Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Traore asaini makubaliano na Tanzania tiba za moyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Peter Kisenge (kulia) na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore wakibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo jana jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Ni ujumbe wa Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore, umetia saini ya makubaliano ya tiba kwa raia wake, mafunzo na tafiti kwa wataalamu wake pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba vya moyo kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeingia katika ushirikiano rasmi na Burkina Faso kupitia kusaini hati ya makubaliano, lengo likiwa ni kuboresha na kuimarisha huduma maalum za matibabu ya magonjwa ya moyo kati ya nchi hizi mbili.

Ushirikiano huo umetokana na mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika mwezi uliopita nchini Burkina Faso, yakihusisha Rais wa nchi hiyo, Ibrahim Traoré, Rais Mstaafu wa Tanzania (Awamu ya Nne), Jakaya Kikwete, na Profesa Mohamed Janabi, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hati hizo zilisainiwa jana, Mei 22, 2025, jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge, na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traoré.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Kisenge alisema kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini Burkina Faso na kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wanaokabiliwa na matatizo ya moyo.

“Tumekubaliana kuwasaidia katika kufanya tatifi, kuwafundisha  wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo na namna ya kutumia vifaa tiba, pia watawatuma wagonjwa ambao wameshindwa kuwafanyia upasuaji waje kutibiwa katika taasisi yetu," alisema.

Katika kutoa mafunzo ya kuwatibu wagonjwa wa moyo kuna wataalamu wetu ambao watakwenda Burkina Faso kufundisha na kuna wataalamu kutoka nchini humo watakaokuja  kujifunza katika taasisi yetu," alisema Dk Kisenge.

Dk Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kuhusiana na upatikanaji wa vifaa tiba wamekubaliana wanunue katika Bohari ya Dawa (MSD) ambao ni wasambazaji wa vifaa hivyo katika taasisi hiyo.

“Kwa namna ya kipekee tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha tiba ya magonjwa ya moyo, pia ninamshukuru Rais wa Bukina Faso, Kapteni Ibrahimu Traore kwa kuiamini nchi yetu.

“Kuwatuma wataalamu wake ambao tumesaini makubaliano nao ili nao kupitia sisi wawe taasisi bora ya matibabu ya moyo na kufika hatua tuliyoifikia sisi na leo tumeingia katika historia na Burkina Faso ya kutangaza utalii tiba ambao umekuja katika afya,"  alisema Dk Kisenge.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore ambaye kwa mara ya pili ameongoza timu hiyo ya wataalamu kuja hapa nchini alisema siku ya kwanza walipotembelea JKCI walivutiwa kwa huduma zinazotolewa.

Amesema pia wamevutiwa na uhusiano mzuri wa uongozi wa manejimenti uliokuwepo na kwamba watakaporudi nchini kwao watavifanyia kazi.

 “Ninawashukuru maraisi wetu wa Burkina Faso Kapteni Ibrahimu Traore na wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tayari kuimarisha huduma za afya katika nchi zao, nimevutiwa na JKCI kwani haitoi huduma tu Tanzania bali Afrika nzima  ndiyo maana nasi tumekuja kujifunza.

“Tunawategemea sana katika mafunzo, utafiti na matibabu ya moyo kwa afya za watu wa Burkina Faso," alisema Traore.