Prime
Hongera Bodi ya Ithibati mwanzo mzuri, ila...
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeanza kazi rasmi na hili ni jambo la kupongezwa. Hii ni hatua muhimu katika kujenga hadhi na weledi wa taaluma ya habari nchini Tanzania.
Hata hivyo, tunapaswa kuwa makini; tusiruhusu bodi hii mpya iwe neema kwa waandishi wakubwa tu, huku ikiwa mwiba kwa waandishi chipukizi au wale wenye vipaji lakini wasiokuwa na vyeti.
Katika tasnia ya habari, mara nyingi waandishi hulalamikia kutothaminiwa kama taaluma nyingine.
Katika mikutano mingi muhimu, waandishi wa habari huachwa nje au hupangiwa kukaa viti vya nyuma, wakati watu wa fani nyingine wakipewa heshima kubwa. Hili ni jambo la kufedhehesha na linahitaji marekebisho.
Kwa kuanzishwa kwa JAB, kuna matumaini ya kurejesha heshima ya taaluma na wanahabari wenyewe kwa ujumla, lakini hilo litafikiwa ikiwa bodi hii itafanya kazi yake kwa haki, usawa na uelewa wa mazingira halisi ya sekta hii.
Na hii ni fursa ya kipekee ya kushirikiana, kuishauri na kuiimarisha Bodi hii ya Ithibati kusudi kiwe chombo cha kweli cha kuendeleza taaluma ya habari na si cha kuibagua.
Licha ya kutarajia mema mengi kutoka kwa bodi hii, lakini katika Ibara ya 5 ya sheria mpya inaeleza kuwa Mkurugenzi wa Habari atasajili vyombo vya habari vya kuchapisha tu, lakini siyo vya utangazaji kama redio, televisheni au mitandao ya kijamii.
Hii inaleta mgawanyiko usio wa lazima kati ya vyombo vya habari, kwa sababu lengo letu siku zote limekuwa kuunganisha wanahabari wote bila kujali jukwaa lao.
Kwa sasa, magazeti yako chini ya Wizara ya Habari, huku redio, televisheni na mitandao ya kijamii vikiwa chini ya Wizara ya Mawasiliano na TCRA.
Mgawanyo huu wa kimamlaka unapaswa kuangaliwa upya ili kuhakikisha kuna mwamvuli mmoja wa kitaaluma unaowaunganisha wanahabari wote.
Bodi ya Ithibati imekuja na lile hitaji la mwandishi wa habari lazima awe na vyeti vya kitaaluma kwa kiwango cha Diploma, hivyo ndivyo sheria mpya ya habari inataka mwandishi wa habari lazima awe na angalau diploma ya habari. Hitaji hili ni neema kwa waandishi wa habari wa magazeti na mwiba kwa watangazaji na online media.
Kwanza mimi kama mwandishi wa habari mkongwe, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100 ili kujenga heshima ya tasnia ya habari kama taaluma zingine za wanasheria, madaktari, mainjinia na nyingine zote.
Lakini uandishi wa habari na utangazaji, zaidi ya taaluma, pia ni kipaji, lakini pamoja na kipaji, ili mtu awe mwandishi au mtangazaji, lazima apite shule ya habari kupigwa angalau msasa tuu wa certificate.
Nilipoajiriwa Redio Tanzania (RTD), tulikuwa tunapimwa kipaji tuu, halafu mafunzo ya kazi unayapatia kazini, kupitia mafunzo kazi kwa kozi ya Radio Induction.
JAB imewaweka waandishi wote wa habari kwenye tenga moja la diploma!
Hii sio sawa, hata baharini na kwenye maziwa, kuna samaki wakubwa papa na nyangumi, kuna samaki wa kati, sato, sangala na kambale na kuna samaki wadogo dagaa! Hawa wote ni samaki, lakini kuwaweka wote kwenye tenga moja kubwa hatuwatendei haki hawa dagaa. Mfumo uliopo sasa wa kuwaweka wanahabari wote kwenye “tenga” moja la diploma, hauwatendei haki wale chipukizi au wenye vipaji bila vyeti. Kama kwenye bahari kuna papa, nyangumi, kambale na dagaa, ndivyo ilivyo kwenye uandishi wote ni sehemu ya tasnia hii, wanapaswa kutambuliwa kwa nafasi zao.
Mfano tasnia ya sheria, mtu huwezi kuwa wakili mpaka uwe na shahada ya kwanza ya sheria.
Baada ya hapo unatakiwa ukasome Shule Kuu ya Sheria ndipo usajiliwe na Mahakama Kuu kama wakili.
Kama huna LL.B huwezi kuwa wakili. Kama kwa wanasheria hili limewezekana kwa nini kwa waandishi lisiwezekane?
Wale wenye vyeti wasajiliwa kama waandishi wasaidizi na wengine wote wenye vipaji lakini hawana vyeti, wasajiliwe kama wanaojifunza kazi ya uandishi, wajiendeleze badala ya kuwaondosha ndani ya vyumba vya habari.
Kwa mujibu wa sheria hii, kama nilivyosema mwanzo, hii ni ile ya Newspaper Act ya 1976 iliyoboreshwa, hiyo bodi ya Ithibati isiishie kusajili waandishi wa habari wenye elimu ya kuanzia ngazi ya diploma tu.
Sheria mpya ya habari ni ile ile Newspaper Act ya mwaka 1976 ambayo imefanyiwa maboresho, lakini bado inahusika tu na vyombo vya habari vya kuchapisha (print). Kwa upande wa utangazaji (broadcast), mamlaka husika ni tofauti kabisa, iko chini ya Wizara nyingine na inasimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ni muhimu sana kwa Bodi ya Ithibati kuzingatia kuwa fani ya utangazaji inategemea zaidi vipaji kuliko vyeti. Kuweka sharti kuwa kila mtangazaji lazima awe na diploma, ni kuwanyima fursa wengi wenye vipaji vikubwa, lakini wasio na sifa za kitaaluma.
Baharini kuna papa na nyangumi, sato na sangara, lakini tusisahau kuwa hata dagaa ni samaki na ana haki ya kuishi, si tu kuwa chakula cha samaki wakubwa.
Hawa “dagaa” wa fani ya habari, waandishi na watangazaji wasio na diploma ndio wanaoendesha radio nyingi na majukwaa ya mitandao ya kijamii nchini.
Kuwawekea vizuizi ni kuzima ndoto na vipaji vyao. Ni vyema wakapewa fursa kwa njia mbadala ya usajili wa dirisha dogo linalotambua vipaji, si vyeti tu.