‘Pre-form one’ ibaki kuwa hiari kwa mtoto

Kumeibuka mashariti mapya kwa baadhi ya shule binafsi za sekondari yanayolazimisha mtoto anayefaulu usaili wa kujiunga na shule zao, lazima asome ‘pre-form one’ kuanzia Oktoba hadi Januari akiishi kwenye bweni la shule.
Baadhi ya shule zimeanzisha na sare kwa kipindi hicho kifupi na atakapoanza kidato cha kwanza atatakiwa kuwa na sare zingine za shule, mbali na hivyo kuna ada na gharama zingine.
Pia, baadhi ya shule zimeweka masharti mtoto anaposhindwa kufanya vizuri kwenye ‘pre-form one’ haendelei kidato cha kwanza hata kama alifaulu usaili.
Hali hii inawaumiza wazazi wengi kwa sababu mtoto akiachwa kwa kushindwa kufanya vizuri kwenye ‘pre-form one’ shule nyingi zinakuwa zimefunga usajili wa wanafunzi wapya na mtoto anakosa kuendelea na masomo ya sekondari.
Suala la kumpeleka mtoto ‘pre-form one’ mara baada ya kumaliza darasa la saba ni suala linalohitaji mjadala wa kina.
Ingawa linaweza kusaidia baadhi ya watoto kujiandaa kwa sekondari, si lazima liwe suluhisho kwa kila mtoto.
Wazazi wanapaswa kupima uwezo na mahitaji ya mtoto kabla ya kumpeleka, na shule zisitumie mpango huu kama njia ya kujiongezea mapato kwa kulazimisha watoto kushiriki.
‘Pre-form one’ inapaswa kuwa hiari, ili kumpa mtoto nafasi ya kupumzika na kuanza sekondari akiwa na nguvu na motisha ya kutosha.
Wakati baadhi ya watu wanaona kuwa ni njia ya kumwandaa mtoto vizuri kwa masomo ya sekondari, wengine wanahisi kuwa ni mzigo kwa watoto na mzazi, hasa kutokana na uchovu wa akili wa mtoto na gharama za ziada.
Katika muktadha huu, kuna swali la kujiuliza, je, ni kweli wazazi wanakwepa majukumu yao ya kumpa mtoto muda wa kupumzika, au ni shule binafsi zinazolazimisha ili kujiongezea mapato?
Kuna mtazamo kwamba baadhi ya wazazi wanatumia ‘pre-form one’ kama njia ya kuepuka jukumu lao la kumtunza mtoto wakati wa mapumziko.
Wazazi wengine huona kuwa mtoto anapoendelea na masomo bila kupumzika, wanaepuka kuwa na mzigo wa kumtafutia shughuli nyumbani au kumtazama.
Kwa mtazamo huu, ‘pre-form one’ inaweza kuonekana kama njia ya kumweka mtoto "bize" na hivyo kumpunguzia mzazi majukumu. Hata hivyo, hii haipaswi kuwa sababu kuu ya kumpeleka mtoto ‘pre-form one.’
Kila mtoto anahitaji mapumziko baada ya kufanya mtihani mkubwa kama wa darasa la saba.
Mchakato wa kujifunza unahitaji utulivu wa akili na nafasi ya kujijenga upya kimwili na kiakili kabla ya kuanza safari mpya ya masomo.
Kuendelea na masomo haraka haraka bila kupumzika kunaweza kumfanya mtoto kuchoka, kushindwa kuelewa vizuri na kupunguza ari ya kujifunza.
Watu wengi wanahoji kuwa ‘pre-form one’ imekuwa ni sehemu ya biashara kwa shule binafsi.
Shule hizi zinatumia mpango huo kama fursa ya kujiongezea mapato kwa kulazimisha wazazi walipe ada za ziada, sare za shule mara mbili.
Mpango huu unawafaidisha shule binafsi kwa sababu huleta mapato kwa kipindi cha likizo.
Badala ya mtoto kuwa nyumbani akipumzika, anashiriki kwenye masomo ambayo huenda yangesubiri hadi mwanzo wa muhula rasmi.
Hili linafanya wazazi kulipa ada za ziada ambazo huongeza gharama ya kumpeleka mtoto sekondari, hivyo kuzifanya shule hizi kujiimarisha kifedha.
Wakati huo huo, kuna dhana kwamba shule binafsi hutumia ‘pre-form one’ kama kigezo cha kumkubali mtoto shuleni.
Watoto wanaohudhuria mpango huu mara nyingi hupewa kipaumbele na wanaweza kukubalika shuleni zaidi ya wale ambao hawakuhudhuria.
Kwa hiyo, ‘pre-form one’ inageuka kuwa "lazima" ili mzazi ahakikishe mtoto wake anapata nafasi ya kusoma katika shule wanayohitaji.
Shule nyingi zinaweza kuweka mazingira ya shinikizo kwa wazazi kwa kigezo cha maandalizi bora ya sekondari, ingawa hili mara nyingi ni la kibiashara zaidi .
Mpango huu unapaswa kubakia kuwa wa hiari kwa watoto na wazazi, bila ya kulazimishwa na mazingira ya kibiashara au shinikizo kutoka kwa shule.
Kwa watoto ambao wana viwango vya juu vya ufahamu na wameonyesha uwezo mzuri kwenye mitihani yao ya darasa la saba, wanaweza kuhitaji muda wa kupumzika badala ya kuendelea na masomo haraka.
Hili litawasaidia kuwa na utayari wa kisaikolojia na kimwili wanapoanza kidato cha kwanza.
Wale wanaohisi wanahitaji maandalizi zaidi wanaweza kushiriki kwenye ‘pre-form one’, lakini lazima kuwe na chaguo badala ya kulazimishwa.
Noor Shija ni mhariri wa Mwananchi mkoani Dodoma. 0788148834