Mbaroni kwa madai ya kumuua mkewe kisa tendo la ndoa

Muktasari:

  • Inadaiwa mtuhumiwa huyo alimpiga mkewe baada ya kumnyima haki ya tendo la ndoa.

Uganda. Agunda James (48) kutoka Nile Magharibi nchini Uganda, amekamatwa na Polisi kutokana na kifo cha mkewe, baada ya kutokea vurugu lililosababishwa na kunyimwa tendo la ndoa.

Inalezwa Chandiru Judith (marehemu) mwenye umri wa miaka 23, ameuawa baada ya kupigwa kutokana na kudaiwa kumnyima tendo la ndoa mumewe huyo, James.

Msemaji wa Polisi, Fred Enanga amesema mauaji hayo yalitokea baada ya kutoelewana wakati Chandiru alipomnyima mumewe haki hiyo ya ndoa.

Tovuti ya Explorer Uganda ya nchini humo imesema uchunguzi wa awali ulibaini kutokuwapo ukaribu wa wanandoa hao, licha ya kulala kitanda kimoja, huku Judith akimshutumu James kwa kuchepuka.

Aidha, tovuti rasmi ya X ya Jeshi la Polisi ya nchini humo imesema ukweli uliokusanywa unaonyesha wanandoa hao wamekuwa wakilala pamoja, lakini hawakuwa wakihusiana kimapenzi.

“Baada ya marehemu kumshutumu mumewe kwa kuwa na uhusiano wa nje (mchepuko), usiku wa Machi mosi, 2024, ulizuka ugomvi, kisha alimwacha mumewe kitandani na kwenda kulala kwenye godoro lingine.

“Akiwa na hasira mumewe alimfuata na kumshika, kisha akampiga mbavuni alianguka chini kwenye sakafu na kufa kutokana na majeraha. Mshukiwa alikwenda ujisalimisha mwenyewe polisi,” imebainisha.

Aidha, Polisi wanasema wameendelea kurekodi matukio ya mauaji kutoka kwa wanandoa kwa sababu ya haki za ndoa na masuala mengine, huku wakishauri kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Ikumbukwe, Desemba mwaka jana, mzee mwenye miaka 110 kutoka Wilaya ya Ntugamo alituhumiwa kumuua mkewe mwenye umri wa miaka 109 kwa kumchoma kisu kwa kumnyima haki ya ndoa.


Imeandaliwa Sute Kamwelwe na Mashirika