ANTI BETTIE: Mke wangu muongo, mchonganishi hadi anatia kinyaa

Sunday January 17 2021
Aunt bettie pic

Habari Anti, Nina mke ambaye napata mashaka kuendelea kuwa naye kutokana na tabia zake.

Mke wangu ni muongo na anajua kuupamba uongo wake hadi ukafanana na ukweli.

Amekuwa akinitia aibu kutokana na kuchonganisha watu.

Nisaidie nifanye nini?

Hujaniambia kama umezungumza naye ili ajue ni kwa namna gani anakukera kutokana na tabia yake ya uongo.

Kabla hujalalamika kuhusu jambo hilo dawa ni kusema naye mwenyewe na usikie uongo wake, unaweza kugundua ana tatizo mbali ya tabia hiyo mbaya.

Advertisement

Pia unaweza kuwashirikisha wazazi wake, huku ukiwaeleza namna anavyokutia aibu kwa kugombanisha watu kutokana na uongo wake.

Lazima ajue kwanza analolifanya ni kosa kwa kukemewa na wanafamilia yake, kama hajui ataendelea, inawezekana anaona anaonewa.

Hali ikizidi shirikisha viongozi wa dini wamuombe au kumsomea, wakati mwingine haya mambo yanahitaji nguvu ya Mungu. Huu uongo wake ni kama laana, haiwezekani mwanamke ameolewa lakini bado anaidhalilisha familia yake kwa uongo.

Anahitaji nguvu ya ziada kuimaliza tabia hiyo.

Ananipenda kweli?

Nilizaa na mume wangu watoto wawili, baadaye kukatokea tofauti kati yetu tukatengana huu ni mwezi wa 10.

Wiki mbili hizi amekuwa akinipigia simu akitaka turudiane na anasema ananipenda sana.

Je, ananipenda kweli, nifanyeje?

Sijaelewa mke na mume mlitengana tu bila kushirikisha familia, napata ukakasi kidogo. Busara unapotengana na mumeo ni kutoa taarifa kwa wazazi wako na wake ili mkutanishwe kwa ajili ya usuluhishi na ikishindikana wakati huo, familia itahusika wakati huu ambapo mwenzako anafikiria mrudiane.

Kusema anakupenda au la ni vigumu kwa sababu moyo wa mtu msitu na ni ngumu kufahamu anawaza nini moyoni mwake, tofauti na unachofikiria au unaweza kupatia, kwa kifupi ni jibu la kufikirika.

Ushauri wangu kuwa makini na anachokisema mwenza wako kulingana na namna mlivyoachana (wewe ndiyo unajua na utapima), pili hakikisha kabla hamjaingia katika mahusiano mnakwenda kupima afya.

Miezi kumi ni mingi lolote linaweza kutokea kati yenu.

Pia nasisitiza kwa kuweka heshima ya ndoa yenu, shirikisheni pande mbili za familia badala ya kulimaliza kihuni.

Advertisement