Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Selasini arejea Chadema, aomba radhi

Muktasari:

  • Mnyika aitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuendelea na kesi ya Lissu ili aachiwe mwanasiasa huyo huru.

Dar/Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema afya ya mwenyekiti wake, Tundu Lissu aliyepo gerezani inaendelea vema, baada ya madai ya kuumwa tumbo ambayo hata hivyo yalikanushwa na Jeshi la Magereza.

Sambamba za taarifa njema ya afya ya mwenyekiti wake, chama hicho pia kimempokea kada wake wa zamani, Joseph Selasini, aliyerudi kundini baada miaka sita tangu alipokihama mwaka 2020 kwenda NCCR Mageuzi.

Taarifa kuhusu afya ya Lissu imetolewa leo, Ijumaa Mei 22, 2026 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alipozungumza katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni Katiba Mpya “Free Tundu Lissu” mkoani Arusha.

Amesema kiongozi huyo amempa mambo mawili ya kuzungumza, ambayo ni kuendelea vizuri kwa afya yake na kuwataka wanachama wasonge mbele, wasirudi nyuma katika harakati wanazozifanya.

“Pamoja na afya kuendelea vizuri, akitoka gerezani lazima tupime kama aliwekewa sumu au hakuwekewa sumu,” amesema.

Sambamba na hilo, Mnyika ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuendelea na kesi ya Lissu ili aachiwe mwanasiasa huyo huru, kama ilivyowahi kufanya kwa mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Mbowe alipewa kesi ya ugaidi na iliisha kwa njia hiyo, kama waliweza kwa Mbowe wafanye hivyo kwa Lissu atoke au kesi isikilizwe kwa wakati,” amesema.


Selasini arudi Chadema

Mapema kabla ya mkutano huo, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi - Bara, Joseph Selasini ametangaza kurejea Chadema, akiomba msamaha na kudai alipata ajali ya kisiasa.

“Nilipata ajali ya kisiasa. Ilinipata, najua kuna watu waliumia, kuna watu walipata shida. Nimesimama hapa kuomba radhi kwa wale wote walioumia. Kwa chama, viongozi, kazi tuliyonayo ni ya taifa siyo mtu,” amesema.

Selasini amewahi kuwa mbunge wa Rombo mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chadema, kabla ya kuhamia NCCR Mageuzi.


Operesheni “Popobawa”

Mbali na matukio hayo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, amesema baada ya kumaliza kuzunguka katika kanda zote nchini, atarudi mkoani Arusha kwa Operesheni Popobawa”.

“Mimi nafanya kazi hii si kwa sababu ina mshahara. Hii kazi ina madhara sana. Sisi tunasimama hapa kusema majeshi kwa niaba yako na nchi yetu. Mnafikiri hatuna roho? Tuna roho, tuna wake na watoto wa kuangalia. Nimekimbiza familia hapa, nina upweke. Ningekuwa na uwezo ningechukua watoto na wanawake tubaki wanaume tupambane,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Boniface Jacob amesema ni muhimu kuwa na Katiba mpya ili kulinda rasilimali zilizopo nchini.

“Umuhimu wa Katiba mpya, kuna watu wanafikiri ni kitabu, ila Katiba mpya ni fikra na moyo wa taifa. Tunapigika wakati tuna rasilimali ikiwemo dhahabu, Tanzanite na Watanzania hatufanani na rasilimali zetu,” amesema.

Naye Deogratius Mahinyila, mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), amesema vijana wamechoka kuona vitendo vya uonevu vinavyoendelea na kuwa ikitokea vijana wamemkosoa mtu wanatekwa.

“Gen Z ni kizazi ambacho kinaamini katika teknolojia, hawadanganyiki, wanaamini katika uwazi na uwajibikaji. Siyo kila tatizo linatumia ustaarabu. Kila mmoja atumie njia anayoona anaweza kufikisha ujumbe. Ukiona unaweza kulia, lia. Ukiona unaweza kwenda kulala msikitini kusali, sali au fanya chochote,” amesema.

Mkutano huo haukumwacha nyumba Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Taifa, Sharifa Suleiman, ambaye amesema demokrasia ya kweli haiogopi mawazo tofauti, haiwezi kusimama kwa kufunga wapinzani, bali inasimama pamoja na haki.

“Akinamama, haki haiombwi, haki hutafutwa, tusimame imara tudai Lissu aachiwe huru na ikiwa hataachiwa huru tutachukua hatua mikononi mwetu. Tupaze sauti kudai Katiba mpya itakayoondoa changamoto zote zinazokabili taifa hili. Tunataka tudai Katiba mpya,” amesema.