Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Guantanamo; gereza la kisiasa ghali zaidi duniani

Muktasari:

Ni gereza linaloendeshwa kwa fedha nyingi za walipakodi nchini Marekani.

Mwanzoni mwa mwaka 2002, washukiwa wa mwanzo kabisa wa ugaidi wa kimataifa walipelekwa katika gereza lililojengwa katika Kituo cha Kijeshi cha Kimarekani cha Guantanamo nchini Cuba, kutokana na amri ya Rais George W. Bush.

Rais wa Marekani aliyefuata, Barack Obama, licha ya kuahidi kwamba atalifunga gereza alipoingia madarakani mwaka 2009, jambo hilo halijafanyika hadi sasa. Lakini jela hilo ni mzigo kwa walipa kodi wa Marekani.

George Bush alihisi kwamba Guantanamo, kipande cha ardhi cha eneo la kilomita 120 za mraba, ndipo mahala panapofaa kabisa kuwazuwia wale watu iliowaona kuwa ni wakorofi kabisa na inaowashuku kuwa ni magaidi sugu.

Utawala wa Marekani baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2011, iliwaita watu wa aina hiyo, ‘wapiganaji maadui’,  tofauti na wafungwa walio wahalifu wa kawaida.

Msamiati huo ulitumiwa kama njia ya kuepuka kuwataja watu wa aina hiyo kuwa ni wafungwa wa kivita, ama sivyo wangekuwa na haki zinazotakiwa wapewe kwa mujibu wa sheria na mikataba ya kimataifa.

Januari 20, 2002 washukiwa wa kwanza 20 walipelekwa Guantanamo kutokea Afghanistan na Pakistan, ikiashiria namna Marekani ilivyovinjari kuingia katika kile ilichokiita ‘Vita dhidi ya ugaidi.’ Wafungwa walioko sasa katika jela hiyo wanaishi katika majengo ya kisasa pembezoni mwa kituo hicho cha kijeshi. Kuna madaktari na wauguzi 100 wanaowashughulikia wafungwa 132 walioko hivi sasa, licha ya kulindwa na wanajeshi 2,000.

Walinzi katika jela hilo walisema wamepewa amri wawafanyie “utu” wafungwa na wahakikishe usalama wao, lakini washukiwa hao wa ugaidi, miongoni mwao wako waliozuiliwa sasa kwa zaidi ya miaka kumi, wana hadithi nyingine.

Hivyo ndivyo wanavyosema mawakili wao. Mwaka jana idadi kadhaa kati yao walisusia kula na ilibidi walishwe vyakula kwa nguvu. Wafungwa hao hawaruhusiwi kuzungumza na waandishi wa habari. Pia, kanuni za usalama zinawapiga marufuku walinzi kuzungumza na vyombo vya habari.

Hairuhusiwi kuyapiga picha majengo wanamoishi wafungwa. Hizo ni amri. Hazina mjadala, japokuwa walinzi wanadai hali ya mambo katika gereza hilo ni bora kuliko ilivyo katika magereza ya aina hiyo huko Afghanistan na Iraq.

Guantanamo ni eneo la kuchekesha hapa duniani. Siyo mali ya Marekani  wala siyo ya Cuba, pia ni mali ya nchi zote mbili. Kwa miaka mingi mahala hapo palitumiwa na wanajeshi wa Marekani kutia mafuta na kuzikarabati manuwari zao. 

Mwaka 1903 Rais Tomas Estrada Palma wa Cuba alilikodisha eneo hilo lililoko karibu na bahari kwa Wamarekani. Lakini pale Fidel Castro alipoingia madarakani huko Havana mwaka 1959 mambo yalibadilika.

Japokuwa Marekani hadi sasa inalipa kodi yake ya Dola 4,000 kwa mwaka, lakini watawala wa Cuba hawazipokei fedha hizo kwani kufanya hivyo kutamaanisha wanatambua kukaliwa ardhi yao na Wamarekani, jambo ambalo wanalipinga kabisa.

Kwa wenyewe wanajeshi wa Kimarekani, Guantanamo ni kama pepo. Ni kama mji mdogo wa Marekani unaopendeza. Kuna mkahawa wa McDonald, sinema zinazoonyesha ni filamu za Marekani, duka kubwa, uwanja wa michezo na shule kwa watoto wa wanajeshi.

Tangu jela hilo ilipoanzishwa, wafungwa 780 wamezuiwa. Mjerumani Murat Kurnaz aliwahi kushikiliwa huko kwa miaka mitano na kuhojiwa.

Katika kitabu alichoandika baada ya kuachwa huru alisimulia kuhusu kuteswa na kwamba kila alipotaka kusali alidai kwamba zilipandishwa sauti kali za muziki zimsumbue.

Shirika la Kimataifa la Amnesty International linalopigania haki za binadamu lililaumu hali ilivyo katika jela hilo na limelitaja jela hilo kuwa ni kashfa kubwa kwa haki za binadamu. Pia Umoja wa Mataifa umeikaripia Serikali ya Marekani kutokana na makosa yanayofanywa katika gereza hilo.

Kuna watu walioshikiliwa Guantanamo kwa muda wa zaidi ya miaka kumi bila ya  kusikilizwa mashtaka ya makosa wanayoshukiwa kuyafanya. Jambo hilo amekiri pia Rais Obama. Siku mbili baada ya kuingia madarakani Januari 2009 alitangaza kwamba anataka kulifunga gereza hilo. Hadi leo bado anasema kwamba gereza hilo ni doa kwa sura ya Marekani, jambo linalowatia moyo  ‘mujahidin’  wenye itikadi kali za Kiislamu.

Jela ya Guantanamo ni mzigo mkubwa kwa walipakodi wa Marekani. Linawagharimu Dola 400 milioni kila mwaka kuliendesha, yaani Dola 2.6 milioni kwa kila mfungwa. Mtu mmoja aliyoko chini ya ulinzi mkali ndani ya jela ya Marekani hugharimu kutumiliwa kiasi ya Dola 34,000 kila mwaka.

Licha ya gharama kubwa, wabunge wa Chama cha Republican na wachache wa kutoka Chama cha Democratic bado wanataka libakie  hivyohivyo.

Mara kadhaa wamepinga kutolewa fedha za kumwezesha Rais Obama aamuru wafungwa wahamishiwe kwenye magereza mengine nchini Marekani. Wabunge hao hawataki zichukuliwe hatua wanazoziita za “kipumbavu” za kuwahamishia Marekani magaidi hao walio hatari.

Kuna wafungwa walioachwa huru wiki chache zilizopita kutoka Guantanamo na sasa wamepatiwa makazi mapya ya kuishi katika nchi kama vile Slovakia, Uruguay na Kazakhstan.

Idadi yao ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya kabla na inasemekana kuna mpango wa kuwasambaza katika nchi nyingine za dunia. Kwa mujibu wa wachunguzi wa mambo ni kwamba mkakati huo utatekelezwa kwa lengo la kupunguza gharama za kuliendesha.

Inaaminika kwamba hata pale karibu wafungwa wote wasiokuwa wa hatari watakapoachiliwa wameachiliwa, bado kutabakia wachache ndani ya gereza hilo.

Hao ni wale wanaokabiliwa na mashtaka kama vile Khalid Sheikh Mohammed aliyeongoza mipango iliyofanikisha mashambulio ya Septemba 11 huko Marekani. Watu wa aina hiyo watatakiwa wajielezee mbele ya mahakama ya kijeshi.

Huenda wakabakia vizuizini maisha yao yote. Haitarajiwi kwamba watakuwa huru. Wao wanaonekana kuwa ni hatari mno, licha ya kwamba hakuna ushahidi uliowazi wa kuwafanya wapatikane na hatia mbele ya mahakama.

Kwa wabunge wa Marekani wa Chama cha Republican wanaamini mahala panapofaa kwa watu hao ni Guantanamo tu na siyo kwingine.