Anti Betty: Ukiona dalili hizi jua shoga yako anakuzunguka

Swali: Anti nahisi kuna jambo haliko sawa kati ya mume wangu na mmoja wa rafiki zangu. Kila nikikaa naye hutuma walau dakika mbili kuponda tabia zake na namna anavyochukizwa nazo. Hivi karibuni amefikia hatua ya kutamani nisiwe karibu naye kabisa. Lakini kinachonisumbua ni namna ya kumuepuka kwa sababu ni miongoni mwa mashoga zangu wenye akili na mipango ya maendeleo. Ninaomba unisaidie nifanye nini ili mume wangu aelewe kuwa licha ya kumuona ana tabia mbaya ni shoga wa faida kwangu.

Jibu:

 Haahaaa, acha kwanza nicheke kidogo, nakupa hii ifanyie kazi, kuna baadhi ya tabia ukimuona nazo mumeo linapokuja suala la rafiki zake fanya uchunguzi, kuna jambo halipo sawa.

Kwanza kabisa akiwa na tabia ya kuwaponda au kuwachukia rafiki zako jua kuna shida mahali. Ama anataka kutoka na huyo rafiki yako sasa anataka uwe mbali naye au walikutana mahali hivyo anajua habari zake anajua atakuambia.

Jambo lingine ukiona mawasiliano kati ya mumeo na rafiki yako yamepamba moto ikiwamo kutoana auti bila wewe kujua.

Yaani unastukia mmoja kati yao ameropoka kuwa walikuwa pamoja mahali, umewakuta au umeambiwa na mtu unayemuamini, kisha ukawauliza wakakataa au kukubali kwa namna ya kukudanganya jua mali yako inaelekea kuliwa au unayoyaona ni manyoya.

Pia kuna suala la mawasiliano yasiyokuwa na kikomo.

Kuna vitu vinaonekana vya kawaida kwa marafiki waliozoeana , lakini kimsingi si vya kawaida, ikiwamo mumeo au mpenzi wako kuzoeana kupita kiasi na rafiki yako.

Mawasiliano kati yao yanazidi, ikiwamo kutumiana ujumbe mfupi mara kwa mara, kusalimiana mara nyingi kuliko anavyowasiliana na wewe.

Wakati mwingine anapompigia hataki kuzungumza mbele yako akirudi, usichekelee mdudu wa sikio huyo atakukera tu.

Pia namba ya rafiki yako kuwa kichwani kwa mumeo, yaani akiitaka anaiandika tu bila kuuliza wala kuitafuta. Akipigiwa simu na rafiki yako anaijua namba yake lakini hajisevu kwenye simu. Kwa kawaida wanaume ni ngumu kushika namba za simu kichwani ukilinganisha na wanawake, lakini mumeo au mpenzi wako anaijua ya rafiki yako akiiona inaita anakuambia fulani anapiga.

Pia urafiki kwa shoga yako ukipungua na badala yake anauhamishia kwa shemeji yake kuwa makini.

Wewe ndiyo umewakutanisha iweje ampende yeye na kukupotezea wewe.

Endelea kushangaa atakuja kukulelea wanao. Muweke mbali mumeo na mashostito wako. Huyo rafiki yako anayekandiwa fuatilia vizuri pengine ndiye mtu anayeongoza kuwasiliana naye. Sikuchonganishi, nakung’ata sikio ili uongeze umakini


Swali: Kuna tatizo niliona linashamiri, siyo kwangu tu, bali wanawake wengi wanalipitia Anti. Wenza wetu wakifanya makosa hawataki tuyajadili ili kama wamekosea wakiri kosa na kuomba msamaha.

Mfano mimi hii ni mara ya tano kama siyo ya sita ninamkamata mume wangu akinifanyia vitu vinavyonikera ikiwamo kuwapo dalili za kuwa na mahusiano nje ya ndoa yetu.

Lakini hakubali, tena hataki hata kusikia kuhusu kujadili suala hilo ili nafsi yangu iridhike.

Unajua Anti ninahitaji hata anidanganye ili niwe na amani, lakini hilo halijawahi kufanyika.

Sasa naishi na jazba na kisirani, likitokea jambo dogo hata likifanywa na watoto ninalia, kwa sababu nina maumivu ya kudumu moyoni mwangu.

Naomba useme nao wanatuumiza nafsi zetu.


Jibu: Najua wengi wanajua kuhusu nyufa za ukuta na kusahau kuwa hata kwenye mapenzi na uhusiano kuna nyufa tena kubwa ambazo zisipozibwa ipo siku zitauvunja uhusiano wenyewe kabisa.

Nyufa hizi hutokana na kawaida ya mwanadamu kupishana Kiswahili, lakini hukaa pamoja na kujadili ili kupata muafaka.

Kwa mfano huu wa mwari wangu ni kuwa wanaume mnakimbia vivuli vyenu na ndiyo maana baadhi yenu wanalalamika wake zao wamekuwa jeuri.

Ngoja nishushe sauti tuzungumze kwa kunong’ona wanawake wasitusikie, ni hivi mwanamke wa aina hii akipata mtu anayemsifia tu na kumsikiliza kidogo utakuwa ‘babu jinga inama ufikiri mali yako inaliwa’, hatosita kwenda huko kwa sababu tu humpi nafasi ya kutoa yake ya moyoni.

Mpe mwanamke nafasi, hasa ukizingatia wewe ndiyo wake na tuhuma alizonazo zinakuhusu. Ukiishi na mtu bila shaka unamjua vizuri, hivyo tumia kumjua kwako kumaliza kesi zinazokukabili huku ukijipanga kuacha kufanya mambo ya maudhi.

Kukimbia kesi si kuimaliza, ni kuweka kiporo, ndiyo maana kuna wakati unamuuliza mwenza wako kitu cha kawaida ila kinaleta zogo na ugomvi mkubwa, kumbe kwa sababu ana dukuduku asilokuwa na pa kulitolea. Nawakumbusha shemeji na wakwe zangu, kuweni makini na moyo wa mwanamke, ni ngumu kuujeruhi lakini ukipata jeraha ni ngumu pia kulitibu hadi lipone. Walio wengi wakishapata majeraha ya moyo huwa hawaponi kamwe.

Pia muhimu kuzingatia kutokuwa mtu wa matukio, kwani utajitetea mwisho utamaliza maneno na kuonekana usiyekuwa na maana mbele ya mkeo na wakati mwingine familia kulingana na ukubwa wa mambo unayoyafanya.

Inawezekana kama binadamu kujizuia kukosea likawa jambo gumu, ila kuheshimu familia yako isijue hizo dhambi zako ni suala lililo ndani ya uwezo wako.

Nakukumbusha usijeruhi moyo wa mwanamke, hatokusamehe.