Uwanja wa ndege Pemba sasa saa 24

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein     

Muktasari:

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Juma Akil alisema kukamilika kwa mradi huo kunadhihirisha kipimo cha ufanisi wa Mamlaka wa Viwanja vya Ndege Zanzibar ambayo ilianzishwa miaka mitano iliyopita.     

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kukamilika kwa mradi wa uwekaji taa zitakazowesha ndege kutua wakati wote katika Uwanja wa Ndege Pemba ni kielelezo cha hatua za Serikali kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo jana, katika uwanja huo uliopo nje kidogo ya Mji wa Chakechake, Dk Shein alisema lengo ni kuhakikisha unafikia kiwango cha kimataifa.

Alisema baada ya uwekaji wa taa, kinachofuata ni ujenzi wa jengo jipya la abiria na kuongeza urefu wa njia ya kurukia na kutua ndege kutoka kilomita 1.5 za sasa hadi 2.5.

Alisema utekelezaji wa kazi hizo utaanza karibuni kwa kuwa Serikali iko katika hatua nzuri ya mazungumzo na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kugharimia ujenzi huo.

Alisema kwamba, uwapo wa taa hizo sasa utawezesha wasafiri hasa watalii kupanga safari zao wapendavyo.

Awali, Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu alitoa wito kwa wananchi kuthamini jitihada za Serikali pamoja na kulinda miundombinu ya uwanja huo. Alisema Serikali inaimarisha uwanja huo ili huduma zote muhimu zipatikane kwa ajili ya maendeleo.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Juma Akil alisema kukamilika kwa mradi huo kunadhihirisha kipimo cha ufanisi wa Mamlaka wa Viwanja vya Ndege Zanzibar ambayo ilianzishwa miaka mitano iliyopita.