Ziara ya ACT Wazalendo na mkakati wa ushindi wa chaguzi, wasomi watoa neno
Dar es Salaam. Ni mkakati. Ndivyo unavyoweza kusema ukizungumzia ziara ya siku 21 ya viongozi wakuu wa chama cha ACT- Wazalendo kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Ziara hiyo iliyoingia siku ya nane leo Jumatano Septemba 18, 2024 imejikita pia kuhakikisha chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar kinavuna wanachama milioni 10, kunadi sera zake, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika maeneo husika.
Katika ziara hiyo yupo Dorothy Semu (Kiongozi wa Chama), Isihaka Mchinjita (makamu mwenyekiti bara), Ado Shaibu (katibu mkuu) na Zitto Kabwe ambaye ni kiongozi mstaafu wa chama hicho. Viongozi hao watatembelea mikoa 22.
Mikoa wanayoitembelea ni Ruvuma, Iringa, Mbeya, Njombe, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam Pwani, Morogoro, Songwe, Tanga, Simiyu, Geita, Mara na Kagera, ziara hiyo ni utekelezaji wa maazimio ya halmashauri kuu ya chama hicho iliyowataka viongozi wakuu kufanya hivyo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika ziara hiyo, viongozi hao wanatumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Watanzania kujitokeza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ili kuchagua viongozi wa vyama mbadala, kikiwemo chama hicho.
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamekuwa wakiwaleeza na kuwashawishi wananchi katika maeneo waliopita kwamba ACT- Wazalendo ndiyo chama mbadala, hivyo wakiunge mkono kwa kukipigia kura kwa wingi ifikapo Novemba 27, 2024 na mwakani 2025 katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Ziara hiyo imejikita kuhakikisha hakuna kijiji, mtaa wala kitongoji uchaguzi huo unafanyika bila ACT- Wazalendo kusimamisha wagombea wake.
Kwa mujibu wa ACT- Wazalendo, jumla ya wanachama 418,000 wameandaliwa kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ambao juzi Serikali ilitangaza mipaka yake.
Pia viongozi hao wataendesha shughuli ya kuwasajili wanachama wapya kwa njia ya kidijitali, ikiwa sehemu kutekeleza mpango wa kampeni ya chama hicho wa kupata makada wapya milioni 10 ifikapo Mei 2025.
Ziara hiyo ni ya awamu ya pili baada ya kwanza kufanyika kati ya Julai 22 hadi Agosti 17 ikihusisha majimbo 125 yaliyopo katika mikoa 22.
Katika ziara hiyo, viongozi hao wamekuwa wakikemea utekaji, kuitaka Serikali kukomesha vitendo vinavyochafua taswira ya Taifa. Pia viongozi hao wanakumbana na kero mbalimbali wanazoelezwa wananchi katika maeneo wanayoyatembelea wakitaka zipatiwe ufumbuzi au kufikishwa katika mamlaka za utatuzi.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Richard Mbunda amesema:"Shughuli za kisiasa kama hizi zinaashiria chama cha ACT- Wazalendo kipo hai, tofauti na vyama vinavyosubiri uchaguzi.
“Huu ni muda wa vyama vya upinzani kuonyesha upungufu wa chama tawala katika utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ambayo wananchi waliichagua 2020," amesema Dk Mbunda ambaye ni mhadhiri wa siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mchambuzi mwingine, Profesa Ambrose Kessy amesema ni jambo jema kwa chama chochote cha siasa kufanya ziara na lengo kubwa wa viongozi wakuu wa kitaifa ni kurudi kwa wananchi kueleza ilani zao, ili Watanzania kuielewa.
"Sio kwa chama hiki pekee bali vyama vyote vinapaswa kushuka kwa wananchi, kwa sababu pamoja na kwenda huko, wanatoa elimu ya mpigakura kwa mwananchi na kuwajengea uelewa utakaowasaidia, " amesema Profesa Kessy ambaye ni mhadhiri wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania).
Yaliyojiri siku sita za ziara
Miongoni mwa mambo yaliyoriji katika siku sita ya ziara ya viongozi hao ni pamoja kutaka hatua zichukuliwe kuhusu matukio ya utekaji, utesaji na mauaji ya raia, kutofungamanishwa kwa sekta ya uchimbaji wa chuma na ukuaji wa viwanda na ajira.
Mengine ni kudaiwa kukithiri kwa migogoro ya ardhi nchini, mageuzi ya demokrasia kuporomoka kwa bei za mazao na kadhia ya stakabadhi ghalani na huduma mbovu za afya na elimu.
Akiwa mkoani Njombe, Zitto anasema bado wananchi wamekuwa na kilio kuhusu mbolea ya ruzuku, wakisema hawaipata kwa wakati, hata ikitokea kupatikana inakuwa kwa shida.
"Mbolea bado changamoto, lakini tunawaambia mambo haya tunaendelea kuyapigia kelele kama mnavyojua chama chetu kimekuwa mstari wa mbele tangu 2022, tukilipigania suala hili.
“Tangu kuundwa kwa baraza la mawaziri kivuli la chama hiki, waziri wetu kivuli wa kilimo na umwagiliaji, Abdallah Mtutura amekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wakulima,” amesema Zitto.
Hata hivyo, Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, amesema kampuni ya Taifa ya mbolea ndiyo suluhisho la kuhakikisha pembejeo hiyo inafika kwa wakati wa wakulima, akiitaka Serikali kuiongeza uwezo zaidi ikiwemo fedha.
“Jambo kubwa la mbolea huwezi kuliacha kwa sekta binafsi pekee, bali na umma kupitia kampuni ya Taifa ya mbolea kushindana katika soko, mara kadhaa nimeimbia Serikali suala hili,”amesema Zitto.
Zitto ametumia fursa hiyo, kuzipongeza sekta binafsi kwa kuleta mbolea nchini wakati huu ambao kampuni ya Taifa ya mbolea ipo nchini, akisisitiza Serikali kutoa ushirikiano kwa kampuni hizo, ikiwemo kuwalipa kwa wakati.
Katika hatua hiyo, Zitto ameishauri Serikali kujenga kiwanda cha kuchenjua vyuma wilayani Ludewa, badala ya Makambako kunakokusudiwa kudaiwa kujengwa kwa mchakato huo ambao malighafi zake zitatoka katika mradi wa Liganga na Mchuchuma.
“Hoja ya ACT kila kitu kifanyike wilayani Ludewa ili kuendana na sera ya Serikali ya ujenzi wa reli ya Mtwara- Mbamba Bay hadi Ludewa, ukipeleka kiwanda Makambako maana yake bidhaa zitasafirishwa kwa kutumia reli ya Tazara kupelekwa bandari ya Dar es Salaam badala ya Mtwara,” amesema Zitto.
Pia, Zitto, ameitaka Serikali kuimarisha demokrasia akiwamwagia sifa baadhi ya viongozi walioasisi suala hilo, akiwemo Bob Makani, Freeman Mbowe (mwenyekiti wa Chadema) na Msafiri Mtemelwa.
Kuhusu vitendo vya utekaji, Mchinjita amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura kujiuzulu nyadhifa zao, akidai wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kulinda usalama wa raia.
Shinikizo hilo linatokana na kifo cha mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao aliyedaiwa kutekwa katika basi la Tashriff Septemba 6,2024 na watu wasiojulikana, eneo la Tegeta Complex Kibo akiwa safarini kuelekea Tanga, kisha mwili wake kuonekana siku inayofuata maeneo ya Ununio.
Semu akiwa Tanga
Semu ambaye yupo mkoani Tanga amesema amekuwa akipokea malalamiko kuhusu upatikanaji wa fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf), akisema bado mwenendo wake huaridhishi akiitaka Serikali kulishughulikia suala hilo.
“Hiki kimekuwa kilio kila tunapopita wananchi wanalalamika kuhusu Tasaf, nimeambiwa hata hapa Lushoto kuna shida hiyo, tunaikumbusha Serikali kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wananufaika na mpango huu,” amesema Semu.
Kwa upande wake, Ado aliyekuwa katika mikoa ya kusini na Pwani amesema chama hicho kitakuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wananchi wa mikoa hasa katika kilimo cha korosho, mbaazi na ufuta na migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara.
“Tutakula sahani moja na watu wanaowanyonya katika zao la korosho na ufuta, tumeamua kujitoa kusimamia hili, kikubwa tunaomba mtupe taarifa za wahusika hao ili tuzifikishe kwenye mamlaka husika,” amesema.