Rais Samia anatakiwa awe ‘rais mwanasayansi si mwanasiasa'

Alinichekesha Baba Askofu, Benson Bagonza, aliposema katika umri wake amegundua watu wazuri huchukiwa kwa uzuri wao. Alikuwa akieleza hisia zake kuhusu Uchaguzi Mkuu KKKT 2023.

Watu wema wasingechukiwa dunia isingekuwa na simulizi ya Yesu (Issa A.S) kuundiwa njama ya kuwambwa msalabani. Muhammad (S A.W), asingeukimbia wanguwangu mji aliozaliwa, Makka, akakimbilia Madina.

Kwani Yusuf aliwakosea nini nduguze hadi wakamtosa kisimani? Uovu gani Samson aliwatendea Wafilisti hata wakamtoboa macho? Dhambi ipi ilimwangusha Ayubu mpaka akafilisika vile, akaandamwa na maradhi yale?
Uchukue ujumbe katika mfumo wa zigzaga, kutoka kauli ya Askofu Bagonza hadi Ayubu mgonjwa na mufilisi, madhumuni ni kushuhudia kuwa wema una kawaida ya kupita njia ngumu.

Huo ndio mkondo wa kila jambo zuri. Chuma ili kiwe imara sharti kipite motoni. Hakuna lelemama kwenye safari ya kusaka matokeo yenye alama ya kudumu.
Alisimulia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa Tabora, kuhusu hadithi ya binti mrembo mlimani, ambaye njia ya kumpata ilikuwa ngumu. Ilijaa vitisho, vishindo na mauzauza. Sharti lilikuwa moja; kwa vyovyote, hupaswi kugeuka nyuma!

Wengi walishindwa kuhimili vitisho, wakageuka nyuma na wakawa mawe. Kadiri unavyopanda mlima kumkaribia binti mrembo, ndivyo ungetishwa zaidi. Sauti za vitisho zingeongezeka.

“Mchinje huyo umeshamfikia.” Wengi waligeuka nyuma kumtazama mchinjaji, matokeo yake wakawa mawe.

Aliyefanikiwa kumposa binti mrembo mlimani ni kijana jasiri aliyeshinda vitisho vyote safarini. Katu hakugeuza shingo. Kelele nyingi alizokutana nazo njiani, alitambua zililenga kumtoa kwenye lengo kuu; kumfikia binti mrembo na kumposa.

Mwalimu Nyerere hakuacha hadithi inaelea, alifafanua kuwa ujenzi wa nchi hubeba shabaha kubwa ambayo safari ya kuielekea hukutana na matatizo mengi. Alisema kama dhamira ni imara basi hakuna kugeuka jiwe. Ikiwa dhamira ilijengwa na utani, utayumba, utageuka jiwe.
 

Baada ya muhtasari

Utangulizi juu ni muhtasari wa maudhui ndani ya ujumbe ninaoulenga kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Imeshatimu miaka miwili na nusu tangu aingie madarakani. Imebaki miaka miwili na mwezi mmoja, Taifa litafanya uchaguzi mwingine wa rais, wabunge na madiwani.

Miaka miwili na nusu imetawaliwa na hali ya kutengua na kuhamisha mawaziri. Wachache mno wanaondolewa, wengi wanahamishwa. Miaka miwili ijayo, panapo majaliwa ya Muumba, shabaha ya Rais Samia itapimwa. Je, ilikuwa imara au ilijengwa kiutani utani?

Sababu za kutengua na kuhamisha mawaziri; narejea maneno ya Askofu Bagonza kuwa wazuri wanachukiwa kwa uzuri wao. Watu wenye majungu, husuda na roho mbaya, wapo ndani ya nchi.

Amesema Mwalimu Nyerere, katika safari ya kujenga taifa la kijamaa, wezi, wanyang’anyi na watetezi wa ubepari wasingekosekana.

Kutoka waziri hadi waziri au katibu mkuu wa wizara mmoja mpaka mwingine, majungu, fitina na kulana visogo, havikosekani. Endapo Rais atashughulishwa na maneno ya watu kuliko kujikita kwenye shabaha, anaweza kuwaacha wazuri wenye kuchukiwa, akawapa nafasi wabaya wanaosifiwa.

Ujenzi wa nchi ni shabaha imara. Kutoka Zama za Shaba hadi Karne ya Sita Kabla ya Kristo (Zama za Chuma), Roma ilikuwa vijiji vya kijima. Ujio wa Wafalme wa Etruscan, ulileta mapinduzi ya ustaarabu wa ujenzi wa kimjini.
Kutoka mfalme mmoja hadi mwingine, Roma ilijengwa kwa miundombinu bora, majengo mazuri, hatimaye baada ya jitihada zenye jasho jingi la miaka 800, Roma ilipata mwonekano bora zaidi duniani. Ndio sababu ya msemo kuwa “Roma haikujengwa siku moja!”

Safari yoyote njema ina mapito magumu. Haikuwa mserereko kuijenga Roma. Mazuri hupigwa vita. Alishatahadharisha Mwalimu Nyerere. Muhimu ni kubaki kwenye shabaha ya kujenga nchi.

Kizuri hakikosi kasoro. Ndivyo wahenga walivyotuandaa kisaikolojia. Uzuri wa mzuri utafichwa chini ya zulia, ile kasoro itapata matangazo mengi. Bila shabaha imara kupitia kwa mzuri mwenye kasoro, atawekwa pembeni. Wafitini watashangilia.

Wafitini wanaweza kuunda na kutengua Baraza la Mawaziri, ikiwa Rais atayumbishwa na maneno. Wafitini pia wanaweza kudhibiti wazuri kuingia serikalini kwa sababu ya masilahi yao. Wafitini hupaza sauti kuliko wakweli na ukweli wao.

Inawezekana ujumbe huu unatumia njia ndefu kukifikia kitovu mahsusi. Unajumuisha mafumbo pengine. Hata hivyo, madhumuni ni kumtaka Rais Samia kutafsiri dhamira yake imara kwenye uteuzi wake, hasa mawaziri na makatibu wakuu wa wizara.

Wakuu wa mikoa na wilaya, hao anaweza kuwabadili atakavyo, asubuhi akawateua, mchana akawaapisha, jioni akawabadilisha vituo, usiku akawafukuza. Madhara ni madogo kulingana na aina ya majukumu.

Mawaziri na makatibu wakuu wa wizara ni tochi, vilevile ni tafsiri ya Serikali kutoka sekta hadi sekta. Ni tafsiri ya nchi. Haipaswi watu wa kubeba majukumu hayo wateulewi kwa kubahatisha. Haipendezi pia wateuliwa wa nafasi hizo wawe na vipindi vifupi kazini.

Inatakiwa waziri ateuliwe kwa vigezo visivyotia shaka. Rais amweleze waziri maono na matamanio. Waziri aende akakae na katibu mkuu wa wizara, wayatafsiri maono na matamanio ya rais. Wayatengenezee misheni na mikakati.

Waziri arejee kwa rais akiwa na mpango kazi madhubuti wenye kuainisha muda wa utekelezaji na matokeo. Rais akiupitisha, hilo ndilo linakuwa agano lao la kikazi. Kisha, Rais aunde viashiria vya ufanisi (KPIs), ambavyo muda baada ya muda, atavitumia kutathmini ubora wa waziri wake.

Kama waziri anafunga magoli mengi kwenye viashiria vya ufanisi, rais hapaswi kumtoa au kumbadilisha, hata kama wafitini wanamsema ni kiongozi mbovu kuliko. Rais anapaswa kukumbuka, kuielekea shabaha yake imara, anahitaji watu wazuri. Hao wazuri, hawataacha kusemwa.

Amesema Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln: “Sikiliza watu wote. Chuja kila unachosikia kwenye kioo cha ukweli. Chukua mazuri yaliyochujwa.”
Hakuna binadamu asiye binadamu. Katika kusikiliza na kuchuja ni rahisi kutambua pumba na mchele. Rais anapaswa kufanyia kazi ukweli ambao umeshachujwa kwenye kioo cha ukweli. Si kufanya uamuzi kwa presha za watu.

Sifa mojawapo ya rais katika nchi ya kidemokrasia ni uwezo wa kukabili presha ya kijamii. Unaweza kuwa na malengo mazuri lakini hayaeleweki vema kwa umma, ama kwa hofu au tafsiri potofu wanayoiamini. Rais anapaswa kusimama imara kuelekea matokeo. Hivyo ndivyo kutogeuka jiwe, kama alivyosema Mwalimu Nyerere.

Mwisho kabisa, ubora wa rais hautapimwa kwa tabasamu, vicheko na mapambio ya kijamii vipindi vya michakato, bali kwa matokeo atakayoonyesha. Rais makini ataheshimika zaidi atakaposema “wengi hamkunielewa ila matokeo haya yanadhihirisha shabaha yetu.”

Rais aliyefeli, atazungumza pembeni “tulitaka kuifanya Tanzania iwe Luxemburg, ila kelele zilipokuwa nyingi tukaacha mipango.” Rais lazima awe na uwezo wa kutafsiri maono yake, kusimamia misheni zake na kulinda mikakati yake hata nyakati za presha kubwa zenye kumpinga.

Ukizomewa, majibu sio kuwaangukia wanaokuzomea hata kama hawapo sahihi. Wewe utawazomea kwa matokeo.
Hutawazomea moja kwa moja, ila tambo za matokeo ndizo zitawafanya wazomeaji wa mwanzo wajione wanalipwa kisasi.
 

Matokeo sio siasa

Hili ni eneo muhimu ambalo natamani Rais Samia anielewe vema. Siasa ndio sanaa inayoleta uongozi wa Serikali na Bunge. Watumishi wa juu wa mihimili hiyo miwili ni wanasiasa. Ni vigumu kuwatenganisha wanasiasa na siasa, ila ukweli ni huu; matokeo ya ujenzi wa nchi hayataki siasa.

Kuifanya Tanzania iwe na umeme wa uhakika na wa kutosha, huduma za afya kuwa bora na zenye kutosheleza, elimu kuwa ya kisasa na yenye kwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia, uchumi kukua, kupambana na rushwa; yote hayo na mengine kama hayo, yanahitaji sayansi, sio siasa.

Amesema Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa “tufunge mkanda”. Alisemwa vibaya kila kanda ya nchi. Akaitwa “Mzee wa Ukapa”, kuonesha kuwa urais wake ni sababu ya fedha kukosekana mitaani. Hakurudi nyuma licha ya kuandamwa.

Alijielekeza kulipa madeni ili nchi ikopesheke, aweze kufanya aliyotamani. Mwisho alifanikiwa. Nchi ikafunguka tena. Alipokuwa anakabidhi nchi kwa mrithi wake, Jakaya Kikwete, hakuna aliyeuzungumzia Ukapa, isipokuwa sifa kwamba miaka 10 ya Mkapa, sio tu ilijenga na kustawisha uchumi wa nchi, bali pia hadhi ya Tanzania ilipanda katika uelekeo wa kiuchumi na uimara wa sarafu yake.

Mkapa angetaka kufanya siasa, angeyumba. Rais anatakiwa kuwa na uhusika thabiti ili kutimiza malengo yake. Mtetezi na mlinzi wa wasaidizi wake anapoona wanasingiziwa. Mkali kwa wazembe. Katili kwa wanaotumia ofisi za umma kujitajirisha.

Miaka 63 ya uhuru, kama nchi ingekuwa na mipango madhubuti, yenye kutafsiriwa kwa vitendo kutoka rais hadi rais, waziri mpaka waziri, vilevile makatibu wakuu wa wizara pasipo kuchepuka, Tanzania ingeshamiri na kujivunia matokeo ya muda mrefu.

Mithili ya tafsiri ya Hekalu la Jerusalem, kuanzia maono ya Suleiman, uratibu wa ujenzi wa Hiram wa Tyre, usanifu wa Hiram Abif, hadi jasho la Cyrus na mateka wa Babylon. Kutoka Mwalimu Nyerere hadi Samia na marais baada yake, ndivyo tafsiri ya ujenzi ya nchi inapaswa kusomeka.

Rais mmoja hawezi kutatua kila kitu. Inabidi kuunga alipoishia mtangulizi wake na kuendeleza hadi tamati yake. Muhimu ni kujenga nguzo za utumishi; nidhamu, uchapakazi, ukweli pasipo ubinafsi. Ujenzi wa nchi sio msako wa sifa binafsi. Rais makini ni yule mwenye kuhakikisha matokeo bora yanapatikana kuliko kuangalia nani atasifiwa.