Zitto ataka kampuni za mbolea zilipwe madeni, Serikali yajibu
Muktasari:
- Zitto amesema katika ziara yake mkoani Njombe, Iringa na Ruvuma alipokea malalamiko kutoka kwa wakulima wakihofia kuhusu upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakati
Dar es Salaam. Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kulipa mabilioni ya fedha akidai inadaiwa na baadhi ya kampuni zinazosambaza mbolea ya ruzuku, ili wakulima wapate pembejeo hiyo kwa wakati.
Zitto amesema akiwa ziarani kwenye mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma alipokea malalamiko kutoka kwa wakulima wanaohofia kuhusu upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakati kutokana na madeni.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema, “hakuna shida ya mbolea kwa sababu bidhaa hiyo ipo, wasichanganye mikataba kati ya Serikali, waingizaji wa mbolea na uwepo wa mbolea ni vitu viwili tofauti.
"Watu wanahitaji mbolea na mbolea ipo. Waingizaji wote wanaendelea kuingiza kama kawaida," amesema Mweli.
Zitto akizungumza leo Jumanne Septemba 17, 2024 na juzi Septemba 15, akiwa ziarani amesema amekuwa akipata kilio kutoka kwa wananchi wanaodai kumekuwa na shida ya upatikanaji wa mbolea ya ruzuku.
"Haya mambo tumekuwa tukiyaeleza tangu mwaka 2022, tumekuwa tukipigania Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuongezewa mtaji wa fedha ili kushindana na sekta binafsi, hili ndilo jambo kubwa la kuhakikisha pembejeo hii inafika kwa wakati kwa wakulima kwa sababu kutakuwa na ushindani.”
"Lazima kuwepo na ushindani, jambo la mbolea haliwezi kuachwa kwa sekta binafsi pekee bali sekta binafsi na umma zishindane katika soko," amesema Zitto.
Zitto amesema watu wa sekta binafsi wamejitahidi kuleta mbolea hivyo ni vyema Serikali ikatimiza wajibu wake wa kulipa madeni inayodaiwa na kampuni zinazotoa mbolea ya ruzuku.
"Wanaidai Serikali kiasi kwamba kampuni zinalazimika kula mitaji yao, wakila watashindwa kuleta mbolea kwa wakati, niwaambie Bashe na Waziri wa Fedha (Dk Mwigulu Nchemba), walipeni fedha zao ili walete mbolea," amesema Zitto.
Zitto amesema chama hicho, hakitaki kuona wakulima wanapata mbolea ikiwemo ya kukuzia wakati mazao yakiwa yameshastawi au kuwa makubwa.
"Tunaitaka Serikali ihakikishe inalipa madeni ili msimu huu tusichelewe kupata mbolea kwa sababu ya kuchelewa kulipa madeni," amedai Zitto.