Tozo Toziana

Muktasari:

  • Mimi sina haja ya kusoma magazeti au kuangalia taarifa ya habari au hata kujiunga na Jamhuri ya Twitter kujua kwamba hali si nzuri. Hali ya mlango wangu wa mbele huwa ni kiashiria tosha cha hali ya nchi.

Mimi sina haja ya kusoma magazeti au kuangalia taarifa ya habari au hata kujiunga na Jamhuri ya Twitter kujua kwamba hali si nzuri. Hali ya mlango wangu wa mbele huwa ni kiashiria tosha cha hali ya nchi.

Unauliza kwa nini? Ni huyu jamaa Musa Lendo! Maana akishachafukwa, lazima aje aonee mlango wangu, utadhani mlango ni mpinzani na ametumwa na wasiotaka maoni mbadala kuushughulikia. Jamani hata mlango!

Ndiyo hivyo. Juzi alijitokeza tena kama jini katika Bongo Muvi. Kapiga teke mlango na kuingia sebuleni kwa nguvu zote.

“We Makengeza, tunawajua. Tunawajua sana. Na dawa zenu ziko jikoni zikipikwa na vijana wetu kwa maelekezo ya wapishi wakubwa.”

“Kwani nimefanya nini?”

“Si unabisha tozo. Tozo ni maendeleo. Tozo ni maisha yetu. Tozo ni matumizi yetu sisi viongozi.”

“Ndiyo maana mimi ninawaambia mpunguze matumizi.”

“Wewe ni nani kutuambia kupunguza matumizi. Hujui tunavyohangaika usiku na mchana kuleta maendeleo ya nchi … usicheke! Tunavyohangaika … usicheke nimesema! Kwa nini tusijipongeze kidogo hapa na pale.”

“Magari yenu ni kujipongeza kidogo? Gari moja ni sawa na madarasa mangapi? Au zahanati ngapi? Au mikopo mingapi kwa vijana waweze kuanza kujikimu? Halafu uzidishe kwa idadi ya wilaya na maofisa wanaojipongeza kidogo. Na posho zenu na …”

“Shaddap. Ndiyo maana nasema dawa yenu iko jikoni.”

“Unaweza kutunyamazisha ni kweli lakini ukweli unabaki palepale na haufichiki. Iwapo pesa hazitoshi, kuna mawili, endelea kumkamua ng’ombe ambaye tayari ameshatoa tone lake la mwisho la maziwa, au punguza kunywa maziwa ili ng’ombe apate nafasi ya kurudisha nguvu zake. Na pia kumpeleka ng’ombe kwenye malisho mazuri zaidi.”

“Una maana gani?”

“Badala ya kuzidi kulemaza uchumi na tozo na kodi hii na ile na ile nyingine na ileeeeee, toa motisha uchumi kukua. Uchumi ukikua, mapato yatakua pia.”

“Tangu lini uwe mwuchumi. Hujui kwamba tuna miradi mikubwa ya kumaliza?”

“Ahaa. Kumbe ndilo tatizo lenyewe. Bahati mbaya hatakushirikishwa kutoa maoni kuhusu miradi yote hii. Kama pesa zimepwaya ni kosa letu? Si mseme ukweli juu ya hayo, tunaweza kuelewa.”

“Tuache hayo. Eti mmetoa tone la mwisho. Mbona michango ya harusi inaendelea kama kawaida? Ni zaidi ya tozo nakuambia. Ni zaidi ya tone, na ndoo na ndoo za maziwa ”

“Hapo nakubaliana na wewe. Lakini huwezi kutumia kisingizio cha matumizi binafsi ya watu kadhaa kuzidi kuwaumiza.”

“Lakini si watu kadhaa na tozo za harusi zinaumiza pia. Eti kiwango cha chini kuchangia. Na hadi ndugu na jamaa na jamaa wa jamaa na jamaa wa jamaa wa jamaa wote wanashirikishwa.”

“Sikatai. Na si hivyo tu. Siku hizi ni michango ya kupata mtoto, na kubatizwa, na kupokea, na kipaimara, na harusi, na kumbukumbu ya harusi, bila kusahau kuhitimu chekechea hadi chuo kikuu. Tozo za tuzo zimezidi.”

“Usisahau siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa. Na huwezi kuniambia kwamba ni matumizi binafsi ya hiari. Siku hizi tunashurutishwa na kutishwa hadi tuchange. Twatangazwa katika makundi sogozi ya Whatsapp kwamba hujatozia hadi usalimu amri na kutozika. Hizi tozo nyingine si hiari ni shari tupu.”

“Hayo yote nakubali Bwana Musa Lendo. Nakubali. Kuna sherehe nyingine hasa za watoto zinatakiwa kuwa za kifamilia tu, au kidini, lakini zimegeuzwa kuwa kama viharusi, hadi hata tukio la champagne (hata kama haina vilevi). Kisha watoto wanapachikwa pale mbele kama sanamu bila hata nafasi ya kuongea na wenzao. Najiuliza iwapo watoto wangeulizwa wanataka sherehe ya namna gani wangesemaje. Si ni sherehe yao jamani! Lakini ukiwaangalia watoto wahusika, wengi wanaonesha sura ya kuboreka kabisa.”

“Ndiyo maana tunataka watoe tozo kwa serikali badala ya haya matumizi ya hovyo. Sherehe zote za nini?”

“Ndiyo maana mnataka kusherehekea peke yenu. Inawaumiza waishiwa wakisherehekea?”

Musa Lendo akagonga meza kwa nguvu.

“Hawana uzalendo hawa. Wanataka kula peke yao.”

Nikabaki namwangalia Bwana Musa Lendo kwa mshangao. Yaani, ashakum si matusi, kweli ameshindwa mkundule?

“Unakodoa macho ya nini?”

“Kwanza Bwana ML una ugomvi gani na meza? Mlango tayari umenywea, sasa unataka kumaliza samani yote ya nyumbani kwangu? Na pili unadiriki kulalamika kwamba watu wanataka kula peke yao. Wakati wao wanajitahidi kupata angalau kapilao, nyinyi mnamaliza mapochopocho yote. Hamtaki kuonesha mfano. Au ni hadithi ya fanya nisemalo siyo nitendalo.”

Musa Lendo akasimama.

“Nimechoka na chokochoko zako. Wewe badala ya kupambana na matumizi mabaya ya tozo za waishiwa wenzio, unapigia kelele tozo zetu za Serikali ambazo ni kwa faida ya maendeleo ya nchi yetu.”

“Magari yenu ndiyo maendeleo? Matumizi yenu ndiyo maendeleo?”

Lakini Musa Lendo hakutaka kusikia tena. Akatoka akibamiza mlango tena na kuondoka huku akiimba “Tozonia Tozonia nakupenda kwa moyo wote …”

Nikashangaa. Iweje aimbe wimbo wa namna hii? Na nani anakataa kulipa kodi, hasa akijua kinagaubaga hizi kodi zinatumikaje kwa faida ya wananchi. Lakini kulazimishwa eti kwa kuwa tunatoziana sisi kwa sisi … duh!