Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekeseke la Waziri Katambi kuburutwa kortini, mwenyewe atoa kauli

Muktasari:

  • Asema hayupo tayari kuona kundi la watu wachache wenye maslahi binafsi likichezea amani iliyopo nchini kwa kujificha kwenye mwavuli wa haki za binadamu na demokrasia.



Dar es Salaam. Baada ya watetezi wa haki za binadamu na wanasheria kumfikisha mahakamani Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, wakipinga zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, Waziri huyo amesema yupo tayari kusimama mahakamani wakati wowote, hata saa nane za usiku, endapo ataitwa.

Katambi amesema hayuko tayari kuona kundi la watu wachache wenye maslahi binafsi likichezea amani iliyopo nchini kwa kujificha kwenye mwavuli wa haki za binadamu na demokrasia.

Kauli hiyo ameitoa jana, Julai 18, 2026, akiwa mkoani Shinyanga wakati akizungumza na makundi ya walinzi wa amani, wakiwemo Polisi Jamii, Sungusungu, wazee, wenyeviti wa mitaa, mabalozi na wenyeviti wa vitongoji mjini Shinyanga.

"Sipo tayari kuona kundi la watu wachache wenye maslahi binafsi linachezea amani iliyopo nchini kwa kujificha kwenye mwavuli wa haki za binadamu na demokrasia," amesema.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Dk Willibrod Slaa, kufungua kesi ya kikatiba kupinga zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Kesi hiyo imefunguliwa Julai 16, 2026, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Tabora, chini ya hati ya dharura dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo, walalamikaji wanapinga tamko la Katambi la Juni 26, mwaka huu, kuhusu kusitishwa kwa utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, wakidai linakiuka haki za msingi zinazolindwa na Katiba.

Pia, wadaiwa wamewaunganisha Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Wadhamini wa Chama cha ACT-Wazalendo kutokana na maslahi yao katika shauri hilo.

Chanzo cha mgogoro huo ni kauli iliyotolewa na Katambi Juni 26, 2026, bungeni jijini Dodoma, alipotangaza kusitishwa kwa utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara nchini.

Katambi alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na sababu za kiusalama na akamwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa katika maeneo yote ya nchi.

Walalamikaji wanadai kauli hiyo imeanza kutekelezwa na Jeshi la Polisi pamoja na maofisa wake, jambo walilosema limeathiri haki za wananchi kushiriki shughuli za kisiasa na mijadala ya umma.

Mbali na kesi hiyo, utekelezaji wa zuio hilo umeendelea kuibua maswali kutoka kwa baadhi ya wadau wa siasa, wanaodai kuwapo kwa viashiria vya upendeleo, baada ya baadhi ya viongozi wengine kuendelea kufanya mikutano hadharani.


Katambi: Niko tayari mahakamani

Akizungumzia suala la yeye kuburuzwa mahakamani, Katambi amesema hadi sasa hajapokea wito wowote wa mahakama, lakini hatasita kuitikia endapo atahitajika kufanya hivyo.

"Sijapokea wito wowote wa mahakama, lakini niko tayari kwenda hata usiku wa manane. Mahakama ndiyo chombo huru chenye mamlaka ya kusema Katiba imevunjwa, si mtu wala taasisi yoyote," amesema.

Akizungumzia hali ya usalama nchini, waziri huyo amesema Serikali haitaruhusu watu wachache wanaodaiwa kutumia ajenda ya haki za binadamu na demokrasia kuchochea chuki na kuhatarisha amani ya Tanzania.

Amesema kuvurugika kwa amani kuna athari kubwa kwa uchumi wa nchi, ikiwemo kupungua kwa watalii, kuyumba kwa uwekezaji, kusimama kwa miradi ya maendeleo na kudhoofika kwa mahusiano ya kidiplomasia.

Katambi pia amehoji kile alichodai ni ukimya wa baadhi ya wadau wanaotetea haki za binadamu katika kukemea vitendo vya uchomaji wa mali, mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi na uharibifu wa miundombinu ya umma.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kulinda amani ya nchi, akisema Tanzania haina mbadala na haiwezi kuruhusu mazingira yatakayoweza kuisukuma kwenye machafuko.

"Tumepewa dhamana ya kulinda amani ya nchi hii kwa mujibu wa sheria na viapo tulivyokula. Hilo hatutaliacha litikiswe na watu wachache wenye maslahi binafsi," amesema.