Diallo asibezwe, kasema wanachohofia walio wengi

Muktasari:

  • Kwa lugha rahisi, wengine wanaweza kusema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo amepasua jipu!

Kwa lugha rahisi, wengine wanaweza kusema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo amepasua jipu!

Dk Diallo ambaye pia ni mfanyabiashara aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa nchini, ikiwemo uwaziri kafunguka kwa kusema ambacho wengi wanahofia kukisema hadharani.

Akizungumza katika mahojiano ya kipindi cha The Big Agenda kinachorushwa na kituo cha runinga cha Star Tv, Waziri huyo wa zamani wa Mifugo na Uvuvi na Maliasili na Utalii alisema kwa miaka mitano iliyopita, Taifa lilipita katika kipindi cha giza.

Kwa kauli yake, Dk Diallo anayemiliki kampuni ya Sahara Media inayomiliki vyombo kadhaa vya habari alisema baadhi ya mambo ya msingi, ikiwemo utii wa Katiba na utawala wa sheria iliwekwa pembeni huku viongozi wakifanya watakavyo bila hofu.

Katika sekta ya biashara ambayo yeye ni mbobevu, kiongozi huyo wa chama tawala alisema wazi kuwa mambo yalikuwa hayatabiriki, huku nguvu zikitumika kukusanya kodi badala ya maarifa.

Japo wapo baadhi ya watu, wakiwemo viongozi na makada wa CCM wamejitokeza kubeza kauli za Dk Diallo, ukweli utabaki wazi kuwa kama siyo yote, basi hoja na maneno mengi yaliyosemwa na kiongozi huyo yana ukweli utakaoendelea kusimama hata kama wengine watabeza.

Wanaombeza Dk Diallo wanaweza kuwa na hoja; lakini ukweli utaendelea kusimama kwamba Taifa limepita katika kipindi cha giza ambacho kila Mtanzania anatakiwa kumwomba Mungu tusipite tena huko.

Kuna kipindi huko nyuma hakuna mtu aliyekuwa na uhakika wa kesho yake. Siyo wafanyabiashara, wanasiasa, viongozi wa umma wala wananchi wa kawaida.

Katika kipindi hicho ndipo tulishuhudia viongozi na watendaji katika ofisi za umma wakitumbuliwa hadharani majukwaani kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za ajira.

Ni katika kipindi hicho, wafanyabishara walipewa makadirio ya kodi zisizolipika kiasi cha wengine kulazimika kufunga biashara zao.

Kodi ilikusanywa katika mazingra ya vitisho ambapo kikosi kazi kilichoundwa na Maofisa wa Mamlaka ya Kodi (TRA) na vyombo vya ulinzi na usalama kilifunga siyo tu maeneo ya biashara, bali pia akaunti za benki za wanaodaiwa au waliokwepa kodi.

Fedha zilizokuwepo kwenye akaunti zilizofungwa pia hazikubaki salama kwa sababu zilichukuliwa.

Huu ni ukweli ambao hata kama hatuupendi lakini ndivyo ilivyotokea na ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan akawaagiza maofisa wa TRA kutumia busara na hekima kukusanya kodi badala ya mabavu.

Sera na mazingira ya biashara nchini pia haikutabirika kiasi cha baadhi ya wafanyabiashara kuhamishia mitaji yao nje ya nchi, ndiyo maana Rais Samia anafanya jitihada kurejesha imani ya wawekezaji.

Mambo hayakuwa salama hata katika utawala wa sheria ambapo mashauri mengi ya jinai yalifunguliwa, huku watu wakisota mahabusu kwa kipindi kirefu hata kwa kesi zenye dhamana.

Mifano iko mingi, lakini itoshe tu kutaja shauri la aliyekuwa mbunge wa zamani wa Arusha mjini, Godbless Lema, aliyekaa mahabusu ya gereza la Kisongo kwa zaidi ya miezi miwili kwa kesi yenye dhamana.

Wapo Watanzania waliolazimika kukiri makosa na kulipa faini na fidia kupitia utaratibu wa makubaliano na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP), licha ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kwa ushahidi mashtaka dhidi yao mbele ya Mahakama.

Wanaopinga uwepo wa matukio haya wana haki ya kufanya hivyo; lakini huo ndio ukweli na ndiyo maana tumeshuhudia kesi nyingi za jinai zilizowasotesha watu mahabusu kwa muda mrefu zikifutwa ndani ya kipindi cha siku 100 za Rais Samia.

Yawezekana Dk Diallo amekosea kwa kutumia sentensi ya muda uliopita katika uwasilishaji wa hoja zake kama alivyonukuliwa baadaye, lakini ukweli utaendelea kusimama kwamba Taifa lilipita katika giza nene ambalo kila mmoja wetu anawajibika kuhakikisha haturejei huko.

Kuna namna nyingi ya kunusuru Taifa kutorejea gizani; moja ni kuwa na taasisi imara zenye nguvu zitakazohakikisha viongozi wanaopewa dhamana hawafanyi watakavyo, bali wanaoongoza kwa mujibu wa sheria na katiba. Tuwe na Mahakama na Bunge imara.

Tujenge utamaduni wa viongozi kuwajibika na makosa yao badala ya kuwawekea wigo wa kutoshtakiwa.