Tuwekwe wazi sababu za Waziri Simai kujiuzulu

Muktasari:

Huo usiri ukiwepo ndipo huzuka uvumi wa kila aina, huyu kasema hili na yule kasema lile. Juhudi zote hizi huwa ni za kutafuta siri iliyopo kwenye kile kilichofunikwa kawa, yaani ni nini hicho kinachofichwa?
 


Jamii ya waswahili imejenga utamaduni wa kulieleza jambo kwa umakini kwa kutumia mafumbo, methali au hekaya za kweli au za kubuni.


Pia, inaeleza mengi na kwa njia mbalimbali juu ya ubaya wa kuwepo usiri kwa kila jambo na hasa likiwa hilo jambo linawahusu wengi.


Huo usiri ukiwepo ndipo huzuka uvumi wa kila aina, huyu kasema hili na yule kasema lile. Juhudi zote hizi huwa ni za kutafuta siri iliyopo kwenye kile kilichofunikwa kawa, yaani ni nini hicho kinachofichwa?


Wiki iliyopita limezuka jambo hapa Zanzibar, lakini ukweli wake hasa haujulikani, japokuwa tukio hilo linauhusu umma ambao umeachwa kufikiria, kukisia au kukusanya kapu la kila aina ya uvumi na baada ya kutathmini kufikiria upi ni ukweli.


Jambo lililoibua mjadala kila pembe ya Unguja na Pemba ni kujiuzulu ghafla, tena kwa tangazo lililotolewa usiku, la aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said.


Mshituko wa kwanza ni kwamba hatua kama hii haijwahi kushuhudiwa Zanzibar, ingawa liliwahi kutokea tukio linalokaribia hilo kwa waziri kufanya hivyo baada ya kutakiwa kuwajibika.


Lakini Simai alipotangaza uamuzi huo hakukuwa na taarifa za aina hiyo na sababu ya kujiuzulu aliyoitoa ya kukosa mazingira rafiki katika utendaji kazi ndiyo yameleta kizungumkuti zaidi.
Watu wanauliza na wanayo haki ya kupata majibu. Kinachoulizwa ni mazingira gani hayo na zaidi kwa vile siku mbili kabla Waziri Simai alionekana kutofurahishwa na utaratibu wa kutoa vibali vya pombe ulioonekana umekiuka utaratibu unaotakiwa kufuatwa.


Hali hiyo aliiona Simai kama njia ambayo itaathiri utalii ambao mchango wake kwa fedha za kigeni kwa Zanzibar sasa unavuka asilimia 30.


Taarifa ya Ikulu imeeleza kwamba Rais Hussein Mwinyi ameridhia kujiuzulu kwa Simai na baada ya saa chini ya 24 tangu amepokea barua ya kujiuzuu Simai, akafanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Sasa uvumi umesambaa kila pembe huku watu wakiuliza kulitokea nini, huku zikiwepo simulizi nyingi katika sakata hili.


Jingine, ni kwa nini Simai ambaye anaheshimika kama mmoja wa mawaziri wenye ushirikiano mkubwa na vyombo vya habari na hasa kwa kuwa ni muwazi wakati wote, hakufunua kawa kuonyesha kilichopo ndani na badala yake kuacha kitendawili?


Lakini wengine wanaona taarifa ya Ikulu ingetoa sababu za kujiuzulu na hasa ukizingatia mambo mengi yanasemwa kuhusu kujiuzulu kwa Simai.


Mengine yanayosumbua watu na kila wakikuna vichwa, chawa aliyepo kichwani hapatikani, ni kwamba Simai amekuwa mtu wa karibu sana wa Rais Mwinyi tangu wakati wa harakati za kutafuta wagombea katika uchaguzi wa mwaka 2020.


Wapo pia wanaouliza ni peke yake aliyekuwa hayaoni mazingira rafiki ya kufanya kazi na je, nini kilipelekea aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Jamal Kassim Ali kuwekwa kando.
Jamal naye anasemekana ni mtu wa karibu wa Rais Mwinyi. Je, suala la kutokuwepo mazingira rafiki ya kazi pia linamhusu Jamal hata akawekwa pembeni?


Katika visiwa hivi vilivyozungukwa na bahari na uvumi mitandao ya kijamii imekuja na hadithi za kila aina, zikiwemo za wanasiasa wakongwe.

Ipo mitandao inayosema Jamal naye alikuwa na nia ya kukaa pembeni kama Simai, lakini panga liliteremshwa kabla hajamwaga wino wa kujiuzulu. Hapa umma unayo haki ya kujua ukweli.
Yote tisa, lililo muhimu ni kuwepo uwazi juu ya suala hili kwa vile limezaa kila aina ya tetesi, ikiwemo ile ambayo baadhi ya wachangiaji katika mitandao ya jamii wanaonyesha kilichofunikwa kawa sio kizuri kwa mustakabali wa Zanzibar.


Ukweli unasubiriwa kwa hamu na ghamu, kwani ukiona kitu kinafichwa basi kina jambo zito na aghalabu sio zuri.


Tunasema uwazi ni muhimili wa utawala bora na hili la Simai, waziri ambaye amekuwa muwazi katika utendaji kazi wake, nalo liwekwe wazi ili ukweli ujulikane na uvumi ambao hauna faida kwa maendeleo ya Zanzibar utoweke.