana, nyingine hazionekani. Ukifuatilia, utaambiwa kuna akaunti ilifunguliwa China. Tukatazame hayo yote,” alisema Rais Samia.

Kwa kauli hiyo, dhahiri shahiri, Rais Samia alitarajia Tume ya Haki Jinai ingerejesha majibu yenye mwanga kuhusu kashfa kubwa ambayo inaikabili Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, kipindi cha Mkurugenzi Biswalo Mganga.

Malalamiko ni mengi kuwa Biswalo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP) na Rais akiwa Dk John Magufuli, matendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu yalikithiri. Watu walilazimishwa kulipa fedha na zilipolipwa, hazikuingia serikalini, bali kwenye akaunti za watu binafsi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, alisema kuwa Biswalo alihodhi mchakato na fedha zote za plea bargain. Hata waliostahili malipo hawakulipwa. Fedha zote zilibaki ofisini kwake.

Kwa mantiki hiyo, Tume ya Haki Jinai, wajibu mkubwa iliyokuwa nao ni kuchunguza na kuweka hadharani tamu na chungu zote za plea bargain. Ukweli na uongo wa yanayosemwa, viwekwe hadharani.

Hata hivyo, Jaji Othman alipokuwa anasoma ripoti yake, alilirejesha suala la plea bargain kwa Rais Samia. Alimwomba Rais Samia aunde tume nyingine mahsusi kwa ajili ya suala hilo.

Tafsiri rahisi ni kuwa suala la plea bargain waliliona lina kina kirefu, ambacho ama walikiogopa au walibaini kwamba sakata ni zito na linahitaji kazi maalumu ili kubaini zote mbivu na mbichi.

Tume ya Rais inapoundwa inakuwa na mamlaka makubwa. Inapewa hadhi ya mahakama (quasi-judicial). Ina nguvu ya kuchunguza, kusikiliza shauri na kumwita yeyote ili kumhoji. Lengo ni kukamilisha taarifa na kumkabidhi Rais.

Tume ilikuwa na nguvu ya kumwita yeyote kwenye ofisi ya DPP ili kujua ukweli. Hata hivyo, imekwepa kikombe. Imeamua kurejesha mpira kwa Rais Samia. Ni kama Tume ya Haki Jinai imemwambia Rais Samia kuwa suala hili analiweza yeye mwenyewe.

Sasa, Rais Samia anapaswa kuamua moja kati ya matatu; mosi, kuteua tume nyingine maalum kwa ajili ya suala hilo, kama alivyoshauriwa na Tume ya Haki Jinai. Pili, kufanya uamuzi kwa njia ya mkato, maana limekuwa kizungumkuti. Hapa ataonesha upande ambao si wake. Ameshajipambanua kama muumini wa haki na utawala bora.

Tatu, kuliacha lipite. Yaani, kufunika kombe mwanaharamu apite. Maana, siku nazo zimepita. Katika hili, atakuwa hachori mstari mzuri wa uongozi. Ukiwa Rais wa nchi, unapaswa kusahihisha makosa ya nyuma na uchore mstari yasijirudie.

Kuweka hoja zote kwenye kapu moja ni kuwa Tanzania ni Jamhuri ya maigizo ya kisiasa. Nyaraka zinasema, vikevile nyakati za uchaguzi, wanasiasa kufanya sanaa mbele ya wananchi kuwa nchi ni Jamhuri, lakini matendo ya viongozi huonesha mwananchi si chochote. Ni kama dola ya Ufalme.

Plea bargainin ni mnofu unaomtaka Rais Samia autafune mwenyewe. Tume nyingine hapana, fedha za wananchi zinazidi kupotea. Akae na Tume ya Haki Jinai, wampe taarifa zao, aoanishe na alizokuwa nazo kabla, achukue uamuzi. Muhimu, atende haki.