Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi waliosimamishwa Chadema watinga kwa Msajili na hoja nane

Muktasari:

  • Katika barua ya pamoja ya malalamiko iliyoandikwa Julai 15, 2026 na kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa leo, viongozi hao wameainisha hoja nane wakidai mchakato wa kusimamishwa kwao haukuzingatia taratibu za chama, Msajili akiri kupokea barua yao akiahidi kufanyia kazi.

Dar es Salaam. Mvutano na kutunishiana misuli ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumeendelea kushika kasi baada ya viongozi watatu waliosimamishwa nyadhifa zao kufikisha barua ya malalamiko katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wakidai hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi yao zilikiuka katiba na kanuni za chama.

Viongozi hao ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Muheza, Joseph Mwakidasi, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilindi, Mathias Cosmas, na Katibu wa Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okolo.

Katika barua ya pamoja ya malalamiko iliyoandikwa Julai 15, 2026 na kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa leo Jumanne, Julai 21, 2026, viongozi hao wameainisha hoja nane wakidai mchakato wa kusimamishwa kwao haukuzingatia taratibu za chama.

Miongoni mwa hoja hizo ni kusimamishwa bila kupewa taarifa rasmi kwa maandishi kuhusu tuhuma zinazowakabili kabla ya kutakiwa kujibu, kunyimwa haki ya kusikilizwa na kujitetea mbele ya vyombo halali vya kinidhamu, pamoja na uamuzi wa kusimamishwa kutangazwa hadharani na viongozi binafsi badala ya kufuata utaratibu wa chama.

Pia wamedai hawakupewa sababu za maandishi ambazo zingewawezesha kutumia ipasavyo haki yao ya kukata rufaa.

Viongozi hao walisimamishwa Julai 8, 2026 na viongozi wa kanda zao kwa tuhuma za kukiuka kanuni za maadili ya viongozi, baada ya kutoa matamko kupitia vyombo vya habari dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, John Heche, bila kufuata utaratibu wa chama.

Kwa mujibu wa barua za tuhuma walizopewa kwa nyakati tofauti, mamlaka za uteuzi zinadai kuwa walitoa tuhuma zisizo na uthibitisho dhidi ya Heche na kuzisambaza kupitia vyombo vya habari kwa lengo la kumchafua na kushusha heshima yake, badala ya kuziwasilisha katika vikao halali vya chama.

Mwananchi limemtafuta Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambaye amethibitisha kupokea barua hiyo ya pamoja na kusema tayari imeanza kufanyiwa kazi.

"Ni kweli wamefikisha barua yao leo asubuhi. Tumeipokea na tunaifanyia kazi. Baada ya kuipitia tutatoa majibu kwa wahusika," amesema Nyahoza.

Hata hivyo, viongozi wa Chadema wamepinga malalamiko hayo wakidai hayana msingi, wakisisitiza kuwa watuhumiwa walishapewa barua za kuwataka wajieleze ndani ya siku 14 kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya, amesema hana taarifa iwapo viongozi wote wawili wa kanda yake waliwasilisha malalamiko kwa Msajili, lakini amesisitiza kuwa taratibu za chama zilifuatwa kikamilifu.

"Utaratibu wa chama unamtaka kila kiongozi au mwanachama anayetuhumiwa apewe barua ya siku 14 ya kujieleza. Barua hizo hutumwa pia kupitia WhatsApp, ambao ni mfumo rasmi unaotambuliwa na chama chetu," amesema Kaunya.

Amesema viongozi hao walitumiwa barua hizo kupitia mfumo huo na zilionyesha kuwa zilisomwa, kabla ya hatua ya kuzifikisha pia kwenye makazi yao.

"Baada ya kumfikishia barua kwa njia hiyo, hatua inayofuata ni kuipeleka nyumbani kwake. Inawezekana baadhi ya barua bado hazijafika kwenye makazi yao, lakini taarifa ya awali waliipokea," amesema.

Kaunya amesema hatua ya viongozi hao kukimbilia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kabla ya kukamilisha taratibu za ndani za chama inaonesha kutotaka kuheshimu katiba na kanuni za chama.

"Katiba yetu inaelekeza kwamba mtuhumiwa apewe siku 14 za kujieleza. Akijibu, vikao vya kinidhamu hukaa na kujadili maelezo yake kabla ya kufanya uamuzi wa kumrejesha au kumchukulia hatua nyingine. Hadi sasa hakuna aliyewasilisha maelezo yake licha ya kupewa nafasi hiyo," amesema.

Amesema iwapo watashindwa kujieleza ndani ya muda uliowekwa, wataandikiwa tena barua nyingine ya siku 14, na baada ya hapo vikao vya kinidhamu vitafanya uamuzi wa mwisho.

"Tunachokifanya ni kutekeleza Katiba na kanuni za chama. Hata kama kuna tuhuma nzito dhidi ya kiongozi, si sahihi kuzitangaza kupitia mitandao ya kijamii au vyombo vya habari badala ya kutumia mifumo rasmi ya chama," amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Ashura Masoud, amesema Katibu wa Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okolo, alipokea barua ya kutakiwa kujieleza ndani ya siku 14 na baadaye aliwasilisha rufaa ngazi ya taifa akidai hakutendewa haki.

"Kwa mujibu wa taratibu za chama, rufaa hiyo inapaswa kushughulikiwa ndani ya siku 14 na muda huo bado haujaisha. Hivyo, hatua ya kupeleka malalamiko kwa Msajili inaleta maswali kwa kuwa tayari alikuwa ameanza kutumia utaratibu wa ndani wa chama," amesema.