Prime
UCHAMBUZI WA MALOTO: Msimamo wa Mandela, ukatili wa Hitler, uovu wa Khomeini
Mjamaa wa Marekani, Bernie Sanders alipokuwa akizungumzia vita ya nchi yake na Israel dhidi ya Iran, alikumbushia mapinduzi ya Mohammad Mosaddegh, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Iran.
“Mosaddegh, wengi hawajui kuhusu Mosaddegh, lakini tulimwondoa kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia kwa ajili ya masilahi ya mafuta ya UK,” alisema Sanders.
Kauli ya Sanders inabeba lawama kwa nchi yake kwamba imekuwa ikiharibu nchi nyingine kwa hoja ya kubadili uongozi. Alisema kwa mfano Mosaddegh alivyoondolewa, ndipo aliyekuwa mfalme (shah) wa Iran, Mohammad Reza Pahlavi, alivyochanua kucha za udikteta, kabla ya kupinduliwa mwaka 1979, na utawala wa Kiislam kushika hatamu.
Mapinduzi ya Mosaddegh, chanzo chake ni UK kuona masilahi yake ya mafuta ya Iran, yanaingiliwa. Mosaddegh baada ya kukalia kiti cha Waziri Mkuu wa Iran, aliitisha ukaguzi wa nyaraka za kimkataba baina ya nchi yake na kampuni ya mafuta ya UK, Anglo-Iranian Oil Company (AIOC).
Kwa sasa AIOC ndiyo BP, ambayo ni kampuni ya kimataifa ya mafuta na gesi, yenye makao makuu London, Uingereza.
AIOC iligomea ukaguzi wa Serikali ya Iran. Kwa kukataa huko, Bunge la Iran wakati huo (Majlis), lilipiga kura ya uamuzi ulioitaifisha AIOC kuwa mali ya Serikali ya Iran.
Kuanzia hapo, aliyekuwa Waziri Mkuu wa UK, Winston Churchill, alizunguka akijenga ushawishi kwa mataifa ya Magharibi, akimpa wasifu Mosaddegh kuwa mkonunisti. Kisha, mashirika ya kijasusi ya M16 (UK) na CIA (Marekani), waliratibu mapinduzi, na kumwondoa Mosaddegh, halafu wakamweka Fazlollah Zahed, hatua ambayo iliimarisha nguvu ya Shah Pahlavi (kibaraka wa UK).
Kutoka Mosaddegh kuwa mkomunisti, hadi Jamhuri ya Kiislam ya Iran, kuitwa ya kidikteta. Ipo nchi ya kikomunisti, inaitwa China. Mifumo yake ya upatikanaji wa viongozi, na namna inavyoendesha serikali, inalandana kwa kiasi kikubwa na Iran. Tofauti iliyopo, Iran inafuata zaidi misingi ya sheria za Kiislam, China wametunga sheria zao ambazo hawaoni aibu kuzitekeleza.
Huwezi kukuta Marekani inaichezea China. Ni kwa sababu wanafahamu nguvu yake. Hutasikia kiongozi wa Marekani akipaza sauti kumwita Rais wa China, Xi Jinping, dikteta, lakini iliwezekana kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kumwita aliyekuwa Kiongozi Mkuu (Rahbar) wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kuwa dikteta na mtu mwovu kuwahi kutokea ulimwenguni.
Sauti ya Trump inapenya kwenye vyombo vya habari vikubwa, inajadiliwa, inachambuliwa. Angalau siku hizi teknolojia imeifanya dunia kuwa na milango bwerere ya taarifa. Hotuba za Khamenei zinatafsiriwa, dunia inamfahamu alikuwa binadamu wa ina gani, na kipi alikisimamia. Mtu mwenyewe, kwa utashi au kupitia mzani wa ukweli, anaamua kuamini yupi mwovu; Khamenei au Trump?
Ulimwengu wa giza, mtu angepewa jina baya, vyombo vya habari vingenadi ubaya wake, na kuyagonga nyundo maoni ya upande wa pili. Dunia ingemwona Shetani. Mathalan, kwa matamashi ya Trump, na nguvu ya vyombo vya habari vya Magharibi, kizazi kijacho kingeweza kupokea na kumhukumu Khamenei kama binadamu mwovu zaidi ambaye amewahi kuiongoza Iran.
Unaweza kupata picha katika Chama cha Ujamaa wa Kidemokrasia cha Urusi na baadaye Chama cha Kikomunisti. Vijana wanne, Leon Trotsky, Joseph Stalin, Grigory Zinoviev na Lev Kamenev, waliingizwa kwenye chombo kikuu cha uamuzi katika chama na Serikali (Politburo), kama sehemu ya wajumbe saba waanzilishi. Hiyo ilikuwa mwaka 1907.
Stalin hakumpenda Trotsky na alimuona ni mtu hatari kwa maslahi yake ya kisiasa, kwa hiyo akawashawishi Zinoviev na Kamenev, wakaunda utatu wa kisiasa na kidola ambao waliuita Triumvirate.
Walijiita Triumvirate wakijilinganisha na utatu wa Julius Caesar, Pompey na Crassus waliounganisha nguvu ili kuitawala Roma, miaka 60 Kabla ya Kristo ambao hufahamika kama The First Triumvirate na ule wa Anthony, Lepidus na Octavian unaofahamika kama The Second Triumvirate, miaka 43 Kabla ya Kristo.
Trotsky akajikuta kwenye mapambano na Triumvirate. Stalin hakuwa na ushawishi mkubwa, hivyo aliwatumia Zinoviev na Kamenev kumshughulikia Trotsky kwenye chama na serikalini. Trotsky akaitwa msaliti, jina likakua.
Baada ya Trotsky kupungua nguvu, Stalin aliwageuka Zinoviev na Kamenev akawachachafya kuwa nao ni wasaliti. Alifanikiwa maana Aprili 3, 1922, Stalin alikamata mamlaka ya chama cha Kikomunisti na baadaye kuongoza Dola ya Kisovieti.
Hata baada ya kukamata nafasi hiyo, Stalin alimhofia Trotsky, hivyo ili kuzidi kumchafua alihakikisha anatambulika rasmi serikalini kama msaliti kwa jina la Yuda Trotsky, yaani Msaliti Trotsky. Vyombo vya habari vikamwita Trotsky msaliti, jina maarufu Yuda Trotsky mpaka kitabu kiliandikwa kuchambua usaliti wa Trotsky kutokana na matakwa ya Stalin.
Oktoba 23, 1926, Stalin alitumia mamlaka yake kushawishi na kumfukuza Trotsky kwenye chama na kumvua vyeo vyote alivyokuwa navyo, ikiwemo ujumbe wa Baraza la Politburo. Warusi kwa sehemu kubwa, kutokana na mapokeo ya vyombo vya habari, walimhukumu Trotsky kuwa msaliti, na Stalin walimwita mzalendo.
Karne ya 21, ni milenia ya tatu, kinaishia kizazi chenye kupokea bila kuhoji, kinatamalaki kizazi cha kuhoji pasipo kutafuta taarifa. Matokeo yake, lipo wimbi linaibuka hivi sasa, likimtetea Adolf Hitler kuwa hakuwa mwovu, isipokuwa alisingiziwa na Maghadibi. Kampeni yake ambayo ilisababisha Wayahudi milioni sita wapoteze maisha, inapingwa. Ni kizazi kinachohoji zaidi kuliko kuzama kutafuta ukweli, na kuubaini uongo.
Kizazi cha kuhoji bila kuyasaka maarifa, ndiyo sababu lipo wimbi la kumtetea Idi Amin Dada, kwamba hakufanya jambo baya. Wanasema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiye alikuwa mshari. Hawakubaliani na ukweli kuwa Amin alivamia Kagera na kuua Watanzania.
Je, wanaowatetea Hitler, Amin na madikteta wengine hawana hoja? Utawahukumu kwa uvivu wao wa kutozama kuuchimba ukweli, kuuelewa na kuukumbatia, lakini mifano yao ina mantiki. Mathalan, wanapomtetea Hitler, wanasema hapo zamani za kale, kabla Nelson Mandela, hajawa Rais wa kwanza wa kidemokrasia Afrika Kusini, aliitwa gaidi hatari wa dunia.
Kwamba Magharibi wanapoamua, au mwenye kujua kutumia vyombo vya habari anapokuwahi, unaweza kuimbwa kwa sifa mbaya kila upande wa dunia. Yapo yatasemwa ambayo yatakuacha kinywa wazi ukihoji kama huyo anayesemwa ni wewe.