RC Mtambi akemea makundi Baraza la Madiwani Musoma
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye kikao maalum cha kujadili hoja za CAG katika baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Mpasuko huo unaonekana kwa namna ambavyo wafuasi wa makundi hayo mawili wanavyoshambuliana kwenye makundi ya WhatsApp, huku kila moja likitetea upande wake na kukosoa upande mwingine.
Musoma. Ikiwa imepita miezi minane tangu kufanyika kwa uchaguzi uliomwingiza madarakani Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji pamoja na Baraza la Madiwani la Manispaa ya Musoma, mgawanyiko unaotokana na makundi ya kisiasa bado umeendelea kutikisa baraza hilo.
Mgawanyiko huo unaelezwa kuanzia wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kumpata mgombea ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini, makundi mawili yaliibuka, moja likimuunga mkono Mbunge Miraji na jingine likimuunga mkono Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Nyabiti.
Kutokana na hali inayosababisha makundi hayo kushambuliana, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ametia mguu akikemea mgawanyiko huo akisema unaathiri utoaji wa huduma na maendeleo kwa wananchi.
Kanali Mtambi ametoa kauli hiyo jana, Juni 25, 2026, wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Mtambi alisema ofisi yake haitasita kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya madiwani watakaobainika kuendeleza siasa za makundi, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa viongozi hao kuwatumikia wananchi badala ya kuendeleza tofauti za kisiasa.
"Sio kwamba hatuwaoni wala hatujui kinachoendelea. Niwatake muachane na huu mgawanyiko kwa sababu hauna manufaa yoyote. Uchaguzi umekwisha, sasa mnatakiwa kuisimamia halmashauri ili iwaletee maendeleo waliowachagua," amesema na kuongeza:
"Msitulazimishe kuchukua hatua zaidi kwa sababu uwezo huo upo kwa mujibu wa sheria na kanuni. Nafasi zenu zisilete doa katika halmashauri yetu, bali zitumike kuwaletea wananchi maendeleo na tabasamu."
Chanzo cha mgawanyiko
Chanzo cha makundi hayo kinatajwa kuwa ni ushindani uliokuwapo wakati wa mchakato wa CCM wa kumpata mgombea ubunge wa Musoma Mjini kati ya Mbunge wa sasa, Mgore Miraji, na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Vedastus Mathayo.
Hata hivyo, Mathayo hakurejeshwa na vikao vya juu vya chama kushiriki kura za maoni, hatua iliyodaiwa kuwakera baadhi ya wafuasi wake. Baadhi yao walitangaza kupitia mitandao ya kijamii, ikiwemo makundi ya WhatsApp, kumuunga mkono mgombea Juma Mokili.
Licha ya hali hiyo, Mgore aliibuka mshindi katika kura za maoni, akateuliwa na CCM kugombea ubunge na baadaye kushinda uchaguzi mkuu dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani.
Mpasuko huo ulizidi kushika kasi wakati wa uchaguzi wa meya wa Manispaa ya Musoma baada ya jina la aliyekuwa meya, William Gumbo kuondolewa katika mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo. Gumbo alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wakimuunga mkono Mathayo.
Baada ya hatua hiyo, madiwani waliokuwa upande wa Mathayo walimuunga mkono Alex Nyabiti ambaye hatimaye alichaguliwa kuwa meya.
Inaelezwa kuwa hadi sasa uhusiano kati ya makundi ya Meya Nyabiti na Mbunge Mgore si mzuri, hali inayodaiwa kuendeleza mpasuko ndani ya baraza hilo licha ya jitihada mbalimbali za viongozi kutafuta suluhisho la kudumu.
RC abadili mpangilio wa viti
Kutokana na hali hiyo, Kanali Mtambi amelazimika kubadili mpangilio wa ukaaji wa madiwani ndani ya ukumbi wa baraza, baada ya kubaini kuwa ulikuwa haukuzingatia utaratibu wa kawaida.
Kwa mujibu wa utaratibu, wenyeviti wa kamati wanapaswa kukaa sehemu moja, lakini katika kikao hicho walikuwa wamekaa kwa kujitenga. Mkuu huyo wa mkoa amewaagiza warejee katika mpangilio unaostahili na kupanga upya viti kwa kuwachanganya madiwani bila kujali kundi analotoka kila mmoja.
"Wewe Meya pia nasikia unashindwa kumuita Mgore 'Mheshimiwa'. Shida iko wapi? Niambie, Mbunge wa Musoma ni nani? Usiseme Mgore, sema Mheshimiwa Mgore,” amesema.
Harakati za kisiasa zaanza
Wakati huohuo, mpasuko huo umeelezwa kuchochea baadhi ya wanasiasa kuanza harakati za kuwania ubunge wa Musoma Mjini kupitia CCM katika uchaguzi ujao, huku majina ya baadhi ya wabunge wa viti maalumu yakitajwa miongoni mwa wanaotajwa kutamani nafasi hiyo.
Miongoni mwa viongozi waliokemea siasa za makundi ni Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, ambaye wakati wa ziara yake mkoani Mara Mei, mwaka huu, alisema chama hakitawavumilia wanachama wanaoendeleza makundi baada ya uchaguzi.
Alisema siasa hizo zinasababisha mpasuko ndani ya chama na kusisitiza kuwa mchakato wa kupata wagombea ulifanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo na Katiba ya CCM, hivyo wanachama wanapaswa kuheshimu maamuzi ya chama bila kujali nafasi au hadhi ya mwanachama husika.
Wakati huo huo, katika kikao hicho, Kanali Mtambi alimwagiza Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa, kuhakikisha mkandarasi Norplan anafikishwa mahakamani kwa madai ya kuwasilisha nyaraka za kughushi na kisha kulipwa zaidi ya Sh272 milioni kinyume cha sheria.
"Hoja hii inapaswa kufikia mwisho. Kinachotakiwa sasa ni kumfikisha mahakamani ili mahakama itoe tafsiri ya kisheria. Ni kweli mkandarasi anakiri kuwasilisha nyaraka za kughushi, lakini anadai kazi alifanya. Hilo sasa linahitaji uamuzi wa mahakama," alisema.