Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira: Wanaotaka tuahirishe uchaguzi waahirishe mambo yao wenyewe

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Stephen Wasira akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Songea katika ofisi ya chama hicho mkoa

Muktasari:

  • Leo Jumatatu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewasili mkoani Ruvuma kuanza ziara ya siku nne

Songea. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema wanaotaka uchaguzi mkuu Oktoba 2025 uahirishwe, waahirishe mambo yao wenyewe.

Wasira amesema tayari CCM imeshajipanga kwa uchaguzi mkuu kwa kuwateua wawakilishi wa nafasi ya urais na makamu wa Rais ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Emmanuel Nchimbi.

Rais Samia na Dk Nchimbi wanasubiri kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa wagombea urais.

Licha ya Wasira kutotaja kwa jina wanaosema uahirishwe uchaguzi huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndiyo chama kinachoendesha kampeni ya No reforms no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ maeneo mbalimbali nchini.

Chadema inafanya mikutano ya hadhara sasa wapo kanda ya kati ya Morogoro, Dodoma na Singida wakielimisha wananchi juu ya kampeni hiyo wakisema hawatashiriki uchaguzi huo hadi mabadiliko yafanyike huku wakitaka uchaguzi huo uahirishwe.

Leo Jumatatu, Juni 9, 2025, Wasira amewasili mkoani Ruvuma kuanza ziara ya ujenzi wa chama.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Songea katika ofisi za CCM amesema ni ngumu kuahirisha uchaguzi.

"Wapo rafiki zangu wa 'Tone Tone' wanapita wanawaambia wananchi tusifanye uchaguzi, mimi nawauliza tusipofanya wananchi waongozwe na nani,” amehoji Wasira.

“Wanasema tuahirishe uchaguzi, hatuahirishi ng’o, aahirishe mambo yako mwenyewe sisi tayari tumeshaweka wagombea."

Hata hivyo, kuna mambo yanayoweza kusababisha uchaguzi mkuu nafasi ya Rais kuahirishwa, moja ni kupitia sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya 2024 na pili ni kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Kifungu cha 40 cha Sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 inasema endapo mgombea urais au makamu wa Rais atafariki, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), itateua siku nyingine ya uteuzi si zaidi ya siku 14 tangu kifo kitokee.

Hii ni kutoa muda kwa chama cha siasa, kuteua mgombea mwingine na INEC itapanga siku nyingine ya uchaguzi wa nafasi ya urais na taratibu husika zitaanza upya isipokuwa hakutakuwa na uteuzi mpya kwa wagombea wengine wa kiti cha Rais kama wapo.

Mwaka 2005, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 30 uliahirishwa baada ya mgombea mwenza wa Chadema, Jumbe Rajabu Jumbe kufariki Oktoba 26, na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikapanga uchaguzi kufanyika Desemba 18,2005.

Sababu ya pili ni Ibara ya 44(1) ya Katiba, baada ya  Rais kutangaza kuwapo kwa vita kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi yoyote kwa sababu nchi inapokuwa inapigana na nchi nyingine, shughuli za kisiasa husimama kwa muda. Hivyo uchaguzi unaweza kuahirishwa.

'Tone tone' ni kampeni maalumu ya Chadema inayolenga kuhamasisha Watanzania kukichangia fedha chaka hicho kuwezesha shughuli mbalimbali za chama hicho.

Mkoa huo wa Ruvuma unakuwa wa 12 kwa kiongozi huyo kutembelea tangu ashike nafasi ya umakamu mwenyekiti wa CCM Bara Januari 2025.

Katika mikoa yote aliyotembelea Wasira amesema chama hicho bado kipo imara na kinamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na utendaji wake.

Awali, akimkaribisha Wasira, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho amesema mkoa huo upo salama na umejiandaa na uchaguzi mkuu.

Wasira atakuwa mkoani Ruvuma kwa siku nne kuanzia leo Jumatatu baadaye kuelekea mkoani Mwanza kwa siku nne na kuhitimisha ziara yake mkoani Geita Juni 23, 2025.