Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Job Ndugai alikuwa baridi, vuguvugu na wa moto vilevile

Ni Mtanzania aliyepanda madaraja hadi kuwa kiongozi mkuu wa mhimili mama wa nchi – Bunge. Mzalendo aliyevalia njuga kashfa ya ufisadi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na akaunti ya Escrow, alipokuwa Naibu Spika.

Spika wa Bunge aliyeunganisha kambi zote na kujenga sauti ya pamoja ili kuisimamia Serikali. Spika wa Bunge, aliyeufanya mhimili mama, kufanya kazi chini ya Serikali. Spika mcheshi, lakini mwenye jazba na hamaki za haraka.

Spika wa Bunge aliyekosa usawa. Uamuzi wake mara nyingi uliacha maswali. Kiongozi mwenye uthubutu wa kuzungumza mawazo yake bila kujali misimamo ya mifumo. Mwanachama na shabiki kindakindaki wa Simba. Ndivyo naweza kueleza kwa ufupi wasifu wa Job Yustino Ndugai.

Alionya nchi kuendeshwa kibabe, lakini yeye aliongoza Bunge kibabe. Alitania na kutabasamu na wapinzani, lakini ni yeye aliyewaonyesha cha moto wapinzani. Alikuwa Spika wa Bunge wa halijoto zote; moto, vuguvugu na baridi kwa wakati mmoja.

Mkutano wa Sita wa Bunge la 11, uliohitimishwa Februari 10, 2017 bungeni, Dodoma ulibeba tafsiri kuwa Bunge lilikuwa moja na kila mbunge alikuwa na haki pamoja na hadhi sawa anapokuwa kwenye kazi yake ya kuwawakilisha wananchi wa jimbo lake.

Siku chache kabla yake, wabunge wa upinzani walisusia kikao cha Bunge kilichoongozwa na aliyekuwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, wakidai waliburuzwa, walipokuwa wanataka Bunge lijadili kitendo cha hadhi yake kuingiliwa na Serikali kiasi kwamba wabunge wanakamatwa bila hata uongozi wa Bunge kupewa taarifa.

Kauli za Job Ndugai zilizotikisa

Mtoa hoja hiyo aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, aliwatolea mfano waliokuwa wabunge, Godbless Lema (Arusha Mjini, Chadema) na Tundu Lissu (Singida Mashariki, Chadema), waliokamatwa bungeni na kuwekwa mahabusu bila uongozi wa Bunge kupewa taarifa.

Zitto pia alimtolea mfano aliyekuwa Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali ambaye alihukumiwa kifungo jela miezi sita, lakini Bunge halikuandikiwa barua na Mahakama, kueleza kuhusu uamuzi ambao iliuchukua.

Tulia alikataa hoja hiyo kujadiliwa bungeni kwa maelezo kuwa, Spika wa Bunge hupaswa kuarifiwa ili atoe ruhusa ya kukamatwa mbunge, hivyo tuhuma za kina Lissu na Lema, vilevile hukumu ya Lijualikali ni mambo ambayo hayakuhitaji kibali cha spika.

Hata hivyo, Februari 10, 2017, wakati Ndugai alipokuwa anatoa hotuba fupi ya kuhitimisha mkutano wa sita na kuahirisha Bunge, alisema wabunge wasikamatwe bila yeye kupewa taarifa.

Alisema kumkamata mbunge bila yeye kujua kunaweza kusababisha kushindwa kufanyika shughuli za kitaifa bungeni, kwa sababu wakati mwingine ili masuala yapite kwenye kamati huhitaji akidi, hivyo anapokosekana hata mbunge mmoja huweza kusababisha shughuli za kibunge zikwame.

Kauli hiyo ilisababisha msisimko na uungwaji mkono wa wabunge wote, hasa wapinzani ambao siku zote wao ndio huonekana waathirika wa kukamatwa mara kwa mara. Hapa Ndugai alidhihirisha kwamba alikuwa na uwezo wa kuongoza Bunge na kuwalinda wabunge dhidi ya mihimili mingine (Serikali na Mahakama).

Pamoja na Ndugai kuelekeza wabunge wasikamatwe bila kupewa taarifa, alionya pia kuwa nchi ikiendeshwa kibabe kutatokea uharibifu. Alitaka kuwepo maelewano badala ya Bunge na Serikali kuonyeshana ubabe, jambo ambalo alisema lingeweza kuharibu nchi.

Pamoja na hoja hiyo ya kupinga ubabe, Ndugai aliweka rekodi ya kuwa Spika wa Bunge aliyewafurusha bungeni wabunge wengi wa upinzani, ikiwemo kuwaadhibu kwa kuwafungia vikao hata mikutano kadhaa. John Mnyika, Zitto, Lissu, Lema, Yosepher Komba ni miongoni, kwa kutaja wachache.

Ndugai akiwa amekalia kiti cha Spika alimtoa nje ya ukumbi aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Chadema, Yosepher, aliyekuwa akilalamikia kudhalilishwa na mbunge Jackline Msongozi (CCM). Msongozi alisema Yosepher alikuwa akipitia unyanyasaji wa kingono Chadema. Ndugai alimnyima Yosepher fursa ya kujitetea, kisha akamtoa nje.


Baridi na moto

Aprili 3, 2019, Ndugai akiwa kwenye kiti aliamua kutumia mamlaka yake yanayolindwa na siwa kumshughulikia Lema, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini.

“Niwaambie waheshimiwa wabunge, Spika Ndugai haogopi kabisa. Wanaofikiri sisi ni dhaifu, sisi siyo dhaifu, nilishasema na nikarudia na kurudia. Yeyote anayetaka kuingia kwenye 18 hiyo, sisi tupo tayari,” alisema Ndugai, akitangaza dhamira ya kumchukulia hatua Lema.

Ndugai alisema Lema alipelekwa Kamati ya Maadili ya Bunge kama sehemu ya utaratibu, akiwa na maana ilikuwa lazima ashughulikiwe. Akasema mwingine yeyote ajitokeze na angeonyeshwa kuwa Bunge la 11 halikuwa dhaifu. Kisha, Ndugai alitaja fedha anazodaiwa Lema kuwa ndiyo chanzo.

“Yapo mambo huwa hatusemi, lakini tuseme kidogo. Mheshimiwa Lema tangu aje hapa bungeni amekopa milioni 644 (Shilingi). Useme aaah, useme eeeh, ndiyo hivyo. Ameshalipalipa, sasa anadaiwa milioni 419. Huu ni msongo wa mawazo,” alisema Ndugai.

Alipokuwa anataja madeni ya Lema bungeni, ilitokea hali ya kushangilia kwa waliofurahi, kuguna na kuzomea, kwa ambao hawakupendezwa na Ndugai kusema hadharani mambo binafsi ambayo ni siri, hapo Ndugai alifoka: “Nimekuona Esther Matiko toka nje. Kusanya vitu vyako, toka nje. Sasa hivi.”

Ndugai akiwa mkuu wa Bunge, aliweka rekodi ya kuwa Spika wa kwanza kuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukamatwa. Ndugai alitoa maagizo hayo baada ya aliyekuwa CAG, Profesa Mussa Assad, kunukuliwa akisema Bunge lilikuwa dhaifu, maana ripoti zake zilionyesha kasoro za kihesabu serikalini, lakini mhimili huo haukuchukua hatua za kiwajibu.

Ndugai akiwa Spika, hakuheshimu falsafa ya “Trias Politica”. Mwanafalsafa wa Ufaransa, Charles de Montesquieu akaita ni roho ya sheria (spirit of the laws). Kwamba, katika kila dola lazima kuwepo mgawanyo wa mihimili mitatu; Serikali, Bunge na Mahakama ambayo misuli yake haiingiliani.

Bunge ndiyo timu ya wananchi kuhakikisha masilahi ya watu yanalindwa. Bunge hutakiwa kukabana na ‘Timu Serikali’ ili kinachoamuliwa na kutendwa na Serikali, kinakuwa ni kwa masilahi ya nchi na watu wake.

Spika wa Bunge ndio nahodha wa timu ya wananchi na kazi yake ni kuwaongoza wachezaji wenzake (wabunge) ili kuibana timu Serikali. Sasa Ndugai akiwa nahodha, aliamua kuwa swahiba wa kiongozi wa timu Serikali.

Septemba 7, 2017, Rais John Magufuli alipopokea ripoti mbili za kamati teule za Bunge zilizochunguza shughuli za uchimbaji na biashara ya Tanzanite na almasi, alisema Ndugai alimpigia simu alipotaka kuteua wajumbe wa kamati.

Rais Magufuli alisema, Ndugai alimweleza jinsi alivyopata wakati mgumu kuteua wajumbe wa kamati hizo. Hapa Ndugai alifungisha. Kiongozi wa Bunge ni mwiko kujadili na kiongozi wa Serikali muundo wa wajumbe wa kamati za kuikagua Serikali.

Ndugai anafahamu kuwa taasisi za Serikali na Bunge hazipaswi kutengeneza timu ya pamoja. Bunge na Serikali kuwa timu moja ni usaliti wa desturi za mifumo ya mihimili ya dola, dhambi kubwa iliyopo hapo ni kuisaliti Katiba. Ukishaisaliti maana yake umewasaliti wananchi.

Hata kama Ndugai alikuwa na nia njema kiasi gani, kitendo tu cha kubainika alimpigia simu Rais Magufuli ili kupata mawazo yake juu ya muundo wa kamati ni kushusha heshima na hadhi ya Bunge. Ni vigumu kwa wananchi kuamini kama Bunge linatimiza wajibu wake sawasawa dhidi ya Serikali.

Ndugai alifahamu kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni la uga mmoja wa mijadala (unicameral), hivyo hoja na ripoti zote za kibunge husomwa na kuwasilishwa kwa wabunge wote, kisha kujadiliwa na kuweka maazimio inapobidi.

Ni kipindi Ndugai akiwa Spika, ndipo Bunge liliandika rekodi kwa kuunda kamati teule za kuchunguza uchimbaji, biashara na mikataba ya almasi na Tanzanite, kisha badala ya ripoti kusomwa na kujadiliwa bungeni, ziliwasilishwa kwa Rais. Ndugai alilifanya Bunge kuwa kama idara ya Serikali, badala ya mhimili unaojitegemea.


Halijoto za Ndugai

Ndugai alikuwa mbunge mzoefu. Aliingia bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, alitumikia jimbo la Kongwa kwa miaka 25. Alikuwa mbunge wa kawaida mwaka 2000 hadi 2005, akawa mwenyekiti wa vikao vya Bunge (2005 – 2010), Naibu Spika (2010 – 2015) na Spika (2015 – 2022).

Uchaguzi wa ndani CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, Ndugai alishaongoza kura za maoni jimboni Kongwa, Mungu angemruzuku uhai wa kuendelea, pengine angehudumia jimbo hilo na Bunge la Tanzania kwa miaka 30. Hata hivyo, Mungu hakumkadiria uhai wa kuendelea.

Agosti 6, 2025, Ndugai alivuta pumzi ya mwisho. Alizaliwa Julai 21, 1963. Hesabu zinaonyesha kuwa kikokotoo chake cha uhai ni miaka 62, miezi sita na siku 16. Uhai wa Ndugai umekuwa pungufu ya miaka mitano, kutoka kadirio la wastani wa maisha ya Mtanzania kuwa miaka 67, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ndugai amekuwa bungeni chini ya maspika watatu, walioongoza Bunge kwa umahiri mkubwa; Pius Msekwa (Bunge la Nane), Samuel Sitta (Bunge la Tisa) na Anne Makinda (Bunge la 10). Hata hivyo, Bunge la 11 aliloliongoza yeye, linakosolewa kwa kushindwa kuiwajibisha ipasavyo Serikali.

Katika halijoto tatu; baridi, vuguvugu na moto, Ndugai anatajwa kuwa baridi mno dhidi ya Serikali iliyoongozwa na Rais wa Tano, Dk John Magufuli. Alichagua kuliondolea meno Bunge ili asilumbane na Serikali, vilevile kutabasamu uso kwa uso na utawala.

Ndugai alikuwa wa baridi nyakati za matendo ya kuogofya, kupotea kwa watu. Matukio maarufu ya kutoweka kwa aliyekuwa kada wa Chadema, Ben Saanane, mwandishi wa habari, Azory Gwanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye, kunyakuliwa na kuuawa watu Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Ndugai aliliongoza Bunge kunyamaza.

Maiti zilikutwa kwenye mifuko, fukwe za Bahari ya Hindi na kando mwa Mto Ruvu, lakini Ndugai hakuunda japo kamati teule ya Bunge kuchunguza. Kadhalika, kupigwa risasi na kuuawa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini. Ndugai alibaki baridi. Bunge nalo lilipoa.

Ndugai alikuwa vuguvugu Lissu alipopigwa risasi Septemba 7, 2017. Kwanza alionyesha kusimama na Lissu kuhakikisha maisha yake yanaokolewa. Alichangisha wabunge na alifanya kila linalowezekana mwanzoni ili mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki apone.

Baadaye Ndugai alibadilika na kuwa wa moto. Alisimama mbele ya picha, wakati Lissu akilalamika kunyimwa stahiki zake za matibabu na Ndugai ndiye aliyehitimisha ubunge wa Lissu, kwa kutangaza jimbo la Singida Mashariki kuwa wazi, kwamba hakuwa na taarifa za mahali mbunge alikuwa, wakati Taifa lilitambua kilichotokea na Lissu alikuwa kwenye matibabu Ubelgiji.

Kuingiza wabunge 19 wa viti maalumu Chadema na kulazimisha kuwapa uhalali bila ridhaa ya uongozi wa chama. Kuruhusu hoja za kejeli dhidi ya viongozi wa upinzani, kama vile aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuitwa mlevi wakati alipodai kushambuliwa na kuteguka mguu. Ni sehemu ya rekodi zilizoachwa na Ndugai.

Ndugai alikuwa wa moto kwa wapinzani na aliwahenyesha kwa kuwatimua alivyojisikia. Alipoingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan, ghafla Ndugai akataka kuwa wa moto kwa Serikali, kwa kuituhumu kuwa inakopa hadi kuiweka nchi kwenye hatihati ya kuuzwa. Kauli hiyo ikamgharimu uspika wake.

Baada ya kujiuzulu uspika, alitangaza asingegombea tena ubunge. Hata hivyo, baadaye alibadili uamuzi na kuchukua fomu. Alikuwa mwema kwa aliowatendea mema, wa tofauti kwa waliokinzana naye. Ni binadamu aliyesimama katika halijoto zote; moto, vuguvugu, baridi.