Wananchi walinda kura uchaguzi mdogo Kenya, chama tawala chabwagwa
Muktasari:
- Kwa wachambuzi wa siasa, uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ulikuwa kipimo cha nguvu za kisiasa kati ya Rais William Ruto na Rigathi Gachagua, maarufu Riggy G, huku ushindi wa DCP ukionekana kuimarisha ushawishi wa Gachagua katika eneo la Mlima Kenya.
Nairobi. Mamia ya wakazi wa eneo bunge la Ol Kalou walijitokeza kwa wingi kulinda kura zao baada ya kushiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge, huku wengine wakisindikiza msafara wa magari yaliyokuwa yakisafirisha masanduku ya kura kutoka vituo vya kupigia kura hadi kituo cha kujumlishia matokeo.
Hatua hiyo ilikuwa sehemu ya kile walichokiita "Operation Linda Kura", wakisema walitaka kuhakikisha kila kura iliyopigwa inalindwa na kufikishwa salama hadi kuhesabiwa.
Wananchi hao walikesha nje ya vituo vya kupigia kura na baadaye katika vituo vya kujumlishia matokeo, wakifuatilia kwa karibu kila hatua ya mchakato wa uchaguzi.
Wengi wao walieleza kuwa walifanya hivyo ili kuongeza uwazi wa uchaguzi na kujiridhisha kuwa matokeo yaliyotangazwa yanaakisi kura zilizopigwa, huku vyombo vya usalama vikisimamia utaratibu na kuimarisha ulinzi wakati wa usafirishaji wa masanduku ya kura.
Hatua hiyo ilitokea wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Alhamisi, ambapo wananchi walifuata wito wa baadhi ya viongozi wa kisiasa waliowahimiza kupiga kura na kubaki karibu na vituo vya kupigia kura hadi matokeo yatangazwe.
Katika vituo vingi vya kupigia kura, wananchi waliendelea kubaki nje ya vituo hadi usiku, wakisubiri kukamilika kwa zoezi la kuhesabu na kutangaza matokeo.
Kwa upande mwingine, uchaguzi huo mdogo uligeuka kuwa mchuano wa kisiasa kati ya Rais William Ruto wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, maarufu Riggy G, wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP).
Baada ya kuhesabiwa kura zote, mgombea wa chama cha DCP, Sammy Ngotho, alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 35,440, akimshinda kwa tofauti kubwa mgombea wa UDA, Samuel Muchina Nyagah, aliyepata kura 5,450.
Mbali na DCP na UDA, vyama vingine saba pia vilisimamisha wagombea, na kufanya idadi ya wanaowania kiti hicho kufikia tisa.
Hata hivyo, kampeni na mjadala wa kisiasa ulijikita zaidi katika ushindani kati ya DCP na UDA.
Kwa wachambuzi wa siasa, uchaguzi huo ulikuwa zaidi ya kumchagua mbunge mpya.
Ulionekana kama kipimo cha ushawishi wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya kati ya Gachagua, ambaye anaongoza DCP, na Rais Ruto, ambaye ni kiongozi wa UDA.
Matokeo hayo yanatafsiriwa kuwa yameipa DCP ushindi mkubwa katika eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likihesabiwa kuwa ngome ya kisiasa ya UDA.
Wakati huo huo, kwa UDA, matokeo hayo yanachukuliwa kuwa mtihani muhimu kuhusu kiwango cha uungwaji mkono wa chama hicho katika eneo la Mlima Kenya baada ya mabadiliko ya kisiasa yaliyoshuhudiwa katika siku za karibuni.
Licha ya uchaguzi kuanza kwa utulivu asubuhi, baadaye ulitawaliwa na matukio ya mvutano, madai ya vitisho kwa wapiga kura, vurugu katika baadhi ya maeneo, pamoja na lawama za kisiasa zilizozua wasiwasi kuhusu uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.
Maofisa wa polisi walijaribu kuwatawanya wananchi waliokuwa wamekusanyika nje ya vituo vya kupigia kura, wakieleza kuwa walikuwa wakikiuka utaratibu wa uchaguzi.
Hata hivyo, wananchi wengi walisisitiza kuwa walikuwa na haki ya kufuatilia mchakato wa uchaguzi kwa karibu kutokana na kutokuwa na imani ya kutosha na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Pamoja na hali hiyo, shughuli za upigaji kura ziliendelea chini ya usimamizi wa maofisa wa IEBC, mawakala wa vyama vya siasa na waangalizi wa uchaguzi waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa zoezi hilo katika vituo mbalimbali.
Takwimu za IEBC zinaonyesha kuwa kati ya wapiga kura 73,480 waliojiandikisha katika eneo bunge hilo, takribani asilimia 57 walijitokeza kupiga kura. Idadi hiyo imeelezwa kuwa ni kubwa ikilinganishwa na viwango vinavyozoeleka katika chaguzi ndogo nchini.
Ushiriki huo mkubwa ulitafsiriwa na wachambuzi wa siasa kuwa ishara ya hamasa kubwa ya wananchi katika uchaguzi uliolenga kuziba nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Ol Kalou, David Kiaraho.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.