Jinsi ya kuboresha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/50

Kwa sasa Taifa letu linaandaa Dira ya tatu ya Taifa ya Maendeleo. Ikumbukwe kuwa Dira ya kwanza ilianza mwaka 2005 – 2019, ya pili mwaka 2020 – 2025 na ya tatu ni mwaka 2025 – 2050.

Dira ni nini? Dira ni mwongozo au taa ya kutuonyesha ni nini cha kufanya kwa mahali gani, kwa jinsi gani, kwa wakati gani na kwa watu gani.

Suala la muda ni la makubaliano kati ya wanajamii husika, lakini wataalamu wanapendekeza Dira iwe ya malengo ya muda mfupi na mrefu. Kwa muda mfupi ni miaka mitano mitano na kwa muda mrefu ni miaka 25, 50, 75 hadi 100.

Dira ya kwanza ya maendeleo ya Taifa iliishia mwaka 1999 na ya pili ilianza mwaka 2000 mpaka leo. Aliyeanzisha Dira ni Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, kabla ya hapo Taifa lilikuwa linaendeshwa na ilani ya CCM.
Ninatoa pongezi kwa Hayati Mkapa kwa kutuanzishia Dira wakati wa awamu yake ya pili ya uongozi.

Pamoja na mafanikio ya Dira katika vipindi viwili viwili vya miaka 25, Dira hizi mbili hasa ya pili (2000 – 2025) ilikuwa na malengo matano ambayo ni haya yafuatayo:
Lengo la kwanza, ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania. Pili, kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja. Tatu, kujenga utawala bora. Nne, kuwepo kwa jamii iliyoelimika vema na inayojifunza. Tano, kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.

Licha ya malengo mazuri ya Dira hizi, bado changamoto zilikuwepo. Baadhi ya changamoto hizo, kwanza, ni ajira kwa vijana. Dira zote hizi mbili zimeshindwa kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya ajira kwa vijana.

Uwezo wa Serikali kuajiri wahitimu wote wa vyuo kila mwaka ni mdogo sana. Idadi ya wahitimu wa elimu ya sekondari, vyuo na vyuo vikuu inazidi kuongezeka kila siku na takwimu za sasa zinakadiriwa kati ya vijana 600,000 hadi 800,000 kila mwaka wanaingia kwenye soko la ajira.

Wahitimu hao ni miongoni mwa asilimia 54 ya watu wasio na ajira wenye umri chini ya miaka 25 katika Taifa la 10 duniani kwa kuwa na kundi kubwa la vijana. Hii ni kwa mujibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Restless Development, yenye makao yake makuu nchini Uingereza.

Hivyo, Dira ya 2025 – 2050 inatakiwa kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi, zikiwa ni pamoja na kuiboresha mitalaa ya elimu ya ngazi zote ili kuwawezesha wahitimu kujiajiri wenyewe, lakini pia kwa wale watakaoajiriwa.

Lazima Serikali ibadilishe mfumo wa ajira kutoka kuwa za kudumu (pension base system) hadi kuwa ajira za mkataba ili kuwawezesha wahitimu kuajiriwa kwa awamu na kuwawezesha wahitimu wote watakaoshindwa kujiajiri kuajiriwa Serikalini na mashirika ya Serikali kwa mkataba badala ya ajira za kudumu ambapo mwisho wa ajira hizo ni miaka 65.

Napendekeza kila ajira Serikali na kwenye mashirika yake iwe ni miaka 10 yenye mikataba miwili ya miaka mitano mitano. Na kwa wale wa nafasi za juu za utawala wataingia mkataba wa miaka sita sita, kwa vipindi viwili itakuwa miaka 12.

Ili kutokuruhusu mashirika na Serikali kuu kuyumba, pamoja na uboreshaji wa mitalaa pia Serikali iondoe mpango wa ajira kwa pensheni kwa ajira za hadi kustaafu katika umri wa miaka 60 – 65.

Suala la tatu ni Serikali kujiandaa kulipa mishahara toshelezi ili kila atakayepata ajira ndani ya miaka 10 – 12 basi apate malipo ya kumwezesha kuendesha maisha yake. Hapa Taifa litaendelea kwa kasi na elimu itaendelea kuwa na thamani.

Mishahara iwe inayokidhi na kuendesha maisha ya watumishi kwa miaka 10 – 12. Kutengeneza ajira litakuwa na ufanisi mkubwa, kwani watumishi watakaokuwa wameshindwa kupata mikataba ya kuendelea, watalipwa stahiki zao na kwa wale ambao watapata mkataba wa pili na wa mwisho nao watalipwa stahiki zao.

Tunategemea Serikali itaendesha mafunzo kwa tasnia zote nchini kuhusu elimu ya ujasiriamali ili wale ambao wataamua kujiajiri, basi waanzishe biashara au shughuli zao mara baada ya kumaliza masomo.

Kuhusu mitaji, Dira ya mwaka 2025 – 2050, napendekeza Serikali ianzishe benki maalumu kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali vijana wanaomaliza shule ya msingi au sekondari, vyuo vya kati, vyuo vikuu vya ndani na nje.

Benki ya wajasiriamali ikishirikiana na halmashauri za wilaya husika, ninaamini kuwa kwa kufanya hivyo tutapunguza ombwe la vijana kukosa ajira kwa Dira ya Taifa ya mwaka 2025 – 2050.

Innocent Siriwa ni Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ADC, anapatikana kwa 0782720088.