Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vuta nikuvute uongozi ndani NCCR Mageuzi

Muktasari:

  • Hali hii inaashiria kuendelea kwa mzozo ndani ya chama hicho ni jambo linaloweza kuathiri ushiriki wake katika uchaguzi mkuu.

Dar es Salaam. Mvutano ndani ya chama cha NCCR Mageuzi unaendelea kuchukua sura mpya huku uongozi wa chama hicho ukianza maandalizi ya kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Hii ni baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kueleza kuutambua uongozi wa mwenyekiti mpya, Haji Ambar Khamis kuwa halali.

Katika mazungumzo na Mwananchi Julai 11, 2025, aliyekuwa kiongozi wa Baraza la Vijana wa chama hicho, ambaye alivuliwa uongozi pamoja na James Mbatia, Nicholas Jovin amesema baada ya kukumbana na vizuizi kurejea ofisini, sasa viongozi hao wanajipanga kwa njia zingine.

“Wiki iliyopita tulikwenda ofisini kama ambavyo Mahakama ilitoa hukumu katika shauri letu, lakini tulizuiwa na baadaye Mbatia akaandikiwa barua na Msajili wa vyama vya siasa kuwa hamtambui kuwa kiongozi wa chama, hivyo asiingie ofisini.

“Baada ya hatua hiyo, kwa sasa tunafanya mashauriano na wadau wakiwemo mawakili wa chama ili kuona namna gani tunafanya ili kuondokana na kikwazo hiki,” amesema mfuasi huyo wa Mbatia.

Ameodokeza kuwa upande wao hauridhishwi na namna Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inavyoshughulikia suala hilo, akidai kuwa wanaona akiegemea upande mmoja licha ya Mahakama kuamua kwa haki shauri lao.

“Tunasikitishwa na msimamo wa Msajili wa Vyama ambao unaonekana kuwa na chuki binafsi dhidi ya Mbatia na hivyo kuwa na msimamo unaoegemea upande mmoja katika mgogoro huu, ni vyema uamuzi wa Mahakama ukaheshimiwa ili kumaliza mzozo huu,” ameongeza.

Julai 9, 2025, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alikiri kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilimwandikia barua Mbatia kufuatia mgogoro uliohusisha uongozi kutoka pande zote mbili kudai kuwa na uhalali wa kuwa ofisini.

Nyahoza aliweka wazi kuwa Ofisi ya Msajiri inautambua uongozi uliopo sasa kwa kuwa ndio uliopatikana kisheria na kwamba uongozi wa Mbatia na wenzake ulikoma muda wake kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa ndani ya ofisi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Evaline Munisi amesema kuwa hali ya chama ofisini imetulia na chama kinaendelea kujipanga kushiriki uchaguzi mkuu.

Hali hii inaashiria kuendelea kwa mgogoro ndani ya chama hicho ni jambo linaloweza kuathiri ushiriki wake katika uchaguzi mkuu.

Mbatia aliondoka madarakani tangu mwaka 2022 kufuatia mgogoro ndani ya chama uliosababisha yeye na viongozi wenzake kusimamishwa na baadaye kuvuliwa uongozi na kamati kuu ya chama chao.

Kufuatia kuondolewa kwao, chama kilichagua uongozi mpya ambapo Khamis alichukua nafasi ya Mbatia kama mwenyekiti wa chama hicho na Munisi akiteuliwa kuwa katibu mkuu wa chama pamoja na viongozi wengine.

Mpaka sasa, uongozi huo unashikilia ofisi licha ya upande wa Mbatia kukimbilia mahakamani na Mahakama kutolea uamuzi wa kuwatambua kama viongozi halali, jambo ambalo linaendeleza mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama hicho.