Mahakama ni muhimu sana katika uchumi wa viwanda

Mahakama ni moja ya mihimili mitatu ya dola baada ya Serikali na Bunge ikiwa na jukumu la kutafsiri sheria za nchi ambazo hutungwa na Bunge wakati Serikali ikiwa na jukumu la kutekeleza na kuzisimamia sheria hizo na kutoa haki kwa wananchi wote.

Kwa mujibu wa Katiba, mahakama ndiyo yenye mamlaka na kauli ya mwisho ya utoaji haki nchini. Katika mfumo wa kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria.

Katika kutoa haki, mahakama zinapaswa kufuata kanuni mbalimbali ambazo ni kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi, kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi, kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine.

Kwa mujibu wa sheria, mahakama ina jukumu la kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro na kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.

Kwa upande mwingine, Katiba bado inaweka kanuni muhimu katika utoaji haki ambayo ni kanuni ya uhuru wa mahakama kwamba katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zinapaswa kuwa huru na kuzingatia masharti ya Katiba na ya sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Katiba na sheria nyinginezo, mfumo wa mahakama nchini unaanzia kwenye Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufaa.

Mahakama Kuu imegawanyika katika vitengo mbalimbali kikiwamo cha biashara, uhujumu uchumi, ardhi, usuluhishi na kazi. Upande wa Zanzibar mfumo huo hautofautiani sana na wa bara pamoja na uwapo wa Mahakama ya Kadhi.

Maendeleo ya nchi yoyote ile hasa uchumi wa viwanda, pamoja na mambo mengine, hutegemea uimara na uthabiti wa mahakama katika kutoa tafsiri madhubuti ya sheria na kutoa haki pasipo kuathiriwa au kuingiliwa kwa namna yoyote ile.

Mara nyingi, kutokana na ushindani wa kibiashara unaojitokeza katika sekta mbalimbali za uchumi, huwa kunakuwa na migogoro ya hapa na pale inayohitaji kushughulikiwa ili uzalishaji na huduma ziendelee kama kawaida.

Mojawapo ya changamoto za utoaji haki kwa mahakama ni maslahi ya Serikali katika jambo husika, kuingiliwa na Serikali au Bunge katika kuamua kesi, uelewa mdogo wa sheria kwa wananchi na mazingira ya rushwa.

Changamoto nyingine ni upungufu au udhaifu katika matumizi ya teknolojia, upungufu wa rasilimaliwatu, miundombinu mibovu na masilahi madogo kwa watumishi.

Ili nchi iwe na uchumi imara lazima mfumo wake wa utoaji haki uwe imara na madhubuti kweli kweli. Lazima wananchi wawe na imani na taasisi hii muhimu ili waweze kuitumia kutafuta haki.

Hautakiwi kuwa mfumo unaoyumbishwa na siasa au masilahi binafsi ya watu wachache. Pesa hazipaswi kuwa mwamuzi wa haki za wananchi bali sheria, maana kila mtu yupo chini ya sheria. Endapo sababu nyingine zozote zitatumika kuamua haki, wapo watakaoikosa kwa sababu kila biashara inaangalia faida.

Hivyo basi ni wajibu wa kila mwananchi kuitambua na kuitumia ipasavyo taasisi hii muhimu. Mahakama si adui wa haki bali chombo cha utoaji haki. Milango ya mahakama ipo wazi ili kila mtu aweze kwenda na kupata haki. Tambua tatizo lako, omba ushauri chukua hatua.

Mgogoro wowote wa kiuchumi ambao wahusika wameshindwa kupata suluhu iwe kwenye mikataba, biashara, miradi au jambo lolote lile ni muhimu kuchukua hatua ili haki itendeke kwa pande zote mbili.

Usikubali kuonewa wala kudhulumiwa wakati mahakama ipo ili kutetea na kulinda haki zako. Hili ni suala unalotakiwa kulikumbuka wakati wote.

Lakini, wakati hamasa hii ikiongezeka huku wananchi wakijipanga kushiriki vilivyo kujenga uchumi wa viwanda, mahakama imara inahitajika ili itende haki pale itakapohitajika.

Hii ni kuanzia kwa wananchi au kampuni za ndani hata za kimataifa zitakazokuwa ama zinatekeleza kandarasi za aina tofauti au wawekezaji watakaoleta mtaji wao ili kusaidia kuzalisha huduma na bidhaa za aina tofauti.

Kadri uchumi unavyokuwa ndivyo mikataba ya kibiashara inavyoongezeka na changamoto iliyopo ni ukiukwaji wa utekelezaji. Hili na changamoto nyingine zilizopo zinahitaji mahakama kuingilia kati vinginevyo, uchumi utaanguka.]

Mwandishi ni wakili. Anapatikana kwa namba 0755 545 600.