Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ruhusa ya Samia na vuguvugu la siasa Tanzania

Muktasari:

Wakazi wa Mwanza jana wamepata fursa ya kushuhudia kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka sita, mkutano wa hadhara wa kisiasa uliofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Viwanja vya Furahisha, jijini humo.

Wakazi wa Mwanza jana wamepata fursa ya kushuhudia kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka sita, mkutano wa hadhara wa kisiasa uliofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Viwanja vya Furahisha, jijini humo.

Kulikuwa na mikutano ya kisiasa mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu uliomwingiza madarakani aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hayati John Magufuli.

Lakini mikutano hiyo ilikuwa ya kampeni tofauti na huu ambao ni wa viongozi kuzungumza na wafuasi wao kuhusu masuala ya nchi yao. Mwaka 2016, Rais Magufuli alitoa agizo kuwa mikutano ya kisiasa ya majukwaani isitishwe mpaka wakati wa Uchaguzi Mkuu ili kutoa nafasi kwa chama chake – CCM, kutimiza ahadi zake ilizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Badala yake, vyama vya siasa viliruhusiwa kufanya mikutano ama ya ndani au kupitia wabunge na madiwani kwenye majimbo na kata wanazotumikia.

Hatua hiyo ililalamikiwa sana na vyama vya siasa na wanaharakati wa masuala ya utawala bora.

Wakati huo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa Kahama mkoani Shinyanga alilizungumzia hilo kwa kusema katazo la mikutano hiyo ni ushahidi kuwa utawala wa Magufuli umeamua kufuata siasa za kidikteta.

Leo, Mbowe anatarajiwa kuwa mzungumzaji mkuu katika mkutano huo wa Furahisha jijini Mwanza. Pamoja naye, karibu viongozi wote wa juu wa Chadema na wanachama wake maarufu wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo. Pasi na shaka, nchi nzima itatamani kujua nini kitatokea kwenye mkutano huo.

Lakini tumefikaje hapa? Jibu pekee ni moja; siasa za maridhiano za Rais Samia Suluhu Hassan.

Ushawishi wa Rais Samia

Katika makala aliyoiandika mwenyewe mwaka jana kwenye maadhimisho ya miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, Rais Samia alisema msingi wa utawala wake utajengwa kupitia kile alichoita 4R; Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Ukuaji). Katika sehemu ya andiko lake hilo, Samia alisema:

“Kwenye kujenga Tanzania bora ninatamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano. Ninatamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote. Hili litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wote. Ninaamini maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia”.

Ni maneno hayo ndiyo yaliyofungua mlango wa majadiliano baina ya CCM na muungano wa vyama vya siasa vilivyo ndani ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia (TCD). Desemba 15 mwaka jana, Rais Samia alihudhuria mkutano ulioandaliwa na TCD jijini Dodoma ambapo kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alizungumza hadharani kumwomba Rais awezeshe kutoka gerezani kwa Mbowe, aliyekuwa akikabiliwa na kesi mahakamani.

Hatua nyingine kubwa katika kufikiwa kwa hali hii ya sasa ilikuwa ni kitendo cha Rais Samia kuunda Kikosi Kazi maalumu, kilichojumuisha wadau tofauti, kutazama namna ya kuondoa vikwazo katika ufanyikaji wa shughuli za siasa hapa nchini.

Mojawapo ya mapendekezo ya kikosi hicho yalikuwa ni kuruhusiwa tena kwa mikutano ya kisiasa, jambo ambalo limefanyiwa kazi na Serikali.

Hata hivyo, kufikiwa kwa hali hiyo kunatokana pia na hatua za makusudi za Rais Samia kukubali kukutana na viongozi wa vyama tofauti, na zaidi, viongozi wa Chadema chini ya Mbowe, kwenye kujaribu kutanzua nchi kutoka katika mkwamo wa kisiasa iliyokuwamo.

Kisheria, hakukuwahi kutungwa sheria iliyokataza kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini. Hata hivyo, agizo la Rais lina nguvu inayofanana na sheria. Rais Samia alikuwa na mambo mawili ya kufanya, moja kuendelea na agizo hilo na pili kubadili kwa maslahi ya Taifa. Inaonekana wazi ameamua kufuata njia ya pili ambayo ndiyo sahihi.

Nini kitafuata baada ya hapa?

Chadema imeamua kuanzia Mwanza na bila shaka itaendelea na mikutano katika mikoa mingine baada ya hapo. Mkutano huu wa kwanza ni kama wa uzinduzi, na vyama vingine navyo vinatafuta namna ya kufanya uzinduzi wao katika maeneo mengine ya Tanzania.

Kuna kila dalili mkutano wa Mwanza utahudhuriwa na watu wengi, kwa sababu Watanzania wana kiu ya kusikiliza tena wanasiasa wakiwa wanachuana kupitia majukwaa ya kisiasa kama ilivyozoeleka tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Changamoto kubwa ambayo vyama vya siasa vitakumbana nayo, ni namna ya kufanya siasa pasipo kutoa picha kwa wananchi kuwa ni afadhali mikutano ilipopigwa marufuku kuliko sasa.

Wajibu mkubwa wa wanasiasa ni kuhakikisha kwamba wanatumia fursa hii kujenga Taifa lililo pamoja zaidi, kuliko lililogawanyika.

Ni rahisi kuona kwamba hatua hii ya Rais Samia huenda haikuungwa mkono sana na kundi la wahafidhina ndani ya chama chake.

Endapo vyama vya upinzani vitafanya mambo yatakayosababisha wahafidhina wapate nguvu ya kusema walikuwa sahihi kufanya walivyofanya huko nyuma, hilo litakuwa pigo kwa jitihada za Rais Samia.

Katika sayansi ya siasa, inajulikana kuwa ni rahisi sana kwa viongozi kurejea katika kile kinachojulikana kama “Comfort zone” (mazingira yaliyo salama kwao), endapo aina yoyote ya mabadiliko inaweza kuleta mvurugano au hali isiyo salama kwa utawala wake.

Hii ndiyo hatari kubwa zaidi katika hatua ambayo Tanzania ipo katika barabara yake kuelekea maridhiano kamili.

Kutokana na matukio yaliyotokea katika nchi kama Brazil na Marekani ambako matamshi ya viongozi kama Donald Trump na Jair Bolsonaro yalizua tafrani kubwa kiasi cha watu kuvamia na kufanya vurugu katika taasisi za dola, ni wazi kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha uhuru huu uliopatikana sasa unatumika kwa maarifa na uangalifu mkubwa.

Katika hotuba yake ya kuruhusu mikutano ya kisiasa, Rais Samia alizungumzia umuhimu wa wanasiasa kushindana kwa hoja kupitia majukwaa hayo na si kutumia fursa hiyo kutweza utu wa wapinzani wao au kutoa taarifa zenye lengo la kuchochea vurugu na kuvuruga maadili ya Kitanzania.

Watanzania wana hamu kubwa ya kusikia nini hasa wanasiasa watawaambia sasa, kitakachoendana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao kwenye nyakati hizi.

Ni wazi wananchi pia wana hamu ya kuwaona viongozi wao uso kwa uso, baada ya muda mrefu wa kuwasikia wakizungumza kupitia mikutano ya waandishi wa habari au kwenye mitandao ya kijamii.

Ni wazi kwamba Chadema wameamua kuanzia Mwanza wakijua ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya watu hapa nchini. Pia wakati fulani ukiwa mojawapo ya ngome zao kuu za kisiasa nchini.

Kwa vyovyote vile, wataitumia nafasi hii kujua ni kwa kiasi gani wananchi wanawaelewa na kuwafuatilia tangu mara ya mwisho walipowashuhudia kwenye mikutano ya namna hii.

Mwaka 2008, Chadema ilianza kujijenga kisiasa kupitia kile ilichokiita Operesheni Sangara ambapo viongozi wake walizunguka nchi nzima kukinadi chama hicho, lakini kampeni hiyo ilianzia kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa; wakianzia mkoani Mara kabla ya kuelekea Mwanza kwa minajili hiyo.

Mara hii, shukrani kwa uamuzi wa Rais Samia, wamepewa ruhusu za kuanza upya katika viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza.

Kila la heri kwa vyama vyote vya siasa ambavyo vitanufaika na ari hii ya maridhiano iliyopo nchini hivi sasa.

Imeandikwa na Michael Mwaigomole