Wachache wajitokeza kupiga kura, amani yatawala

Baadhi ya Wananchi wakiangalia majina yao kwenye ubao katika kituo cha kupigia kura cha Kwa Wazee Jimbo la Amani. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

Wakati shughuli ya uchaguzi mdogo ikiendelea huku hali ya amani ikiwa imetanda katika Jimbo la Amani Zanzibar, imeshuhudiwa idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wengi wao wakiwa ni wanawake.

Unguja. Wakati shughuli ya uchaguzi mdogo ikiendelea huku hali ya amani ikiwa imetanda katika Jimbo la Amani Zanzibar, imeshuhudiwa idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wengi wao wakiwa ni wanawake.


Uchaguzi wa jimbo hilo unafanyika leo Jumamosi Desemba 2022 kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mussa Hassan Mussa kilichotokea Alhamis Oktoba 13, 2022 kisiwani humo.


Mwananchi imezunguka vituo kadhaa vya kupigia kura na kushuhudi kukiwa na utulivu huku wananchi wakiendelea kupiga kura.

“Mimi nimejitokeza kupiga kura kwasababu ni haki yangu na nimekuja kumchagua ninayemtaka, tayari nimeshapiga kura kwahiyo nasubiri matokeo yatakapotangazwa,” amesema mzee Mangama Makame


Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mfaume Mfaume mkazi wa Kilimahewa, amesema “uchaguzi ni wa haki na huru lakini watu hawajitokezi kwasababu ya mazoea kwamba atakayetangazwa ndiye mshindi hata kama hakushinda.”

Wananchi wakihakikiwa majina yao katika kituo cha kupiga kura Kilimahewa Jimbo la Amani. Picha na Jesse Mikofu

Wakati akisema hayo, Rahma Said Soud amesema, wananchi hawajitokezi hususani vijana kwasababu pengine wanaona hakutakuwa na haki hivyo bora wasipoteze muda badala yake waendelee na shughuli zao za kujiingizia kipato.


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Jacobs Mwambegele amesema hali ni shwari katika vituo alivyozungukia na hajapokea malalamiko yoyote.


“Nimeshuhuduia ufunguzi pia nitaangalia kwenye kufunga, ikifika saa 10:00 jioni vituo vitafungwa na hatarusiwa mtu yeyote kuingia ndani ya kituo,” amesema


Kuhusu idadi ndogo ya wapiga kura, Jaji Mwambegele amesema “watu wamejitokeza na wanaendelea kujitokeza kadiri waanvyoweza.”