Usiri watawala vikao vya CCM

Muktasari:
- Usiri watanda vikao vya CCM, watia nia 3,293 wa ubunge wakiwa kwenye sintofahamu ya mchujo wa Kamati za Siasa.
Dar/ mikoani. Usiri umetawala wa kinachoendelea ndani ya vikao vya Kamati za Siasa za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ngazi ya mikoa vitakavyotoa mapendekezo ya kuwafyeka watiania 3,293 wa ubunge.
Kwa mujibu wa taarifa ya karibuni ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla watiania wa nafasi ya ubunge katika majimbo 272 ya bara na visiwani wako 4,109, lakini Kamati za Siasa zinalazimika kutoa mapendekezo ya kukata majina 3,293 na kubaki majina 816 yakiwa matatu kwa kila jimbo kisha yatapendekezwa kwenye Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Kamati Kuu pia, itafanya kazi ya kuondoa majina 544 na kubakiza 272 ambao watakuwa wagombea wa CCM na vyama vingine vya upinzani.
Leo, Julai 10, 2025, Kamati za Siasa za mikoa zimemaliza kuchuja majina ya watiania wa nafasi za udiwani na kuteuwa majina matatu kwa kila kata/wadi watakaokwenda kuchuana na wagombea wa vyama vingine vya siasa.
Makalla kwenye taarifa yake, amesema waliochukua fomu kwa majimbo Tanzania Bara wako 3,585 na Zanzibar 524, jumla katika majimbo walioonesha nia wako 4,109 na majimbo yako 272.
Pia, Makalla amesema upande wa uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu za kutia nia ni wanachama 503 wakati Umoja wa Wanawake (UWT) wako 623, Tanzania Bara na ndani yake wako 61 wa makundi maalumu lakini Zanzibar wamechukua wanane.
Kwa viti maalumu vya uwakilishi kule Zanzibar, amesema wako tisa, kwa hiyo jumla ya UWT waliojitokeza ni 640 lakini umoja wa vijana wamechukua 161 na Zanzibar wako saba.
Amesema Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara wako 55 huku Zanzibar pamoja na uwakilishi wako 575.
Uchunguzi wa Mwananchi
Mwananchi imefanya uchunguzi katika baadhi ya ofisi za CCM mikoani na imebaini kuwapo hali ya usiri na utulivu ambayo imezima tambo na majigambo, badala yake imeongeza "matumbo joto" kwa watia nia wengi.
Katika kipindi hiki kigumu, simu kutoka kila kona zimekuwa zikivuma kwa lengo la kutafuta faraja na taarifa za kinachoendelea.
Wengine wamejitokeza kujinadi kama watu wenye ‘habari za ndani’ wakibashiri matokeo huku wakijipatia umaarufu wa muda kwa madai ya kuwa karibu na vyanzo vya uhakika, ingawa mara nyingi taarifa hizo hukosa uthibitisho rasmi.
Hali ya ‘matumbo joto’ kwa watia nia imeongezeka kutokana na ilivyojionesha kwenye maeneo mengi ya ofisi za mikoa za CCM.
Jijini Dar es Salaam, ukimya, usiri na ulinzi ulitawala katika ofisi za CCM mkoa ambako Kamati ya Siasa ya Mkoa ilikuwa ikiendelea na kikao cha mapendekezo ya mchujo wa watiania wa ubunge huku nafasi ya udiwani mchujo wake ukikamilika jana.
Tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:13 jioni, wajumbe walikuwa bado ndani ya kikao, huku makada na wakeleketwa waliokuwa nje ya jengo hilo, wakionekana kubadilishana mawazo kwa tahadhari.
Ulinzi mkali uliimarishwa, askari kanzu wakiwa wamezunguka kila kona, huku walinzi wa chama waliovaa sare na kofia nyeusi wakisimamia lango kuu la kuingilia.
Magari yote yaliyotaka kuingia yalifanyiwa upekuzi mkali, mengine yakizuiwa na kuagizwa kupaki mbali, huku waliomo wakihojiwa kabla ya kuruhusiwa kuelekea ndani.
Mfanyakazi mmoja ameeleza kuwa, ulinzi huo maalumu uliwekwa ili kuhakikisha wajumbe wanatekeleza majukumu yao bila bughudha au usumbufu wa aina yoyote.
Jijini Dodoma Kamati ya Siasa imeendelea kujadili na kuchambua majina ya watiania wa ubunge wa majimbo, viti maalumu vya ubunge na udiwani, kabla ya kuyapeleka kwenye ngazi za juu kwa hatua zaidi.
Kwa nafasi za udiwani viti maalumu, mchakato unahitaji kasi kwa kuwa, Julai 20, 2025 ni siku rasmi ya upigaji kura kuwachagua waliopitishwa.
Mkoa wa Dodoma, hadi leo mchana kulikuwa na utulivu huku kikao kikiendelea ndani kwa usiri mkubwa.
Fomu za wagombea zimehifadhiwa ofisi ya katibu wa mkoa na hutolewa kwa taratibu maalumu kwa ajili ya kupitia na kupanga majina ya watakaoshindanishwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Mkoani Kilimanjaro nako ukimya na usiri umeendelea kutawala katika ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro, wakati Kamati ya Siasa ya mkoa huo ikiendelea na kikao cha ndani kwa siku ya pili, kujadili majina ya watiania wa ubunge na udiwani.
Kikao hicho kinafanyika kwa faragha tangu Julai 9, 2025, katika ukumbi maalumu wa ofisi hizo, huku hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia zaidi ya wajumbe wa kikao.
Mashuhuda wamesema wajumbe waliingia saa 4:00 asubuhi na kujifungia hadi jioni.
Taarifa kutoka ndani ya chama zinaeleza kuwa, mchakato huo ni hatua ya awali kabla ya majina kupelekwa ngazi ya Taifa kwa uteuzi rasmi.
Hadi saa 9:55 alasiri ya jana, wajumbe walitoka kimya kimya bila kuzungumza na waandishi wa habari.
Mkoani Mwanza, vikao vya uchujaji vya wagombea wa nafasi za udiwani, viti maalumu na ubunge vimeendelea kwa ratiba, huku ripoti ya mwisho ya wagombea waliopitishwa ikitarajiwa kutolewa baada ya kumalizika kwa mchakato mzima.
Majina hayo hayatatangazwa na wajumbe wa vikao vya mkoa, bali yatatangazwa rasmi na Kamati Kuu ya Taifa ya CCM.
Hali ya kisiasa mkoani Mwanza ni tulivu na hata watiania hawajahudhuria kwa wingi vikao, huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikifanyika kawaida.
Waandishi wa habari na wasio wajumbe hawaruhusiwi kusogea karibu na maeneo ya vikao, huku walinzi wakihakikisha usalama na usiri.
Kwa mikoa ya Tabora na Geita pia imeonesha hali sawa ya utulivu na hadi sasa hakuna mizozo au mkusanyiko wa watu wasiohusika, huku uongozi wa CCM mikoa hiyo ukitangaza kutoa taarifa rasmi mara mchakato utakapokamilika.
Mkoani Simiyu wajumbe wa Kamati ya Siasa wamejifungia ndani ya ukumbi wa ofisi za chama kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 9:56 alasiri, wakijadili majina ya watiania wa ubunge na udiwani.
Hakuna mtu yeyote asiyehusika aliyeruhusiwa kuingia, hata baadhi ya makatibu wa wilaya walibakia nje wakisubiri taarifa kutoka kwa waliokuwepo ndani.
Nje ya ukumbi, hali ilikuwa ya wasiwasi mkubwa, vikundi vya wanachama wa CCM vilizungumza kwa sauti ya chini, wengine wakipiga simu kwa watu waliotajwa katika mchakato wa uteuzi, huku wapambe wa wagombea wakizunguka kwa tahadhari.
Baadhi wamebashiri matokeo kabla ya kutangazwa rasmi, huku wengine wakionesha hisia za mshangao au kukata tamaa kimya kimya.
Baada ya saa saba za kusubiri jana, hakuna tangazo lolote rasmi kuhusu waliopenya au waliokatwa, hali iliyoongeza shaka kwa waliokuwa nje ya kikao.
Mkoani Morogoro, tofauti na misimu mingine, idadi ya watu waliokuwa ofisini kupita kiasi imepungua sana huku walioonekana ni wale waliohusika na vikao hivyo.
Mmoja wa watiania aliyeomba jina lake kuhifadhiwa amesema hawezi kuzungumza kwa sasa kwa kuwa, vikao bado vinaendelea na uamuzi wote ni siri kulingana na kanuni za chama.
"Sipaswi kujua chochote hadi vikao vitaisha," amesema.
Jijini Mbeya hali ya ukimya imeendelea kutawala katika ofisi za CCM Mkoa wa Mbeya huku baadhi ya viongozi waliohusika na vikao wakipishana na makada wengine.
Mwananchi imefika ofisini humo na kuona baadhi ya makada wakiwa katika makundi wakijadiliana mambo mbalimbali.
Ofisi za Katibu wa CCM mkoa, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Wazazi na Umoja wa Vijana zilikuwa wazi na wahusika waliendelea na majukumu yao.
Imeandikwa na Hamida Shariff (Morogoro), Samwel Mwanga (Simiyu), Saada Amiri (Mwanza), Habel Chidawali (Dodoma), Tuzo Mapunda (Dar es Salaam), Saddam Sadick (Mbeya) na Florah Temba (Kilimanjaro).