Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi Chadema wafurika makao makuu kusubiri tamko

Muktasari:

  • Vikao viwili vinafanyika kuamua kauli ya pamoja itakayotolewa na Chadema, siku tatu baada ya mauaji ya kada wake, Ali Kibao.

Dar es Salaam. Wafuasi na wanachama wa Chadema, wazee kwa vijana wanawake kwa wanaume, wamejitokeza katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Mikocheni, jijini Dar es Salaam kusubiri tamko la viongozi wao.

Tamko hilo ni matokeo ya kikao cha viongozi wote wa chama hicho, Dar es Salaam na Pwani Kaskazini kuanzia ngazi ya Kata kilichofanyika katika ofisi hizo zilizopo Mikocheni.

Kikao hicho kimetokana na wito wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alioutoa akiwa mkoani Tanga baada ya mazishi ya Kada wa chama hicho, Ali Kibao ambaye Septemba 8, mwaka huu, mwili wake uliokotwa eneo la Ununio, Dar es Salaam, baada ya kutekwa na kuuawa na watu wasiojulikana.

Katika mazishi hayo, Mbowe alisema baada ya msiba, Septemba 11, 2024 viongozi wote wa Dar es Salaam na Pwani Kaskazini kuanzia ngazi ya kata, majimbo, mabaraza (wanawake, vijana, wazee) na Taifa wanapaswa kukutana katika ofisi hizo kwa kile alichodokeza, watakuwa na jambo lao.

Mwananchi iliyofika katika ofisi hizo dakika 20 kabla ya muda uliyotajwa kuanza kwa kikao hicho saa 9:00 alasiri, imeshuhudia mamia ya watu nje ya ofisi hizo, wengi wakiwa wamevalia sare za Chadema.


Kwa kadri muda ulivyozidi kusogea na ndivyo idadi ya wafuasi na wanachama ilivyokuwa inaongezeka, wakishushwa na mabasi aina ya Eicher na Coaster kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Wajumbe wa kamati Kuu wa chama hicho walishuhudiwa wakiingia na kutoka, huku viongozi wakiendelea kuongezeka.

Ulinzi uliimarishwa katika geti la ofisi hiyo, hakuna aliyeruhusiwa kuingia bila kujisajili kwa kuandika jina lake na anwani.

Saa 9:55 alasiri, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge alitoka kwenye kikao cha Kamati Kuu na kutoa ratiba na itifaki za tukio lote.

Kwa mujibu wa Ruge, mkutano na waandishi wa habari utafanyika baada ya vikao viwili, ambavyo ni Kamati Kuu, kisha viongozi wa majimbo, vyote vinaongozwa na Mbowe.

Nyimbo zilizotajwa kuwa za ukombozi ndizo zilizokuwa zinasindikiza subira ya wanahabari na wanachama wengine, kuelekea tamko litakalotokana baada ya vikao hivyo.

Kila aliyejuana na mwingine walionekana kupiga soga na wengine wakikaa kwa makundi na wazee wa kujitenga hawakukosekana, kwa sehemu kubwa vijana ndiyo waliohudhuria zaidi tukio hilo.

Kauli za masikitiko juu ya kifo cha Kibao ambaye aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema ndizo zilizosikika miongoni mwa wanawake wengi waliokuwepo katika kusanyiko hilo.

“Hakuna kinachofanywa kwa bahati mbaya, wanajua wanachokifanya na wanajua walipo waliowateka,” alisikika mmoja wa wafuasi aliyevalia kofia la nyekundu aina ya baret.

Saa 10:34 jioni, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu alifika katika ofisi hizo, tayari kwenda kushiriki kikao cha Kamati Kuu kilichokuwa kinaendelea.


Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali